Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA MKOA AMUAGIZA RPC KUSAKA WAGANGA WA JADI


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Mathias Nyangi kuhakikisha anafanya msako wa waganga wa kienyeji katika mkoa na kuwakamata wale wote wanaofanya uganga wa kienyeji bila ya kuwa na leseni halali za kuwaruhusu kufanya shughuli hizo.

Ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza vilio vya wananchi wakati wa mkutano ulifanyika mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga, wananchi waliokuwa wakiomboleza vifo vya watoto wawili na mmoja kubaki mahututi katika hospitali ya rufaa ya mkoa baada ya mganga wa kienyeji kuwateka na kuwaficha katika gari lake chakavu tangu watoto hao kupotea tarehe 21.3.2019 na wawili kupatikana wakiwa wamefariki tarehe 23.3.2019 baada ya mmoja aliyepona kutoroka na kuwajulisha wananchi kilichotokea.

Amesema kuwa msako huo wa waganga wa kienyeji ufanyike katika wilaya zote tatu za mkoa ili kuwahakikishia wananchi amani na utulivu ambayo imekuwepo kwa miaka yote na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha wanawafagia waganga hao wanaonyesha dalili za kuvuruga utulivu uliopo katika mkoa.

“RPC fanya Operesheni kali ya waganga wa Kienyeji ndani ya Mkoa huu, wale ambao wana leseni tutajua hukohuko kwamba huyu ana leseni n ani halai au siyo halali na kama sio halali basi huyo ni halali yako, na kama kuna mganga wa kienyeji asiye na leseni, huyo ndio kabisa halali yako zaidi, kuanzia sasa hivi bonde la ziwa Rukwa kule Nkasi, Kalambo, Sumbawanga yenyewe hapa kote, opresheni ipite ya kamatakamata waganga wa kienyeji, tumechoka,” Alisisitiza.

Wakati wakitoa malalamiko yao kwa mkuu huyo wa mkoa, wananchi hao walisema kuwa vifo vya watoto hao vinahusishwa na Imani za kishirikina ambapo kumekuwa na wimbi la vijana wanaoonekana wakila, wakinywa na kuvaa vizuri bila ya kujulikana shughuli zao maalum wanazofanya jambo mbalo limekuwa likiwaumiza kichwa wananchi hao na kukosa majibu.

Mmoja wa wananchi hao Debora Maenge alisema “ Nasikitika kwa tukio hili lililotokea mtaa wa Vuta, huyu mtu tunaishi nae jirani sana, tunajua ni mtu mwema, kumbe ni mtu ambae sio mwema na hafai kabisa katika jamii, cha kushanga alikuwa na vibali ambavyo alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ni mganga wa jadi, vibali hivi vinatolewa serikalini, Je serikali yetu mtaendelea kutoa vibali hivi ili watu waendelee kuuawa kiasi hiki? serikali angalieni mnapotoa vibali je ni waganga Kweli?” Aliuliza.

Mh. Wangabo alitembelea eneo la nyumba ya mganga huyo wa kienyeji ambayo gari alilowafichia watoto ilikuwamo na kukuta nyumba hiyo ikiwa imevunjwa na gari la mganga huyo kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali.

Watuhumiwa James Kapyela (52) pamoja na mtoto wake Michael Martin (14) wa tukio hilo la mauaji ya watoto Nicolous Mwambage (7) pamoja na Emanuel Juma (4) hivi sasa wanashikiliwa na polisi huku uchunguzi wa awali ukionyesha watoto hao walifariki kwa kukosa hewa baada ya kufungiwa ndani ya gari chakavu aina ya Chaser Saloon iliyokuwa haitumiki na vioo vya gari hiyo kufungwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com