Kiongozi wa Chama Cha ACT - Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe amesikitishwa na majaji kutotumia mamlaka yao katika kuwapatia dhamana Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Zitto Kabwe ametoa maoni yake hayo muda mfupi baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa za DPP na kwamba hazikuwa na mashiko.
Kesi hiyo iliyokuwa ikisimamiwa na Wakili upande wa utetezi, Prof. Abdullah Safari, Jopo la majaji limesema rufaa ya DPP haina mashiko na kwamba Jaji Sam Rumanyika alikuwa sahihi kukubali kusikiliza rufani ya kupinga kutenguliwa dhamana ya washtakiwa.
Zitto amesema, "Nimeridhika na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa za DPP dhidi ya uamuzi wa Jaji Rumanyika kutupilia mbali pingamizi zao. Hata hivyo nimesikitishwa sana na Majaji kutoamua kutumia mamlaka yao kutoa dhamana ilhali kuna ‘precedent’( historia) ya Jaji Luanda kwenye kesi ya Lema".
Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23, 2018 baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo pamoja na viongozi wengne saba wa chama hicho.
Chanzo - EATV
Social Plugin