Vijana wa Chama cha ACT-Wazalendo wanatarajia kufanyamaandamano kesho jijini Dodoma kushinikiza Bunge kufuta azimio lake la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa vijana wa chama hicho, Karama Kaila alisema lengo la maandamano hayo ni kulitaka Bunge kufuta azimio hilo na kuendelea kufanya kazi na CAG.
“Sababu nyingine ni kulitaka Bunge kuweka kwenye shughuli za Bunge (Order Paper) upokeaji wa taarifa ya CAG ikiwa na saini ya Profesa Assad ifikapo Aprili 10 mwaka huu saa tatu asubuhi.
“Tumefikia uamuzi huu baada ya kujiridhisha kwamba uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai na Bunge kwa ujumla wake kusitisha kufanya kazi na CAG ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeanzisha mamlaka ya CAG na kuzuia kabisa kuingiliwa katika majukumu yake. Hivyo ni wajibu wa kila raia kulinda Katiba.
“Maandamano yataanzia eneo la Nyerere Square jijini Dodoma kupitia barabara ya Jamatini na kuingia barabara ya Bunge hadi Jengo la Bunge jijini Dodoma. Tumemwomba Spika wa Bunge au Naibu Spika wapokee maandamano yetu haya ya amani,”alisema Kaila
Kaila alisema kwa Mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Polisi (police ordinance) ambayo inataka kutoa taarifa kwa saa 48 kabla ya muda wa maandamano, umma ufahamu kuwa tayari wamekwisha toa taarifa ya kufanyika kwa maandamano hayo kwa OCD-Dodoma.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, amesema hana taarifa za maandamano hayo.