WAZUNGU WA SINGIDA UNITED WATISHIA KUFUNGASHA VIRAGO



Wakati Singida United inatapatapa kujinasua kushuka daraja, makocha wake wawili wa kigeni wametishia kufungasha virago na kurejea makwao kwa madai ya kutolipwa maslahi yao na Uongozi wa timu hiyo.

Madai hayo yamebainishwa na makocha Dusan Momcilovic na Dragan Popadic jana mjini Singida.

Makocha hao wamedai kuwa tangu waingie hapa nchini Januari 10 Mwaka huu na kujiunga na timu hiyo wamekuwa wakiambulia ahadi hewa tu kutoka kwa Mkurugenzi wa timu hiyo, Festo Sanga na kwamba sasa wameamua kubwaga manyanga.

Walidai kuwa ingawa walipopokelewa na uongozi wa Singida United, waliahidiwa kupewa nyumba, chakula, mpishi na usafiri binafsi lakini hadi leo walichoambulia ni nyumba tu huku siku nyingine wakilazimika kushindia ndizi mbivu, msaada wa chakula kidogo kutoka kwa majirani wema au wakati mwingine kulala njaa.

Mserbia Dusan ambaye ni Kocha wa viungo alisema yeye aliahidiwa kupatiwa Mkataba lakini hadi sasa hana Mkataba, hajalipwa mshahara wowote wala bonasi yake aliyoahidiwa kupewa wakati Singida United ilipocheza na JKT kwenye Kombe la Shirikisho.

"Ni kweli tumepewa nyumba nzuri lakini haina chakula na kuna wakati tunalala giza kwa kukosa umeme kwa vile hatuna hela za kununua LUKU. Binafsi nimeamua kuacha kujishughulisha na timu hadi nitakapolipwa stahiki zangu" alisema Dusan.

Naye Kocha Mkuu, Popadic alidai kuwa ingawa ana Mkataba lakini Uongozi hauheshimu Mkataba huo kwani halipwi mshahara wake kwa wakati wala hapati marupurupu mengine kulingana na mapatano yao.

"Kinachoniuma zaidi ni Uongozi wa juu kutoshirikiana nami. Mkurugenzi Sanga anaishi Dar na Rais wa timu, Mwigulu Nchemba sijui alipo. Waliopo hapa tunashindwa kuwasiliana kutokana na kikwazo cha lugha... Kwa kifupi tumeachwa solemba hatujui nani wa kumweleza shida zetu" alilama na kuongeza,

Idadi ya wachezaji inazidi kupungua, wengi wao wanakimbia njaa na kwenda kutafuta malisho bora mahali pengine. Hivyo, si kweli klabu inauza wachezaji wake kama ambavyo anadai Mkurugenzi Sanga bali wachezaji wanakimbia njaa".

Aidha, alilaumu tabia ya Uongozi huo kusajili wachezaji wengi wa kigeni ambao hata hivyo alidai kuwa uwezo wao ni wa kiwango cha chini ikilinganishwa na baadhi ya wachezaji wa humu nchini. “Hivi unawezaje kusajili wachezaji saba wa kigeni kwenye timu?” alihoji.

Kutokana na hali hiyo kwenye klabu, makocha hao wametishia kufungasha virago na kurudi makwao ifikapo Machi 15 mwaka huu huku Kocha Dusan akisisitiza kupatiwa haki zake zote kabla ya kuondoka nchini.

Wakati makocha wanadai kukosa mishahara, wachezaji nao wanadai kutokulipwa mishahara yao kati ya miezi miwili hadi minane na kula wali maharage kila siku huku Uongozi ukiwapiga danadana kila wanapokumbushia haki zao hali ambayo Kocha Popadic anadhani imechangia kwa kiasi kikubwa matokeo mabaya ya timu hiyo kwenye Ligi Kuu inayoendelea.

Mkurugenzi wa Singida, Festo Sanga alipoulizwa kuhusiana na madai hayo alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wachezaji hawajalipwa mishahara yao na kusema kuwa hali kama hiyo ipo kwa timu nyingi hapa nchini. Kuhusu kushindwa kumpa Dusan Mkataba, Sanga amedai hawakufanya hivyo baada ya Kocha huyo kuwaarifu amepata timu nyingine nje ya nchi.

Kwa sasa, Singida United inashika nafasi ya tatu kutoka mwisho kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imejikusanyia alama 32 tu kutokana na mechi zake 27. 

Na Abby Nkungu, Singida


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post