Shirika la Agape AIDS Control Program limeendesha kikao cha ushawishi na utetezi wa masuala ya afya ya uzazi na ujinsia katika kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ili kutokomeza mila na desturi kandamizi zinazochangia mimba na ndoa za utotoni.
Kikao hicho kimefanyika leo Jumatano Aprili 17,2019 katika shule ya msingi Shingida na kukutanisha pamoja viongozi wa ngazi ya kata,walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari,viongozi wa dini na kimila,wawakilishi wa wanafunzi na wataalamu kutoka halmashauri ya wilaya idara ya elimu na maendeleo ya jamii.
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana unaotekelezwa na Shirika la Agape kwa ufadhili wa shirika la Sida na nchini Sweden, Lucy Maganga alisema mbali na kutokomeza mila na desturi kandamizi pia washiriki wa kikao hicho watakuwa chachu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni hasa kwa watoto wa shule.
“Kupitia kikao hiki cha ushawishi na utetezi washiriki hawa wa kikao watakuwa mstari wa mbele kuishauri halmashauri ya wilaya kuongeza bajeti ya masuala ya afya ya uzazi ikiwemo miundombinu rafiki shuleni hasa vyoo,maji na vyumba vya kujisitiri kwa watoto wa kike”,alisema Maganga.
Kwa upande wake,Afisa Elimu Vifaa na Takwimu Idara ya elimu sekondari halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Lucas Mambile alisema tayari halmashauri imeshatenga bajeti kwa mwaka 2019/2020 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa kike shuleni.
Aidha alisema halmashauri inaendelea kushirikiana na jamii kujenga na kujenga vyumba vya watoto wa kike kujistiri.
Kwa upande wao,wajumbe wa kikao hicho waliahidi kuendelea kutoa elimu katika jamii ili iondokane na mila na desturi zinazochangia ukatili dhidi ya watoto lakini pia kulea watoto katika maadili mema.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape ACP Lucy Maganga akizungumza wakati wa kikao cha ushawishi na utetezi wa masuala ya afya ya uzazi na ujinsia katika kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo katika shule ya msingi Shingida- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape ACP Lucy Maganga akizungumza ambapo wajumbe wa kikao hicho watakuwa mabalozi wa kuishauri halmashauri ya wilaya kuongeza bajeti ya masuala ya afya ya uzazi ikiwemo miundombinu rafiki shuleni hasa vyoo,maji na vyumba vya kujisitiri kwa watoto wa kike.
Wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza Lucy Maganga.
Afisa Elimu Vifaa na Takwimu Idara ya elimu sekondari halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Lucas Mambile akielezea mikakati iliyopo katika halmashauri katika kusaidia masuala ya afya ya uzazi na ujinsia kwa wanafunzi ambapo alisema wametenga bajeti kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa kike shuleni.
Kaimu Ofisa Elimu wa shule za msingi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mary Maka akiwaomba viongozi wa kata na walimu kuwa na mawasiliano na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa inapobainika watoto wa kike wamepewa ujauzito ili watuhumiwa wakamatwe na kuchukuliwa hatua.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Aisha Omary akizungumza katika kikao hicho na kueleza kuwa wazazi na walezi wanatakiwa kuwa walinzi wa watoto wao na kuwalea katika maadili mema.
Wajumbe wa kikao wakimsikiliza Lucy Maganga.
Kiongozi wa kimila,Lucas Kiyenze akizungumza katika kikao hicho.
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape ACP Lucy Maganga akiangalia kazi ya kundi la walimu wakuu shule za msingi katika kata ya Usanda wakijadili mikakati mbalimbali ya kukabiliana na mimba na ndoa za utotoni.
Viongozi wa jamii wakiwemo watendaji wa vijiji na maafisa maendeleo ya jamii wakijadili mikakati ya kumaliza mimba na ndoa za utotoni kwa wanafunzi.
Wataalamu kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga idara ya elimu na maendeleo ya jamii wakijadili mikakati wanayoendelea nayo kuongeza bajeti ya masuala ya afya ya uzazi na ujinsia ikiwemo miundombinu rafiki shuleni hasa vyoo,maji na vyumba vya kujisitiri kwa watoto wa kike .
Afisa Idara ya Miradi kutoka shirika la Agape Prosper Ndaiga akifuatilia majadiliano ya wawakilishi wa wanafunzi shule za sekondari Shingita na Samuye kuhusu mikakati yao ya kutokomeza mimba kwa watoto wa shule.
Afisa Mtendaji kijiji cha Singita akiwasilisha kazi ya kundi la viongozi wa jamii kuhusu mikakati ya kutokomeza mila na desturi kandamizi zinazochangia mimba na ndoa za utotoni.Alizitaja baadhi ya mila hizo kuwa ni 'watoto kuogeshwa dawa ' samba' ili wapendwe, watoto kusindikiza bibi harusi.
Mkuu wa shule ya sekondari Samuye,Jackson Mganga akiwasilisha kazi ya kundi la wakuu wa shule namna walivyoweka mikakati kutokomeza mimba kwa watoto wa shule.
Sheikh Soud Ally wa msikiti wa Usanda akielezea mikakati ya kulea kwenye maadili ya dini watoto ili kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.
Mchungaji Lameck Makungu kutoka kanisa la AICT Busanda akielezea namna kanisa linavyotoa elimu kwa watoto ili kuepuka mimba na ndoa za utotoni.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin