Wabunge wawili wa Chadema, Susan Kiwanga (Mlimba), Peter Lijualikali (Kilombero) na wenzao saba wanaoaminika kuwa wafuasi wa chama hicho wamerudishwa rumande hadi Machi 7, 2019 na mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro itatoa uamuzi wa dhamana yao.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Machi 4, 2019 saa tano asubuhi lakini kesi hiyo ilianza kusikilizwa majira ya saa saba mchana kufuatia hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Elizabert Nyembele kuwa na kesi nyingine ya kusikiliza.
Hakimu Nyembele ambaye ni hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo ameahirisha kesi baada ya kusikiliza hoja zilizotolewa na upande wa mashtaka na ule wa utetezi kuhusu dhamana ya washtakiwa hao.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Hekima Mwasipu ndio uliokuwa wa kwanza kuwasilisha hoja za kupinga zuio la dhamana lililotolewa na upande wa mashtaka ambapo amedai zuio hilo halikufuata taratibu za kisheria na hivyo si halali.
Wakili Mwasipu amedai upande wa mashtaka umeshindwa kuonyesha kifungu maalumu walichokitumia katika kupinga dhamana ya washtakiwa hao badala yake wanaonyesha kuomba huruma ya mahakama katika kuzuia dhamana.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali mwandamizi, Neema Haule ulidai umefuata taratibu zote za kisheria za kupinga dhamana ya washtakiwa hao na wametumia kifungu cha sheria namba 392 A cha mwenendo wa makosa ya jinai.
Wakili Haule amedai kifungu hicho chenye vifungu kidogo cha kwanza hadi cha tatu kinaeleza taratibu zinazopaswa kufuatwa wakati wa kupinga dhamana hivyo aliiomba mahakama ipokee hoja za kupinga dhamana ya washtakiwa hao kama walivyoziwasilisha.
Social Plugin