Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini wajitathmini kwa kina zaidi kuhusu namna walivyotekeleza wajibu wao na watafakari njia bora ya kuyatangaza na kuyatetea mafanikio ya mageuzi makubwa yanayoendelea nchini.
Pia, amewataka Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini wahakikishe wanatumia vizuri taaluma zao na nyezo wanazopatiwa kusema mambo yanayofanywa kwenye sekta zote na wasipofanya hivyo watatoa fursa kwa taarifa zinazosemwa na wapinga maendeleo kuonekana kuwa ni kweli.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Machi 18, 2019)katika ufunguzi wa Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini, kinachofanyika katika ukumbi wa BOT jijini Mwanza. Kikao hicho kinahudhuriwa na Maafisa Habari na Mawasiliano takbaribani 400.
Amesema maafisa hao wanatakiwa wakumbuke kuwa wanapaswa kuueleza umma wa Watanzania kwa kina masuala yanayofanywa na Serikali hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) wenye kuweka msisitizo kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“Mkumbuke kuwa kazi ya utoaji taarifa kwa wananchi kwa sasa si utashi binafsi wa mtoa habari bali hainabudi kufanywa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi. Mathalan Sheria mpya ya Haki ya Kupata Taarifa Na. 12 ya mwaka 2016 yenye kuzitaka mamlaka za umma kuwapa wananchi taarifa zinazowahusu”.
Waziri Mkuu amesema sheria hiyo, inakwenda sambamba na sheria nyingine ya kumlinda mwananchi asilishwe taarifa za uongo, uchochezi na uzushi yaani Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016.
Amesema lengo la katiba na sheria hizo mbili, pamoja na mambo mengine, ni kuwahakikishia wananchi haki ya kupata habari tena zilizothibitishwa kwa maana ya usahihi wake na kwa wakati. “Sababu hizo, ndizo zilizofanya niguswe sana na kauli mbiu yenu isemayo: “utoaji habari sahihi na kwa wakati ni chachu katika kuifikia Tanzania ya kipato cha kati”.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kupongeza kazi nzuri zinazofanywa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (hususan Idara yake ya Habari - MAELEZO) na timu za habari za viongozi wakuu kama Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na watendaji wengine.
Pia, Waziri Mkuu amesema ameguswa na baadhi ya mada ambazo zitajadiliwa katika kikao kazi hiko, ikiwemo ya namna ya kushughulikia habari za uongo, kutunga, kughushi na namna kada yao inavyoweza kusaidia kukidhibiti kichochoro hicho haramu katika habari.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi na watendaji wote wa taasisi za umma, kuanzia sasa washirikiane na maafisa wa habari kwenye maeneo yao kuhakikisha kuwa habari muhimu kwa wananchi hazizuiwi kwa urasimu kama hazijazuiwa kisheria. Habari zitolewe kwa haraka na kwa njia anuai za kisasa.
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe afuatilie kuhusu uzinduzi wa tovuti za Halmashauri walioufanya jijini Dodoma tarehe 27 Machi 2017, kama zinafanya kazi ipasavyo.
Amesema lengo la tovuti hizo ni kuiongezea Serikali uwezo wa kuwapatia wananchi habari na taarifa kwa haraka kwa kuzingatia kwamba wako katika kipindi muhimu cha mageuzi katika historia ya nchi, ambapo mambo mengi yanafanyika Serikalini ya kiuchumi na kijamii lakini hayafikishwi kwa wananchi.
“Kuhusu hili, naiagiza Wizara ya Habari kufanya tathmini ya mara kwa mara na kuniletea taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu yenu na matakwa haya ya kisheria miongoni mwa wizara, taasisi za umma na sekretarieti za mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini”.
Waziri Mkuu amesema maafisa hao wanapaswa kufahamu kikao chao kimekuja wakati muafaka kwani Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, ipo katika mwaka wake wa nne wa kutekeleza mageuzi makubwa katika kila sekta zikiwemo za kiuchumi na kijamii nchini.
Amesema katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu kazi kubwa tena ya kihistoria imefanywa na Serikali ya awamu ya tano na wao ni mashahidi wa hayo yanayofanywa. “Ni jukumu lenu sasa kuuhabarisha umma wa Watanzania kama ambavyo Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyotaka katika Ibara ya 18(d).
Waziri Mkuu ametaja mapinduzi makubwa yaliyofanyika kwenye kila sekta nchini ikiwemo elimu; afya; nishati; mifugo; viwanda; barabara; viwanja vya ndege; uchukuzi wa anga; uchukuzi wa reli; uchukuzi wa majini; madini; sanaa za filamu na muziki; utalii na michezo mbalimbali. Amesema maafisa hao wanapaswa kuyatangaza mageuzi hayo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin