Kijiji cha Mafi Dove kilichopo kusini mwa nchi ya Ghana, chenye wakazi takribani 5000, lakini hakuna kati yao aliyezaliwa kijijini hapo kutokana na mila inayokataza kuzaliwa watoto.
Kama ilivyo kwa vijiji vingi kuwa na tamaduni zao, kijiji cha Mafi Dove kimekuwa na mila hii ambayo imegeuka kuwa mwiba kwa wanawake, kwani wanapokuwa wajawazito na kutaka kujifungua, hulazimika kuondoka kijijini hapo na kwenda kijiji cha jirani, ili aweze kujifungua mtoto wake na kisha kurudi.
Mwananchi wa kijiji cha Mafi Dove asimulia.
“Wakati mababu zetu walipokuja katika ardhi hii, sauti kutoka mbinguni ilisikika ikiwaambia hapa ni mahali patakatifu, hivyo ukitaka kuishi ni lazima ufuate masharti, sheria ya hapa ni hakuna mtu anayeruhusiwa kuzalia hapa”, alisikika moja wa wakazi wa kijiji hicho alipohojiwa na BBC.
Hiyo ni moja tu ya mila za ajabu zinazopatikana kijijini hapo, kwani zipo mila zingine ambazo pia wakazi wake wanazitekeleza mpaka sasa, ikiwepo kutofuga mnyama yeyote au hata ndege wa kufuga, na pia hawaruhusiwi kuchinja mnyama yeyote.
Lingine la kushangaza zaidi katika kijiji hicho ni kwamba hakina kaburi hata moja, kwani pia hawaruhusiwi kuzika wafu, hivyo mtu akifa hulazimika kwenda nje ya kijiji ili kuzika ndugu yake.
Mpaka sasa mila hizo zinaendelea kutekelezwa, huku baadhi ya wanawake wakilalamika kupata shida kubwa hususan juu ya mila ya kutojifungua kijijini hapo, kwani hulazimika kutembea umbali mrefu kwenda kijiji kingine kujifungua.