Watoto pacha wawili kati ya watatu waliozaliwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita wamefariki dunia wakiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa uchunguzi.
Watoto hao wawili waliokuwa wameungana katika eneo la kifua walipoteza maisha kwa nyakati tofauti kwani mmoja alifariki dunia wakati wakivuka kivuko cha Busisi wilayani Sengerema, huku mwingine akipoteza maisha mara tu baada ya kufika kwenye lango la hospitali hiyo.
Muuguzi mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Geita, Charugamba Jackson alisema jana kuwa, kwa mujibu wa muuguzi aliyekuwa akiwapeleka watoto hao Bugando, mtoto wa kwanza hali ilibadilika wakiwa kwenye kivuko na mapigo ya moyo kuanza kushuka.
“Wakiwa njiani muuguzi aligundua hali ya mtoto mmoja imebadilika na mapigo yake yalianza kushuka na anapumua kwa shida, alijitahidi kumsaidia lakini alifariki walipovuka,” alisema Charugamba.
“Alimtaka dereva kuongeza mwendo wa gari, lakini kwa bahati mbaya walipofika getini mtoto mwingine naye alifariki.”
Na Rehema Matowo, Mwananchi
Social Plugin