Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesikitishwa na baadhi ya Maafisa na Askari wake kujihusisha na vitendo vya rushwa na unyanyasaji kwa wachimbaji wadogo wa madini huko Wilayani Chunya Mkoani Mbeya. Vitendo hivyo ni kinyume cha Sheria, kanuni, Taratibu, Miiko na Maadili ya Utumishi wa Umma.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limechukua jambo hili kwa uzito na tayari limeshatuma Maafisa waandamizi kwa uchunguzi wa kina ikiwa ni pamoja na kuwafungulia watuhumiwa wote mashtaka ya kijeshi. Mara baada ya uchunguzi kukamilika Umma utajulishwa juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika na tuhuma hizo ambazo zimechafua taswira ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa wito kwa Umma kutoa taarifa mapema kwa Makamanda wa Zimamoto wa Mikoa pindi wanapokutana na matendo yoyote wanayoyatilia shaka hususani kwenye shughuli za ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya moto unaofanywa na Maafisa na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwenye maeneo ya umma, binafsi, biashara na mengineyo. Ukaguzi huu huambatana na ukusanyaji wa tozo ya usalama wa moto na baadaye kutolewa kwa vyeti vya Usalama wa moto kwa waliokidhi vigezo.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa shukrani kwa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano waliotoa katika hatua za awali zilizoanza kuchukuliwa dhidi ya tuhuma hizo na kwa vyombo vyote vya habari kwa namna ambavyo vimeendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuhabarisha umma juu ya utendaji kazi wake kila siku.