Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAVAMIZI SHAMBA LA MITI BIHARAMULO WAPEWA MIEZI 3

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ametoa muda wa miezi mitatu kwa wananchi waliovamia na kuanzisha shughuli za kibinadamu ndani ya Shamba la miti la Biharamulo kuondoka mara moja kwa hiari yao bila shuruti kabla ya mwezi Juni mwaka huu.


Ametoa muda huo ili wananchi  waliolima   mazao mbalimbali yakiwemo  mahindi na pamba  waweze kuvuna mazao yao  kabla ya kuanza kwa oparesheni maalum ya kuwaondoa, iliyopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu itakayofanywa na Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania ( TFS) kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo.

Mhe.Kanyasu  ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya   kutembelea shamba la miti Biharamulo lililopo katika wilaya ya Chato mkoani Geita.

Amesema Oparesheni hiyo haitasubiri taarifa ya Wizara tano inayoendelea kufanyiwa kazi kwa kuwa eneo hilo halihusiani na vile vijiji 366  vilivyokutwa ndani ya Hifadhi.

Amesema  haiwezekani wananchi waliovamia eneo hilo waendelee kuachwa kwa kisingizio cha Kauli ya Rais aliyoitoa Januari 15 mwaka huu kuhusiana na vijiji 366 vilivyokutwa ndani ya maeneo ya Hifadhi.

Amebainisha kuwa wananchi waliovamia eneo hilo wameitafsiri visivyo Kauli hiyo na kuongeza kuwa baada tu ya tamko la Mhe. Rais , baadhi ya wananchi hata wale waliokuwa wakiishi  katika maeneo mengine nje ya hifadhi waliendelea  kuvamia na kuanza kujimilikishia  maeneo makubwa  wakidai kuhalalishwa na tamko la Rais.

Amefafanua kuwa taarifa inayoendelea kufanyiwa kazi  na timu ya Mawaziri na Makatibu Wakuu kutoka Wizara tano imebainisha kuwa mpaka sasa zaidi ya vijiji 700 vimekutwa ndani ya Hifadhi badala 366 vilivyoripotiwa awali.

Kufuatia hali hiyo amesema baadhi ya wavamizi wa Hifadhi katika maeneo mbalimbali wataendelea kuondolewa bila kusubili kukamilika kwa zoezi linaloendelea kwa kuwa walieendelea kuvamia maeneo ya Hifadhi kwa kisingizio cha tamko la Rais huku maeneo hayo yakizidi kuharibiwa kwa miti kukatwa na shughuli nyingi za kibinadamu

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) kutenga Bajeti ya kugharamia operesheni ya kuwaondoa  wavamizi ndani ya Shamba hilo.

Ameitaka TFS kuendesha oparesheni za mara kwa mara ili wavamizi hao wajue Serikali ipo kazini kulinda rasilimali za Taifa muda wote.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chato,  Mtemi Simeoni akizungumza katika ziara hiyo  alisema kuwa  baadhi ya wananchi kutoka nje ya wilaya hiyo wamekua wakivamia na kuanzisha shughuli za kibinadamu ndani ya Shamba hilo, suala ambalo ni kinyume cha sheria.

Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa wananchi katika maenro hayo wana mahitaji makubwa ardhi na kuiomba Wizara iangalie  namna ya kuwasaidia  hekari 5000 ili wapate maeneo ya kulima na kuchungia mifugo yao.

Kwa upande wake Meneja wa Shamba hilo Bw. Thadeus Shirima  amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa hadi sasa zaidi ya hekari 900 zimepandwa miti licha ya Shamba hilo  kukabiliwa  na changamoto ya uhaba wa watumishi pamoja na vitendea kazi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com