Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAPIGWA RADI BAADA YA KUPOKEA MAHARI YA BINTI YAO

Wakiwa wanajiandaa kupiga vigeregere baada ya mazungumzo ya mahari ya binti yao kumalizika, ndugu wanne wa familia moja wamenusurika kifo baada ya kupigwa na radi.

Ndugu hao wakiwa kwenye sherehe ya kupokea mahari ya binti yao Machi 21, saa kumi jioni, walijikuta wakipigwa radi ambayo iliwaacha na majeraha katika miili yao.

Tukio lilitokea katika kijiji cha Sima wilayani Sengerema.

Kaimu ofisa mtendaji wa Kata ya Sima, Benedicto Welo aliwataja ndugu hao kuwa ni baba wa binti anayetarajiwa kuolewa Thomas Ngoshiwabhanya (42), mama Rejina Kube (32), shemeji wa binti, Jerina Majige (30) na Neth Thomas (15).

Alisema radi hiyo ilisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa saa tatu na kwamba majeruhi hao kwa sasa wanapatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bahati Mhangwa alisema tukio ni la kwanza kutokea na kusababisha taharuki kijijini hapo.

Shuhuda wa tukio hilo aliyekuwa miongoni mwa waalikwa wa sherehe hiyo ofisa mtendaji wa kijiji cha Sima, Yusuph Mang’ombe alisema wakiwa katika mazungumuzo ya mwisho ghafla radi ilipiga na kukatisha shughuli hiyo.

“Tulikuwa tukijiandaa kupiga vigeregere mara tuliona radi ikipiga na kila mtu kuzimia, walipozinduka watu wanne hali zao zilikuwa mbaya na kukimbizwa hospitali kwa matibabu,’’ alisema Mang’ombe.

Mgaga mkuu wa hospitali hiyo, Mary Jose alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri.

Alisema watu waliopata majeraha makubwa ni Ngoshiwabhanya aliyejeruhiwa sehemu za siri na Kube aliyeumia katika paji la uso huku wengine wakipatwa na mshtuko.
Na Daniel Makaka, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com