Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LIPO SOMO TUNALIPATA SIMBA SC KUTINGA ROBO-FAINALI ACL


Hapana shaka mashabiki wa Simba hawataweza kuusahau usiku wa tarehe 16 Machi 2019. Hawatasahu namna kiungo fundi Mnyarwanda Haruna Niyonzima alivyoupisha mpira uliopigwa na Nahodha wao John Bocco. Ni watu wachache wenye akili ya mpira tena ile ya kuzaliwa nayo ndiyo wangeweza kufanya alichokifanya Niyonzima.
Utasema nini zaidi ya kumpa kongole Niyonzima ambaye wakati anaingia "Watu wa Mpira" walijisemea moyini kwamba "Huyu anakwenda kubadili matokeo!" Ndicho alichokifanya. Dunia nzima imeona na unatamani uurudishe nyuma umri wake ili uendelee kumuona akifanya vitu kama hivyo. Walakini, haiwezekani.

USHINDI WA SIMBA UNA MAANA GANI?

Pamoja na Simba kupanda katika nafasi za Ubora wa Soka kwa Vilabu na nafasi ya uwakilishi ambayo Nchi itanufaika kwa Vilabu vyetu, ushindi huu una maanisha:

1. Tunahitaji kufanya UWEKEZAJI mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya SOKA letu, siyo ubabaishaji. Mpira wa sasa unahitaji uwekezaji, tunawahitaji akina Mo zaidi ya 5. Uwekezaji wa watu wa aina ya Mo kwa Vilabu vyetu 5 utatupa nafasi ya kuwa na uhakika wa kufanya vizuri katika michuano ya Kimataifa. 

2. Somo kwa Vilabu vingine. Viongozi wa Vilabu vingine vya Tanzania hasa Yanga, Azam na vingine waone faida ya kuwekeza na kuacha kabisa migogoro. Tangu Simba waingie katika mfumo wa Kampuni, siyo tu wamepunguza migogoro, bali imeondoa kabisa.
3. Wachezaji wazawa wajipange. Ni ukweli usiopingika msimu ujao tutaanza kuona WIMBI la wachezaji wa kigeni kutoka Nchi za Magharibi ambao siku zote wapo vitani kusaka mafanikio popote wanaposikia kuna soka la kulipwa. Kama utakumbuka, mechi ya juzi, Simba SC ilikuwa na wachezaji watano wazawa kwenye kikosi cha kwanza; Aishi Manula, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin na John Raphael Bocco. Hii maana yake nini? Inamaanisha kwamba hakuna nafasi kwa watu wanaoleta blah blah. 

Wachzaji wazawa waitumie nafasi hii kujitangaza kwa sababu vipo Vilabu Nje ya Tanzania vitataka kujua zaidi kuhusu Soka letu, Vilabu vyetu na wachezaji wetu.
SHIRIKISHO LA SOKA

Huu ndiyo wakati pekee wa TFF kuutumia kuboresha Ligi yetu na kuacha blah blah. Niwakumbushe tu TFF kwamba Bingwa wetu anaenda kukutana na Mabingwa wenzake not otherwise.

Shirikisho lisimamie kwa weledi Soka letu, Waamuzi wetu na litoe 'sapoti' ya uhakika kwa Vilabu vyetu vinapofikia hatua ya kuonesha kiu au haja ya kujiendesha kwa mfumo wa kisasa kama ilivyo kwa Simba. Kwa hivi, siyo tu tutalikuza soka letu, bali tutavutia Makampuni na Wadhamini mbalimbali kutaka kuwekeza katika Ligi yetu kwa sababu wataona vinafanya vizuri katika uga wa Kimataifa. 

WABABAISHAJI

Huu ndiyo wakati wa Vilabu vyote nchini kuwakataa wababishaji aina ya Mzee Akilimali na wengine mfano wake. Watu wa namna hii hurudisha nyuma maendeleo ya Vilabu vyetu. Watu wa sampuli hii hautokaa uwasikie pale Barcelona, Chelsea, Arsenal ama Man U. Vilabu vyenye watu wa aina hii vianze sasa mchakato wa 'kuwapiga pini' hawatakiwi kwenye soka.

BIG UP KWA MOHAMED 'MO' DEWJI

Pamoja na mapenzi yake kwa Simba kiasi cha kuamua kuwekeza "Noti" zake pale Msimbazi, ni kitendo cha kupongezwa na kuungwa mkono na hatimaye KUIGWA kwa vitendo na "Matajiri" wengine.
Mo angeweza kufanyia mambo mengine fedha yake, lakini kwa mapenzi yake kwa Simba na Soka lakaamuaa Tanzania ameamua kufanya hivyo na hatimaye kwa hatua ya timu kukata tiketi ya kucheza Robo-fainali itamfariji na kumfanya atembee kifua mbele. 

Big up Mo, big up wana Simba kwa hatua hii mliyofikia na iwe funzo kwa Vilabu vingine.

Midfield Maestro,
Emmanuel 'Petit' Msigwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com