Akaunti ya twitter ya Rais Kenyatta.
Akaunti za mitandao ya kijamii za Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, katika mitandao ya Facebook, na Twitter, zimefutwa kwenye mitandao leo asubuhi Machi 22, 2019.
Akaunti hizo zimefutwa ikiwa ni muda mfupi, baada ya kutoa ujumbe ambao ulikuwa unasema kwamba hakuna atakayepona kwenye vita dhidi ya ufisadi.
“Kama wewe ni fisadi tutapigana na wewe. Unaweza ukawa dada yangu, kaka au mtu wa karibu na mimi kwenye siasa. Siwezi kushikamana au kukubaliana na hilo katika jitihada zangu, nitaendelea kuimarisha umoja wa Kenya” Yalisomeka maneno yaliyoandikwa Twitter.
Mkuu wa wafanyakazi wa ofisi ya Rais, Nzioka Waita amesema kwamba akaunti hizo zimezuiliwa kwa muda.
“Hii ni kutokana na kuingiliwa kiharamu kwa akaunti rasmi za mitandao ya kijamii za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta. Akaunti zote rasmi za mitandao ya kijamii zimesimamishwa kwa muda kwa ajili ya kuruhusu kufanyika marekebisho yanayotakiwa,” amesema Waita.
Akaunti za Twitter na Facebook za Bwana Kenyatta zina mamilioni ya wafuasi.
Gazeti la kibinafsi la The Star nchini humo limeripoti kuwa ujumbe uliotumwa kwenye Twitter unaoangaliwa kama kuwa wenye utata wa kisiasa, uliotumwa leo asubuhi, ulikuwa ndio sababu ya kufungwa kwa akaunti hizo.
Gazeti la The Star lilishirikisha umma picha ya ujumbe huo wa Twitter:
Gazeti hilo limeripoti kuwa maneno yaliyoandikwa kwenye ujumbe huo tata yaliyosema "mshirika wangu wa karibu wa kisiasa" katika twittee hiyo huenda ulimaanisha Naibu rais wa Kenyatta, William Ruto.
Wafuasi wa Bwana Ruto wamekuwa wakikosoa vikali vita vya rais Kenyatta vya hivi karibuni dhidi ya ufisadi ambavyo vimesababisha kukamatwa na kuhojiwa kwa maafisa wa serikali, wakisema kuwa vimekuwa na njama dhidi ya naibu wake.
Wanasema kuwa watu walio karibu na Bwana William Ruto wamekuwa wakilengwa.Uhusiano wa karibu wa hivi karibuni wa rais Kenyatta na Bwana Odinga aliyekuwa mpinzani wake unaonekana kama njama za kuweka kando kisiasa naibu rais William Ruto
Uhusiano baina ya viongozi hao wawili , ambao waligombea nafasi zao chini ya Muuungao wa Jubelee, katika uchaguzi wa mwaka 2013 na 2017, unasemekana kuingia dosari hivi karibuni, husasn baada ya Bwana Kenyatta kusaini makubaliano na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Bwana Odinga na Bwana Kenyatta - walikuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2017 - walikubaliana kufanya kazi pamoja mwaka 2018 kwa ajili ya "kuteta amani nchini ".
Uhusiano wa karibu wa Bwana Kenyatta na Bwana Odinga na pia kuongezeka wa umaarufu wa Bwana Odinga tangu walipofanya makubaliano kunaangaliwa na baadhi ya watu kama njama za kisiasa za kumaliza mpango wa Bwana Ruto wa kumrithi Bwana Kenyatta kama rais.