Tetemeko la ardhi lililodumu kwa takriban dakika moja leo mchana Alhamisi Machi 21, 2019 limetokea mkoani Mbeya na kuzua taharuki huku baadhi ya wananchi na wafanyakazi katika ofisi mbalimbali wakitimua mbio.
Baadhi walilazimika kuacha ofisi zao huku waliopo nyumbani nao wakitoka nje ya nyumba zao.
Mwandishi wetu alishuhudia mkurugenzi wa Jiji la Mbeya James Kasusura na meya wa jiji hilo David Mwashilindi na wafanyakazi wengine wa ofisi zilizopo Uhindini jijini hapa wakitimua mbio.
“Kumbe na wewe unajua kukimbia,” alisikika akitamka Kasusura akimtania Mwashilindi na kuongeza:
"Tulikuwa na maongezi na meya wangu lakini nikashangaa viti vinasogea ikanibidi nichukue hatua kukimbia ila cha kushangaza wakati natoka sijamuona meya katoka kupitia njia gani".
Watumishi wa kampuni na mashirika ya umma yenye ofisi zake jijini hapa walionekana kukaa vikundi na kuzungumza kuhusu tetemeko hilo.
Na Ipyana Samson, Mwananchi
Social Plugin