NAIBU WAZIRI KANYASU AAHIDI KUBORESHA MAKUMBUSHO YA MWL.NYERERE BUTIAMA


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Constantine Kanyasu amesema Wizara kupitia Taasisi zake imejipanga kukikarabati na kukiendesha Kituo cha Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, kwenye makazi ya Baba wa Taifa wilayani Butiama mkoani Mara.


 Amesema hatua hiyo inalenga kukiboresha kituo hicho ili kiweze  kuwavutia watalii wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.


Akizungumza mara baada ya kutembelea kituo hicho wilayani Butiama mkoani Mara,  Mhe. Kanyasu amesema Makumbusho hiyo  ni hazina ya Taifa kutokana na uwepo wa mikusanyo na historia iliyobeba taswira ya Taifa la Tanzania  kabla na baada ya Uhuru.


Amesema yeye akiwa Naibu Waziri  atahakikisha Makumbusho hiyo inatengewa bajeti ya kutosha ili kuiwezesha kuwa ya kisasa na yenye kuwavutia watalii.


Ameeleza  kuwa nchi mbalimbali duniani ikiwemo China zimekuwa zikiingiza fedha nyingi kupitia Makumbusho za viongozi ambao walikuwa  waasisi wa nchi hizo kama alivyokuwa Mwl.Nyerere.


Amesema sifa aliyokuwa nayo Mwl. Julius Kambarage Nyerere lazima iakisi Makumbusho yake kwa kuwa bora na yenye kuwavutia watalii.


Makumbusho hiyo lazima iwekewe mazingira mazuri ili  iakisi utu na uzalendo wake kwa taifa la Tanzania.
 Aidha, amesema Makumbusho hiyo itafanyiwa utaratibu wa kuwa na watumishi wa kutosha wa kuihudumia.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Makumbusho hiyo, Emamuel Kiondo  amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa  kituo hicho kina watumishi wawili pekee walioajiriwa na  wengine wakiwa  watumishi wa kujitolea.


Aidha, ameeleza kuwa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa vitendea kazi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post