Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe, leo Jumatano Machi 13, 2019 ametoa ujumbe kwa viongozi na wabunge wa chama hicho akiwashukuru baada ya kukaa rumande kwa siku 104.
Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko walikaa mahabusu ya Segerea tangu Novemba 23, mwaka 2018 hadi Machi 7, 2019 baada ya kushinda rufaa ya dhamana waliyoikata Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika ujumbe huo, Mbowe ameanza kwa kusema, “Naomba niwashukuru sana wale wote walioshiriki nasi kupigana, kulia na hata kuimarishana kwa njia mbalimbali katika kipindi chote cha miezi mitatu na nusu tuliyoishi gerezani.”
“Natambua na kuheshimu mno ushiriki wenu kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na sala, ushauri, huduma ya chakula, michango ya fedha, solidarity support mahakamani na zaidi walioweza kutenga muda wao na kuja kututembelea na kutufariji gerezani Segerea kulikoambatana na zawadi mbalimbali vikiwemo vitabu na magazeti, matunda, maji, juisi na hata machozi!!!.”
“Nitambue kipekee kazi kubwa na ya kutukuka iliyofanywa na Mawakili Wasomi waliounda defence team yetu!! You were great all the way through!!”
Mbowe ameendelea kusema, “nitoe shukrani vilevile kwa wale wote waliotoa support kwa familia zetu na hata kututunzia na kujenga kwa njia mbalimbali majimbo yetu ya uchaguzi ikiwemo kazi ya Chadema ni Msingi.”
“Kwa wale walioshindwa vyote hivyo, watambue kwa dhati nawapenda na kuwaombea yote yaliyo mema... au kama wapo wengine waliokwazika kwa njia moja au nyingine.... pia nichukue fursa hii kuwaomba msamaha na kuitaka amani miongoni mwetu!!,” amesema
Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai amesema, “niwape pole nyingi wenzetu wote waliokumbwa na masahibu mbalimbali katika kipindi chote hiki!! Tuimarishwe zaidi katika mapito haya ili itimie kauli ya “kesho yetu kuwa bora kuliko jana.”
Mbarikiwe sana!!
Social Plugin