Jamii imetakiwa kuachana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwani vinachangia umaskini katika familia,ikiwa ni pamoja na kurudisha nyuma ukuaji wa uchumi wa mtu binafsi,wilaya na taifa kwa ujumla.
Hayo yalielezwa jana na diwani wa viti maalumu kata ya Sekebugolo Suzana Makoye ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uzinduzi wa kampeni ya kumlinda mtoto wa kike,iliyofanyika kijiji cha Seseko kata ya Songwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga iliyoandaliwa na vituo vya taarifa na maarifa vinavyosimamiwa na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP).
Makoye alisema bado kuna changamoto ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii ikiwemo kunyanyasa wajane,wanawake kutopewa haki ya kumiliki mali na matukio ya ubakaji ambapo aliwataka wanaharakati kuendelea kutoa elimu ili kuleta mabadiliko makubwa zaidi.
“Suala la ukatili ni kubwa linahitaji tuunganishe nguvu pamoja wanaharakati,serikali na jamii itoe ushirikiano kuwafichua wanaoendeleza vitendo vya ukatili,TGNP wamefanya kazi kubwa kuelimisha wananchi juu ya ukatili wa kijinsia wanastahili pongezi ni mfano wa kuigwa wameleta mabadiliko”,alisema Makoye.
Alisema changamoto nyingine ni ukatili wa kiuchumi ambao unafanyika ngazi ya familia na huo unatokana na kuwepo mfumo dume,kwani baadhi ya wanaume wamekuwa wakitumia wake zao kama kitega uchumi cha kuzalisha mali na mwisho wa siku wanaenda kuziuza na kuowa mke mwingine huku familia ikitaabika.
Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la The Voice of Marginalized Community(TVMC) Musa Ngangala,aliwataka wanawake kuacha uoga,kujiamini na kuwa na ujasiri kwani wanahaki sawa kama wanaume,licha ya kukabiliwa na vikwazo mbalimbali ambavyo alisema ni vya muda na wanatakiwa kukabiliana navyo ili kufikia daraja la mafanikio.
Alisema wanawake wamekuwa wakishiriki kwa asilimia kubwa kwenye shughuli za kilimo lakini matokeo yake wakati wa mavuno wanaume ndiyo wamekuwa na sauti na kufikia hatua ya kutaka kudhulumu haki ya familia yake,jambo ambalo alisema halifai ni ukatili mkubwa na kuitaka jamii kubadilika na kuwathamini wanawake kwani wana mchango mkubwa.
Naye diwani wa kata ya Songwa Abdul Ngolomole alisema vituo vya taarifa na maarifa vimesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko kutokana na kuifikia moja kwa moja jamii na kueleza madhara ya ukatili wa kijinsia yanavyochangia kuzorotesha familia na kuirudisha nyuma.
Taarifa hii imeandaliwa na mwandishi wa Malunde 1Blog Shinyanga.
Diwani wa viti maalum Suzana Makoye ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe ya uzinduzi wa kampeni ya kumlinda mtoto wa kike,iliyofanyika kijiji cha Seseko kata ya Songwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga ambayo iliandaliwa na vituo vya taarifa na maarifa vinavyosimamiwa na mtandao wa jinsia Tanzania TGNP. Aliwaasa kuachana na vitendo hivyo kwani vinarudisha nyuma maendeleo huku akiwasisitiza kuwalinda watoto wao wa kike na kuachana na tamaa ya kuwaoza katika umri mdogo ili wapate mali.
Mwenyekiti wa kijiji cha Seseko kata ya Songwa Kalonga Mwandu akizungumza na wananchi kwenye sherehe za uzinduzi wa kampeni ya kumlinda mtoto wa kike.
Katibu wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Maganzo Jayunga James akitoa taarifa ya vituo vilivyoshiriki ambapo alisema ni kituo cha Mondo,Maganzo,Mwaduiluhumbo na Songwa. pamoja na baadhi ya wajumbe kutoka vituo vya Kishapu na Bunambiyu.
Alisema changamoto kubwa walizozibaini kupitia vituo vyao ni kuwepo kwa rushwa ya ngono,vipigo kwa wanawake,natatizo la mimba kwa wanafunzi,ambapo wameiomba serikali na wadau wengine kutatua changamoto hizo.
Mwanaharakati Imelida Moris kutoka kituo cha taarifa na maarifa kata ya Maganzo akichangia mada kwenye ufunguzi wa kampeni ya kumlinda mtoto wa kike.
Sherehe inaendelea
Akina mama wakiendelea kufuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na viongozi wao.
Mgeni rasmi akizungumza na wananchi wa kijiji cha Seseko
Diwani wa kata ya Songwa Abdul Ngolomole akizungumza na wananchi wa kijiji cha Seseko kata ya Songwa,ambapo alisisitiza wanawake kushirikishwa katika maamuzi ngazi ya familia na jamii.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Songwa wakifuatilia nasaha zilizokuwa zikitolewa kwa ajili ya kumlinda mtoto wa kike.
Mkurugenzi wa Shirika la TVMC Musa Ngangala akizungumza na wananchi kwenye sherehe za uzinduzi wa kampeni ya kumlinda mtoto wa kike,alitumia fursa hiyo kuwataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao.
Social Plugin