Mwenyekiti wa Stand United, Dkt. Ellyson Maeja
Klabu ya Stand United 'Chama la Wana' imetamba kutembeza kipigo kwa Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Simba SC katika mchezo utakaopigwa Jumapili Machi 3,2019 katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ijumaa, Machi 1,2019, Mwenyekiti wa Stand United, Dkt. Ellyson Maeja amesema wamejiandaa vizuri kupeleka kilio kwa Wekundu wa Msimbazi 'Simba SC'.
Amesema wamepata wiki nzima ya mapumziko,uongozi na benchi la ufundi chini ya Mwalimu Athuman Bilal 'Bilo wa Bironga', wamekaa na kuangalia namna ya kupata pointi tatu kutoka kwa Simba SC.
"Mwalimu amerekebisha mapungufu yote yaliyokuwepo na bado tumepata nafasi ya kutizama mikanda ya mechi za Simba jinsi alivyocheza na wenzetu Lipuli FC,Azam FC tukaona mapungufu yaliyokuwepo na wenzetu wakapoteza, tumekubaliana ni namna gani tutaziba hayo mapungufu na sisi kuweza kufanya vizuri kupata hizo pointi",amesema Dkt. Maeja.
"Kwa mechi hii wananchi wa Shinyanga na wadau wasiwe na wasiwasi, Boko atakuwa bokoboko,Kagere kwetu ni kasamaki,hivyo kataliwa,halafu huyu Okwi mechi zote huwa hamalizi,huwa anaishia dakika 20,15 anavua viatu anaomba atoke,sasa huyu tutamwite Ong'wise (wa kwetu),kijana wa kwetu....
Wazee wa Shinyanga wamesema msiwe na wasiwasi kwamba Simba lazima Bhakindwe "Simba lazima washindwe" na vijana waseme Yes! Yes! kwa hiyo karibuni muangalie mechi nzuri",amesema Dkt. Maeja.
Mashabiki na wapenzi wa Stand United wamesema wanafurahia kuona Mnyama Simba akifungwa naye asikie machungu ya kufungwa,wakiipa moyo Stand United kwamba ipo nyumbani hivyo ni lazima Simba alale.
"Viporo vya Simba vinaweza kuchacha au kuvila vizuri lakini kinachotakiwa ni mpira kuchezwa kwa ufundi,kila timu itumie dakika 90 vizuri, waamuzi wawe fair wazingatie sheria 17 na atakayetumia hizo dakika 90 basi ni halali yake",ameongeza.
Aidha ameishukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Vinywaji Jambo Food Products LTD Salum Hamis (Salum Mbuzi) maarufu Jambo ambaye ni mdhamini Mkuu wa Stand United kupitia kinywaji chake cha Jambo Cola kwa kuendelea kuwa pamoja na Stand United kuhakikisha wachezaji wanakula vizuri kambini na kusafiri vizuri lakini pia wadau,wapenzi na wanachama kwa kuendelea kuiunga mkono timu.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin