Mwanamme mmoja wa kijiji cha Mureku eneo bunge la Navakholo kaunti ya Kakamega nchini Kenya anaishi kwa upweke baada ya mkewe kumwacha kwa tetesi kuwa hana sehemu zake za siri.
Alfred Sifuna mwanaume mwenye umri wa miaka 30 anaishi kwa upweke na uchungu baada yake kuvamiwa na kikundi cha watu alipokuwa barabarani na kumuibia pesa kabla kuzinyofoa sehemu zake za siri na kutoroka nazo huku sababu ya kutendewa unyama huo ukiwa haujulikani.
"Nilivamiwa nikitoka sokoni na watu ninaowajua, wengine wao ni majirani wangu, walinibeba na kunibana kwa nguvu kisha wakaniibia pesa nilizokuwa nazo kabla yao kunivua nguo na kukata sehemu yangu ya siri ambayo walitoroka nayo sijui kile walichoenda kulifanyia." Alisema sifuna.
Sifuna anasema mbali na kuachwa kwa uchungu ameshindwa kutimiza majukumu yake kama mwanaume katika familia yake suala ambalo anadai limesababisha mke wake kumwacha huku watoto wake wakitaabika.
Sifuna anaeleza kuwa mkewe alimtoroka kwa sababu hana uwezo wa kumtosheleza kimapenzi.
"Familia yangu imenitoroka watoto wangu wanahangaikia mitaani wakirogota makombe na kuwaomba watu vyakula, nahofia wanaweza kuuawa ama kujiingiza katika makundi mabaya.
Niliachwa na mke ambaye amehamia pengine baada ya kugundua sina sehemu zangu za siri zimenyofolewa kwa hivyo siwezi kumtosheleza ipasavyo, nashinda nikitembea na leso kama mtu ambaye ametahiri na sasa naomba serikali pamoja na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kuingilia kati na kunisaidia kupata haki.",aliongezea.
Sifuna anadai kuwa licha ya kuripoti kesi hiyo katika kituo cha polisi cha Navakholo, hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya wahuni hao kwani walikamatwa na kuachiliwa kwa dhamana jambo ambalo limepelekea yeye kutishiwa maisha na watu hao.
"Nilienda katika hospitali ya Navakholo kutibiwa kabla kuripoti kesi hii kwa OCS katika kituo cha polisi cha Navakholo. La kushangaza ni kuwa hakuna hatua zozote za kisheria zimechukuliwa dhidi yao. Walikamatwa na kupelekwa kortini mjini Kakamega na kuachiliwa kwa dhamana ya KSh 20,000 kila mmoja. Kwa sasa wanatembea wakiwa huru na kunitishia maisha kuwa wataniua." Sifuna alisimulia kwa masikitiko.
Ameviomba vitengo husika pamoja na mashirika ya kutetea haki za kibinadmu kuingilia kati ili kumwezesha kupata haki.
Na Dennis Avokoywa -Kakamega
Social Plugin