Mwanasiasa Mkongwe na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja baada ya ukimya wa muda mrefu amesema kesho Jumatano ya Machi 6, 2019 atazungumzia mustakabali wa nchi na mwenendo wa demokrasia nchini Tanzania.
Hamis Mgeja ni mmoja wa marafiki wakubwa wa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ambapo wakati alipoamua kwenda upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Mgeja naye aliamua kumfuata na aliacha nafasi zake zote ndani ya CCM na kisha kuungana na Lowassa upinzani.
Taarifa yake iliyotolewa katika vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Mgeja amesema kuwa amekuwa nje ya ulingo wa siasa kwa muda mrefu na katika kipindi chote alijikita kwenye shughuli za kilimo lakini kesho (Jumatano) amejipanga kuzungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari kuhusu mustakabali wa nchi katika nyanja mbalimbali pamoja na demokrasia.
"Mimi Khamisi Mgeja kesho Jumatano ya Machi 6 , 2019 , kuanzia saa 4:30 asubuhi nitaongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa Hoteli ya Lamada iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam. Nataka kuzungumza hali ya nchi yetu katika nyanja mbalimbali ikiwemo eneo la demokrasia nchini kwetu,"amesema Mgeja na kutoa mwito kwa waandishi wa habari kujitokeza kwa wingi ili kupata nafasi ya kumsikiliza na kisha kumuuliza maswali.
Hata hivyo haifahamiki iwapo Mgeja naye atatangaza kurudi CCM au laa hasa kwa kuzingatia kuwa Lowassa ambaye ni rafiki yake mkubwa tayari amerejea nyumbani (CCM), mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza kwa njia ya simu leo , Mgeja amesema hiyo kesho ndiyo itakuwa siku ya pekee kwake kutoa ya moyoni , hivyo Waanzania watapata nafasi ya kumsikia kile ambacho amepanga kukizungumza.
Alipoulizwa iwapo naye atarejea CCM, Mgeja amejibu "Hiyo kesho nitakuwa na nafasi ya kutosha kuhusu mambo mbalimbali, hivyo hilo swali lako nitalijibu kesho ambayo nimepanga kuzungumzia mustakabali wa nchi yetu."
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
Chanzo- Michuzi blog
Social Plugin