Rais wa zamani wa Peru, Alejandro Toledo, ambaye anakabiliwa na uwezekano wa kuondolewa Marekani ili arudi kwao kujibu mashtaka ya rushwa, aliwekwa mahabusu kwa muda mfupi baada ya kuonekana hadharani akiwa amelewa baada ya kunywa pombe katika mgahawa mmoja jijini California, polisi wamesema.
Toledo, 73, alikamatwa karibu na Palo Alto Jumapili, na akalala mahabusu kabla ya kuachiwa huru jana Jumatatu, msemaji wa polisi wa kaunti ya San Mateo, Rosemerry Blankswade aliiambia AFP.
Toledo anatakiwa nchini Peru akihusishwa na tuhuma za kupokea dola 20 milioni za Kimarekani kutoka kampuni ya ujenzi wa Brazil ya Odebrecht, ikiwa ni sehemu ya kashfa za ufisadi dhidi ya viongozi wa juu nchini Peru.
Lakini Blankswade alithibitisha kuwa Toledo, ambaye aliiongoza Peru kuanzia mwaka 2001 hadi 2016, hatarejeshwa kwao baada ya kukamatwa.
Na Waziri wa Mambo ya Nje wa Peru alithibitisha kuwa kukamatwa kwake hakuhusiani na mchakato unaoendelea kuhusu kurejeshwa kwao.
Social Plugin