Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA ONYO KWA VIONGOZI WA SERIKALI KUWATUMIA WAANDISHI WA HABARI BINAFSI

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa wizara, taasisi au mikoa kuacha mara moja tabia ya kuwatumia waandishi wa habari binafsi katika utekelezaji wa majukumu yao ya Kiserikali na kuwaacha wale ambao wameajiriwa na Serikali katika ofisi zao kwa kazi hiyo.

“Kwanza tabia hii ni hatari kwa usalama wa taarifa za Serikali. Nitumie nafasi hii kukemea viongozi na watendaji wenye tabia za namna hii kuacha mara moja tabia hizo zisizo kinyume na matakwa ya maadili ya utumishi wa umma.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Machi 18, 2019)katika ufunguzi wa Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini, kinachofanyika katika ukumbi wa BOT jijini Mwanza. Kikao hicho kinahudhuriwa na Maafisa Habari na Mawasiliano takbaribani 400.

Katika kuhakikisha suala hilo linakomeshwa Serikalini, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo umpelekee majina ya kiongozi au mtendaji wa ngazi yeyote ile ambaye bila sababu zozote anawapuuza waliajiriwa na Serikali kufanya kazi hiyo.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatumia rasilimali nyingi kuajiri, kuanzisha, kuiendeleza na kuitunza kada ya maafisa habari Serikalini, hivyo, maafisa habari waliopo wapewe nafasi ya kutekeleza majukumu yao kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Waziri Mkuu amesema maafisa hao wanatakiwa wapewe ushirikiano na viongozi wa taasisi wanazozitumikia ili habari za utekelezaji wa Serikali ziwafikie wananchi badala ya viongozi na wataalamu wengine kukalia habari hizo. “Mawaziri na Wakuu wa Mikoa, simamieni Maafisa Habari kutimiza wajibu wao”.

Waziri Mkuu amesema anafahamu changamoto nyingine kwa maafisa habari ambazo husababishwa na viongozi au watendaji katika taasisi za umma na hasa katika ngazi za Wizara, Mikoa na Halmashauri za kutotambua mchango wa sekta ya habari katika maendeleo ya nchi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema anazo taarifa za baadhi ya maafisa habari ambao wana vifaa vyote pamoja na ofisi nzuri zenye kuvutia lakini bado hawatimizi wajibu wao ipasavyo katika kutangaza shughuli za Serikali. 

“Wengine hawajui shughuli zinazofanywa na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wakuu wa Sekta kwa siku, wiki hata mwezi…Taasisi haina taarifa. Badilikeni, nenda mkakusanye taarifa na mzitoe hadharani”.“Tambueni kwamba Serikali haitowavumilia Maafisa Habari wa namna hii kwani ni wazi kabisa kuwa hawatufai na ni mzigo kwa Serikali. Basi, wale wote wenye mienendo ya namna hiyo chukueni hatua, mjitathmini na mjirekebishe mara moja. 

Amesema maafisa hao ambao wamepata mafunzo ni lazima utendaji wao ukazingatia maadili na weledi na wakati wote utekelezaji wa majukumu yao ujikite katika kuboresha masilahi ya umma, kuepuka uchochezi, ushabiki, vijembe na kuepuka kuandika habari zinazopandikiza chuki katika jamii. 

Pia, ameielekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari-MAELEZO ifanye tathmini ya kina kuhusu utendaji wa maafisa habari hasa wale wanaoongoza vitengo na watakaoonekana kuwa hawaisaidii Serikali waondolewe mmoja baada ya mwingine bila kupepesa macho.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kila nchi inayo misingi, utamaduni na tunu zake, hivyo amewataka maafisa hao watambue kuwa wao ni sehemu muhimu katika kusimamia na kuendeleza misingi,utamaduni na tunu za Taifa. 

Amesema maafisa hao hawana budi kuhakikisha wanabeba agenda za Kitaifa katika utekelezaji wa majukumu yao kwani yapo mambo ambayo ni msukumo wa kitaifa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. 

“Kutokana na haya kila tunachoandika ni lazima kiwiane na agenda zetu kitaifa katika sekta mbalimbali. Kwa mfano: Kisiasa msukumo wetu ni amani na utulivu, kiuchumi msukumo wetu sasa ni ujenzi wa viwanda na kulifikisha Taifa katika uchumi wa kati. Kiutamaduni msukumo wetu ni kulinda na kudumisha mila na tamaduni zetu”. 

Waziri Mkuu amesema mambo hayo wao wana wajibu wa kuyapa kipaumbele ili jamii iweze kuhabarishwa vizuri. Vyombo vingine vya nje haviwezi kuyaandika na kuyatangaza mambo hayo vizuri na kwa msukumo wa Kitaifa kama wao. Nawasihi chukueni nafasi yenu katika kuzibeba agenda zetu za Kitaifa.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com