Shirika la Miracle Corners Tanzania(MCT) kwa kushirikiana na Kampuni ya Colgate Palmolive na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Vyuo vya Tabibu Meno (Mbeya na Tanga) wameadhimisha siku ya afya ya kinywa na meno Duniani.
Maadhimisho haya huadhimishwa kote duniani kila ifikapo tarehe 20 mwezi Machi kila Mwaka. Kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yalianza kuadhimishwa nchini Tanzania mwaka 2014 katika mkoa wa Dar es Salaam.
Kila maadhimisho hubeba kauli mbiu yake ambayo hutumika kuhamasisha watu kutunza afya ya kinywa na meno,ambapo
Kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Sema Ahh :Chukua hatua zinazozingatia afya ya kinywa na meno”.
Maadhimisho haya yameadhimishwa kwenye mikoa miwili ya Mbeya na Tanga ambako Shirika la MCT linafanya kazi zinazolenga afya ya kinywa na meno.
Madhumuni ya maadhimisho hayo ni kutoa elimu ya afya ya kinywa na meno, uchunguzi wa kinywa na meno, kupunguza uwezekano wa meno kuharibika kwa kupaka dawa ya floridi pamoja na kugawa dawa za meno na miswaki kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Katika kuadhimisha siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani, Shirika la MCT limetoa elimu na huduma ya afya ya kinywa na meno zoezi ambalo lilifanyika siku ya Jumatatu hadi Jumatano jijini Tanga na Mbeya.
Kupitia zoezi hilo jumla ya watu 1,226 wakiwemo watu wazima na wanafunzi wa shule za msingi katika jiji la Tanga walifikiwa huku Jumla ya wanafunzi 246 wa shule za msingi jijini Mbeya wamepatiwa huduma siku ya kilele cha maadhimisho tarehe 20 mwezi Machi,2019.
Wataalam mbalimbali wa huduma za afya ya kinywa na meno ikiwa ni pamoja na wanafunzi walio katika mafunzo kwa vitendo kutoka Vyuo vya Tabibu wa meno vilivyopo Tanga na Mbeya wakisimamiwa na wakufunzi wao wameshiriki maadhimisho haya.
Aidha MCT pia imetoa elimu ya afya ya kinywa na meno kupitia vyombo mbalimbali vya habari zikiwemo radio na vituo vya televisheni ambavyo ni Radio Free Africa, Baraka FM, Sweet FM, Bomba FM, TK FM na Tanga Television.
Wanafunzi pamoja na wakufunzi wao kutoka katika chuo cha Tabibu meno Tanga wakiwa katika maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno duniani.
Uchunguzi wa kinywa na meno ukiendelea.
Uchunguzi pamoja na matibabu yakiendelea – Tanga.
Wanafunzi wakipata elimu zaidi juu ya afya ya kinywa na meno.
Joseph Haule ambaye ni mwanafunzi aliyepo katika mafunzo kwa vitendo kutoka Chuo cha Tabibu Meno Mbeya akionyesha njia sahihi ya kupigwa mswaki.
Joseph Haule akiendelea kutoa maelezo kuhusu upigaji sahihi wa mswaki.
Mwanafunzi akionesha njia sahihi ya kupiga mswaki baada kupata elimu.
Wanafunzi wakifurahia zawadi ya dawa ya meno na mswaki kutoka Kampuni ya Colgate Palmolive.
Wa kwanza kushoto ni Mkufunzi kutoka Chuo cha Tabibu Meno Tanga,Dkt. Digna Komba akifuatiwa na Mratibu wa afya ya Kinywa na meno jiji la Tanga Dkt. Gideon Joshua na Afisa Mradi wa MCT mkoa wa Tanga,Sara Mtagwa wakitoa elimu ya kinywa na meno kwa njia ya Radio TK Fm mkoani Tanga.
Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Idara ya kinywa na meno hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya - Dkt. Hery Mwakayoka, akifuatiwa na Afisa Mradi kutoka MCT - Fredrick Meena, Meneja wa Shirika la MCT - Jane Shuma na Mkuu wa Chuo Tabibu Meno Mbeya - Dkt. Ibrahim Kasambala (wa kwanza kulia) baada ya kumaliza kutoa elimu ya afya ya kinywa na meno kupitia Radio Sweet Fm Mbeya.
Picha ya pamoja ya washiriki wa maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno duniani - Mbeya.
Wanafunzi wa Chuo cha Tabibu Meno mkoani Tanga pamoja na wanafunzi wa shule za msingi.
Wanafunzi walio katika mafunzo kwa vitendo kutoka Chuo cha Tabibu Meno mkoani Mbeya wakiwa katika picha ya pamoja.
Social Plugin