Timu ya Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga jioni ya leo.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 51 baada ya kucheza mechi 20 sasa ikiendelea kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 53 za mechi 26 na Yanga SC pointi 64 za mechi 26.
Shujaa wa Simba SC leo ni Nahodha wa timu hiyo, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mabao yote hayo kipindi cha pili.
Bocco, mchezaji wa zamani na wa muda mrefu wa Azam FC, alifunga bao lake la kwanza dakika ya 51 kwa penalti iliyitolewa na refa Emmanuel Mwandembwa kutoka Mwanza baada ya Majaliwa Shaaban wa Stand United kushika mpira wakati akivishwa kanzu na mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere mwenye asili ya Uganda.
Bocco, mchezaji mrefu na mwenye nguvu akafunga bao la pili dakika ya 65 akiusindikiza kwa kichwa mpira ulioelekezwa langoni na beki Mghana, Nicholas Gyan aliyeunganisha mpira uliorudi baada ya kuokolewa kwa kona iliyopigwa na kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
Simba SC iliendelea kulitia misukosuko lango Stand United ambayo leo safu yake ya ulinzi ilikuwa inafanya makosa mengi, lakini tu haikuwa na bahati uya kuongeza mabao.
Kikosi cha Stand United kilikuwa; Mohamed Makaka, Makenzi Kapinga, Majaliwa Shaaban, Jisendi Maganda, Ahmed Tajdeen, Majid Kimbindile, Datus Peter/William Kimanzi dk69, Hafidh Mussa, Six Mwasekaga, Maurice Mahela/Mwinyi Elias dk70 na Jacob Massawe.
Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Serge Wawa, James Kotei, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga/Muzamil Yassin dk82, John Bocco, Adam Salamba/Meddie Kagere dk46 na Rashid Juma/Jonas Mkude dk58.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mtibwa Sugar imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, mabao ya Jaffar Salum Kibaya dakika ya 37 na Salum Kihimbwa dakika 49.
Singida United imetoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Namfua mjini Singida. Adam Adam alianza kuifungia Tanzania Prisons dakika ya tano, kabla ya Geofrey Mwashiuya kuisawazishia Singida dakika ya 52 na Jumanne Elifadhili kujifunga dakika ya 87 kuwapa wenyeji bao la ushindi.
Na mabao ya Venance Ludovic dakika ya 21 na Kasim Khamis dakika ya 54 yakaipa ushindi wa 2-0 Kagera Sugar dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, wakati Mbeya City imelazimishwa sare ya 0-0 na Ndanda FC Uwanja wa Sokoine.
Chanzo - binzubeiry
Social Plugin