Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, linamshikilia askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Friday Kumingi (29), kwa kushirikiana na majambazi kufanya matukio ya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema askari huyo alikamatwa kwenye msako uliofanywa na jeshi hilo Machi 3, mwaka huu.
Alisema askari huyo wa JWTZ Kikosi cha 36KJ Kibaha Msangani, alipohojiwa na polisi baada ya kukamatwa alikiri kumiliki silaha mbili kinyume cha sheria.
Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo aliwajulisha askari hao kuwa huwa anazihifadhi silaha hizo nyumbani kwa mke wake mdogo mtaa wa Muheza Kibaha, Pwani na huzitumia kufanyia matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Pwani.
Alisema baada ya mahojiano, askari hao na mtuhumiwa walifika kwenye nyumba hiyo na kufanikiwa kukamata silaha aina ya AK 47 yenye namba NM174844 ikiwa na risasi 20.
Mambosasa alisema askari walikuta boksi moja likiwa na risasi 27, bastola moja yenye namba 3249 ikiwa na risasi saba ndani ya magazine na risasi tatu za silaha aina ya G3.
Aidha, Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo alikubali kuwaonyesha wenzake watatu anaoshirikiana nao katika matukio hayo na askari walipofika kwenye nyumba wanayoishi watuhumiwa walianza kukimbia.
Aidha, Mambosasa alisema baada ya watuhumiwa hao kuanza kukimbia kupitia mlango wa nyuma, askari walianza kurusha risasi hewani kuwaamuru wasimame, lakini walikaidi.
"Walikaidi na ndipo askari walipowafyatulia risasi za miguu ambazo ziliwajeruhi na kufariki dunia wakiwa njiani kupelekwa hospitali," alisema Mambosasa bila kutaja majina ya watu hao.
Social Plugin