Mchungaji Alph Lukau wa Afrika Kusini ambaye alitikisa dunia kwa habari ya kufufua mtu, ameomba radhi wananchi kwa kufanya tukio ambalo limekuwa msumari kwake.
Akizungmza na kituo cha redio cha Power FM cha Afrika Kusini, Mchungaji Lukau amesema kwamba mtu ambaye alionekana akimfufua, alikuwa hajafa kama ilivyosemwa, hivyo anaomba radhi kwa kutosema ukweli tangu awali.
Mchungaji Lukau ameendelea kusema kwamba mtu huyo alionekana kuwa hai kabla hajaletwa kanisani, na ndugu zake huenda walifanya hivyo wakiamini kuwa kuna kitu kinaweza kikatokea kwa ndugu yao ambaye alitangazwa kufariki.
“Kwenye ibada ya Jumapili ya February 24 katikati ya ibada, nilishtuliwa na kuambiwa kwamba kulikuwa na mtu kwenye sanduku, na kabla ya kuinghia kanisani sanduku lilianza kutikisika, ikimaanisha mtu alikuwa hai, nikaenda chini tukafungua sanduku, na mtu alikuwa anapumua, hata mimi nilisema anapumua, anapumua, ikimaanisha kuwa mtu alikuwa hai, nikaanza kumuombea", amesema Mchungaji Lukau.
"Samahani sana kwa uwasilishaji mbaya wa ukweli, mtu alikuwa hajafa na hajawahi hata kuwa mochwari kama ilivyosemwa awali, tulikuwa kwenye nyumba ya Mungu na mimi ni mchungaji tu, lakini samahani hatukuwaambia watu ukweli tangu mwanzo. Nadhani ndugu zake walimleta kanisani wakiamini kuna kitu kinaweza kutokea kwa ndugu yao”, aliendelea kuzungumza Mchungaji Lukau na akiomba msamaha. .
Akiendelea na mahojiano katika kituo hicho cha redio, Mchungaji Lukau amesema kwamba yeye hana uwezo wa kufanya hivyo isipokuwa Mungu ndio anamtumia kufanya hivyo, na kwamba alishawahi kushuhudiwa kuwa alirudisha uhai wa mtoto ambaye alifariki tumboni mwa mama yake baada kumuombea, kutokana na kauli ya daktari kuwa mapigo ya moyo ya mtoto hayapo.
“Naweza kukwambia sina uwezo wowote, sina uwezo wa kufanya chochote isipokuwa iwapo Mungu akinitumia kufanya jambo, tulishakuwa na kesi nyingi kama hizo, kwa mfano kesi ya mtoto ambaye alikuwa amefia tumboni mwa mama yake, mapigo ya moyo hayakuweza kupatikana, lakini baada ya maombi tukaambiwa mtoto yuko sawa”, amesema Alph Lukau.
Wakati huo huo mwanasheria wa kanisa la Alleluia Ministries International ambalo ni la mchungaji huyo, amekanusha taarifa za kulipa mtu aliyesadikiwa kufufuliwa, na kusema kwamba mtu huyo hakulipwa hata senti moja ili kushiriki muujiza huo.
Social Plugin