Mtu mmoja huko Uingereza ambaye alikuwa ni muathirika wa UKIMWI, amekuwa mtu wa pili ulimwenguni kupona ugonjwa huo, baada ya kupandikizwa chembe chembe hai zinazokaa ndani ya mifupa ama seli - (Bone Marrow).
Ikiwa ni takriban miaka mitatu imepita tangu awekewe cells za bone marrow za kipekee zenye uwezo wa kuzuia maambukizi ya HIV na kutumia dawa maalum, mtu huyo ameonesha kutokuwa na dalili zozote za kwamba aliwahi kuwa na HIV.
Madaktari wanasema mtu huyo aliyepewa jina la Mgonjwa London alipandikizwa chembe chembe hizo takriban miaka mitatu iliyopita na hajaonesha dalili za virusi hivyo kwa zaidi ya miezi 18, licha ya kuacha kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.
“Hakuna virusi ambavyo tunaweza viona, hatuwezi kuvipata”, amesema Dkt. Ravindra Gupta, ambaye pia ni Profesa na mtaalamu wa masuala ya HIV aliyeongoza timu ya wanasayansi kutoa tiba hiyo ya utafiti.
Kutokana na hilo, Dkt Gupta amesema kwamba kesi hii ni uthibitiso tosha wa dhana kwamba ipo siku wanasayansi wataweza kupata tiba rasmi ya UKIMWI na kumaliza kabisa tatizo hili.
Mmoja wa madaktari waliohusika na matibabu yake hata hivyo ameonya kuwa ni mapema kuzungumzia tiba hiyo hivyo haimaanishi kuwa wameshaipata tiba ya UKIMWI kwa sasa.
Mtu huyo kutoka Uingereza anakuwa wa pili ulimwenguni kupata tiba hiyo, baada ya kijana wa Marekani Timothy Brown, kufanyiwa tiba hiyo hiyo na kupona kabisa, huko nchini Ujerumani mwaka 2007.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa UKIMWI tayari umeshaua takriban watu milioni 35 duniani tangu ulipoanza katika miaka ya 1980s, na hadi kufikia mwaka 2017 takriban watu milioni 37 wanaishi na virusi vya ugonjwa huo, huku madaktari wakikesha kutafuta tiba kumaliza kabisa ugonjwa huo hatari.
Chanzo - BBC
SIKILIZA HAPA