Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA FEDHA DKT. MPANGO AAGIZA KUTOTUMIA FUNGU LA LISHE KWA MATUMIZI MENGINE


Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Binti wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, ambaye ni Mwanaharakati  wa masuala ya lishe, wanawake na watoto Duniani, jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao, Dkt. Mpango, alimweleza Princess Sarah Zeid kwamba Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya masuala ya lishe, utapiamlo na udumavu wa watoto licha ya nchi kuwa na chakula cha kutosha.

Dkt. Mpango alisema kuwa iwapo eneo la lishe halitasimamiwa kikamilifu Taifa litazalisha watoto wenye udumavu wa ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na utendaji hafifu wakiwa katika shughuli mbalimbali.

Alisema ipo mikoa ambayo inazalisha mazao mengi  kama Mbeya na Njombe lakini ina kiwango kikubwa cha watoto wenye utapiamlo, na kutoa wito kwa kila mtanzania kuhakikisha anaangalia ni chakula gani kinahitajika kwa ajili ya lishe ya watoto na wakinamama wajawazito ili kupunguza udumavu na vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.

Aidha amempongeza Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, kwa kampeni yake anayoifanya duniani kote kupambana na vifo vya wakinamama wajawazito na watoto kwa kuwa mchango wa wanawake ni mkubwa katika jamii ikiwemo uzalishaji mali.

Alisema idadi ya wanawake nchini Tanzania ni asilimia 51 ya idadi ya watu wote wanaokadiriwa kufikia milioni 55 ambapo mchango wako katika sekta mbalimbali za uchumi umekuwa mkubwa hivyo jitihada za kuwalinda zinahitajika.

Alimweleza Binti Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid kwamba kwa kutambua umuhimu wa lishe serikali imelivalia njuga suala la lishe kwa kutenga bajeti kila mwaka katika kila wizara na kwamba fedha hizo zimewekewa wigo zisitumike kwa matumizi mengine.

"Nimeziagiza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote nchini kutumia fungu lililotengwa kwa ajili ya lishe  kwa matumizi yaliyopangwa  ili kuhakikisha watanzania wanaimarika kiafya na kushiriki kikamilifu katika Shughuli za Maendeleo" Alisema Dkt. Mpango.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa Mkutano kati yake na Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia, Sarah Zeid na

Kwa upande wake Mwana wa Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid, ambaye aliambatana na Mwakilishi wa Shirika  la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Tanzania, Bw. Michael Dunford, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake katika kupambana na utapiamlo unaosababishwa na ukosefu wa lishe.

Amewataka watanzania kuhakikisha suala la Lishe linapewa kipaumbele  na kila mmoja kwa manufaa ya Taifa na Dunia kwa ujumla na kwamba atahamasisha jumuiya ya kimataifa kuchangia jitihada za Serikali za kupambana na tatizo la lishe, na vifo vya wanawake wajawazito na watoto.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa-WFP nchini Tanzania Bw. Michael Dunford, amesema kuwa shirika lake linatambua mchango mkubwa wa Serikali katika kupambana na masuala ya lishe duni na shirika lake litaendelea kushirikiana na nayo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com