Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao
Vijana wawili Rosemary Embasy (17) na Yohana Petro (19) wamenusurika kufa baada ya kunywa vidonge vingi na unga wa betri za remote na maji kutokana na mgogoro wa mapenzi ulioigubika familia ya Petro Dalali (41) mkazi wa kijiji cha Mwime ya Ilindi kata ya Zongomela wilayani Kahama. Anaripoti Kadama Malunde.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao tukio hilo limetokea Machi 18,2019 majira ya saa ya saa tisa alasiri Kijiji cha Mwime ya Ilindi.
Akisimulia kuhusu tukio hilo,Kamanda Abwao amesema siku ya tukio hilo, binti aitwaye Rosemary Embasy (17) mkazi wa Mwime alijaribu kujiua kwa kunywa vidonge vingi pamoja na unga wa betri za remote uliochanganywa na maji baada ya kumuona mtoto wa mama yake mkubwa aitwaye Yohana Petro (19) na yeye amekunywa vidonge vingi kwa lengo la kujiua.
“Chanzo inadaiwa kuwa wazazi wa Yohana Petro wamekuwa na mgogoro ambapo mama yake aitwaye Magdalena Lucas (39), amekuwa akimtuhumu mtoto wa mdogo wake yaani Rosemary Embasy kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mume wake . Pia baba yake Yohana Petro aitwaye Petro Dalali (41 amekuwa akimtuhumu mtoto wake Yohana Petro kuwa anatoka kimapenzi na Rosemary Embasy ambaye ni mtoto wa shemeji yake”,
“Ndipo tarehe 18/03/2019 majira ya saa nne asubuhi Yohana Petro alifika nyumbani kwa Rosemary Embasy na kuingia ndani kisha kunywa vidonge vingi ambapo Rosemary Embasy baada ya kuona hivyo na yeye alimeza vidonge vilivyobaki na kuponda unga wa betri ndogo kisha kunywa pamoja na maji”,ameeleza Kamanda Abwao.
Amesema tayari baba wa familia Petro Dalali na mkewe aitwaye Magdalena Lucas, na Dominic Magoha (31) wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Aidha amesema Rosemary Embasy na Yohana Petro wanaendelea na matibabu hospitali ya Halmashauri Mji wa Kahama wakiwa chini ya ulinzi na hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda Abwao ametoa wito kwa wananchi, pale inapotokea migogoro ama matatizo ya kifamilia kutojichukulia maamuzi ya kujidhuru, kwani ni kosa kisheria, badala yake waripoti kwa mamlaka za kisheria/ kiushauri ili kutatua matatizo yanayotokea.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin