Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo akizungumza katika kikao cha Viongozi wa Jamii kata ya Usanda.
Shirika la Agape AIDS Control Program la Mkoani Shinyanga limekutana na viongozi wa jamii katika kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kutambua na kutokomeza mila na desturi kandamizi zinazochangia ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili kupunguza mimba na ndoa za utotoni na maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Kikao hicho cha siku moja kimefanyika leo Jumanne Machi 19,2019 katika shule ya msingi Shingida iliyopo katika kata ya Usanda na kukutanisha pamoja wenyeviti wa vitongoji 30 vya kata hiyo,viongozi wa kimila,dini,watu wenye ulemavu na vijana.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape, Lucy Maganga alisema viongozi wa jamii wanayo nafasi kubwa ya kuielimisha jamii kuachana na mila na desturi kandamizi ambazo zimekuwa zikichangia mimba na ndoa za utotoni.
“Mila na desturi kandamizi zinachangia kwa kiasi kikubwa ukatili lakini pia maambukizi ya VVU na UKIMWI,ni jukumu letu sote kushirikiana kupiga vita mila na desturi hizi ili jamii yetu iwe salama”,alieleza.
“Tuwaambie wananchi waache kufanya vitendo vya ukatili,mfano ukimnyanyasa mama nyumbani ni sawa na kwamba umenyanyasa familia nzima,mama atawaambia pia watoto jinsi anavyotendewa ukatili matokeo yake chuki inatawala katika familia”,aliongeza Maganga.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo aliwataka wazazi na walezi kupeleka watoto shule badala ya kuwapa kazi ya kulinda ‘kuswaga’ mifugo na kuwaozesha wakiwa na umri chini ya miaka 18.
“Lazima tuwalinde watoto wetu, pelekeni watoto shule, Kuswaga ng’ombe siyo kazi ya mtoto,jitahidini pia kuzungumza na kucheza na watoto wenu na kuwaeleza mambo mazuri na mabaya ambayo hawapaswi kuyafanya”,alisema Mweyo.
Aidha aliwashauri akina mama kujiunga katika vikundi vya ujasirimali ili kuimarisha uchumi wa kaya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).
Nao wajumbe wa kikao hicho walizitaja baadhi ya mila na desturi zilizopitwa na wakati zinazoendelea kuwepo katika eneo hilo kuwa ni kurithi wajane,kutopeleka watoto shule, kuozesha watoto,kugawa mali kwa watoto wa kiume tu baba anapofariki na mwanawake kutorithi mali mme anapofariki dunia.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape, Lucy Maganga akizungumza katika kikao cha Viongozi wa Jamii katika kata ya Usanda Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu mila na desturi kandamizi zinachongia mimba na ndoa za utotoni sambamba na maambukizi ya VVU na UKIMWI - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape, Lucy Maganga akiwasihi wajumbe wa kikao hicho kushirikiana katika kupiga vita mila na desturi kandamizi katika jamii.
Wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape, Lucy Maganga.
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo akiwasilisha mada kuhusu Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) na kuwataka wajumbe wa kikao cha Viongozi wa jamii kuwa tayari kushirikiana na viongozi wa serikali na wadau mbalimbali kutokomeza mila na desturi kandamizi zinazochangia mimba na ndoa za utotoni.
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo akiwataka wanaume kubadilika na kuacha kuozesha watoto chini ya umri wa miaka 18 na wawapeleke shule badala ya kuwapa kazi ya kuswaga mifugo.
Wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo (kushoto).
Mratibu wa Mradi wa Afya ya Uzazi na Ujinsia - Save The Children Sweden unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Sida la nchini Sweden,John Maliyapamba Komba akiwasihi viongozi wa jamii kushirikiana na shirika la Agape na serikali ili kutokomeza mila na desturi kandamizi katika jamii.
Afisa Ustawi wa Jamii kata ya Usanda,Halima Tendeja akizungumza katika kikao hicho.
Shimba Bundala akichangia hoja wakati wa kikao hicho kuhusu mila na desturi kandamizi zinazochangia mimba na ndoa za utotoni.
Kijana Helen Mwita akieleza kuhusu mila na desturi zilizopitwa na wakati katika jamii.
Mwanasheria wa Agape,Emmanuel Nyalada akiwasilisha mada kuhusu sheria zinazomlinda mtoto.
Paul Nkarangi akichangia hoja kuhusu suala la malezi ya watoto katika jamii.
Mzee wa mila, Shija Jimisha akichangia hoja kuhusu malezi ya vijana katika jamii.
Ashura Shija akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Shija Malundi akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin