Na Bakari Chijumba, Mtwara.
Mbunge wa CUF anayewakilisha Jimbo la Tandahimba Mkoani Mtwara, Katani Ahmed Katani, amesema kwa sasa hawezi kusema kama anaunga mkono maamuzi ya maalim Seif Ama Laah! Hadi pale atakapopata ushauri kutoka kwa wapiga kura wake.
Akizungumza mapema leo Asubuhi kupitia Pride Fm Radio (Mtwara), Katani ambaye ni mmoja ya wabunge waliokuwa wanaiunga mkono CUF ya Maalim Seif, amesema wapiga kura wake ndio waliompa dhamana hivyo wana nafasi kubwa ya kumpa muelekeo.
"Ukiona mbuzi kapanda juu,kuna aliyempandisha,Mimi nafasi ya ubunge sikufika tu,wapo wana Tandahimba walionipandisha..Kwahiyo kwa sasa siwezi sema naunga mkono alichokifanya Maalim Seif Sharif Hamad bila kurudi kwa wapiga kura wangu ili wanipe muelekeo" amesema Mbunge Katani na Kuongeza ;
"Napenda sana ushauri wa wapiga kura wangu,siwezi fanya maamuzi bila kurudi kwa walionipa dhamana, watakachonielekeza ndicho nitakachofanya..Hata wakisema Katani kwa tulipofika pumzika siasa ufanye vitu vingine nitaacha,sikuzaliwa nikiwa Mbunge"
Tayari hii Leo 19 March 2019, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemkabidhi maalim Seif Hamad kadi namba moja ya ACT Wazalendo ambayo imeshalipiwa kwa kipindi cha miaka 10.
"Mimi nina kadi namba nane.. Kadi namba moja kuna mtu aliiwahi na kwa heshima kadi hii imekwenda kwa Maalim Seif" amesema Zitto.
Shughuli ya kukabidhi kadi hizo imefanyika, makao makuu ya ACT- Wazalendo yaliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Viongozi wengine ambao wamekabidhiwa kazi ni Ismail Jussa, Mbalala Maharangande na Sheweji Mketo.
Maalim Seif ambaye Alikuwa katibu Mkuu CUF Taifa, alitangaza rasmi kujiunga chama cha ACT Wazalendo,pamoja na wafuasi wake jana 18 March 2019, muda mfupi baada ya Mahakama,kukubaliana na maamuzi ya msajili ya kumtambua Prof. Lipumba kama Mwenyekiti halali CUF.
Social Plugin