Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AJALI ZA MAJINI 300 HUTOKEA KILA MWAKA MKOANI MWANZA


Na. OWM, MWANZA.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amebainisha kuwa takribani ajali za majini  zaidi ya mia tatu huripotiwa kuwa zimetokea mkoani humo. Ajali hizo ni zile ambazo huripotiwa rasmi  tu  katika mamlaka husika , aidha inasadikika zipo ajali nyingi ambazo hutokea lakini huwa haziripitiwi  kutokana na jiografia ya mkoa huo. Mkoa wa Mwanza una visiwa zaidi ya 162 ambapo kati ya Visiwa hivyo vipo ambavyo watu wanayo makazi ya kudumu na vingine watu huishi kwa muda mfupi.

Akiongea wakati  akifungua Mafunzo kwa Kamati  ya  Usimamizi wa maafa  ya mkoa huo,  yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa shughulii za maafa Leo, tarehe 17 Aprili, 2019, jiijini Mwanza, Mongella amefafanua kuwa ajali za vyombo vya usafiri hasa vya majini zinaweza kupunguzwa sana kama wamiliki na waendeshaji wa vyombo hivyo watazingatia sheria na Kanuni  zinazotawala uendeshaji wa vyombo hivyo.

“Suala muhimu la Kuzingatia ni kuhakikisha mamlaka zetu za serikali za mitaa zinaimarisha utawala bora unaotoa nafasi kwa  jamii kushiriki katika kuzuia na Kupunguza madhara ya majanga, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya maafa kutokea ikiwa ni pamoja na kutoa elimu, taarifa za tahadhari ya awali kwa wakati muafaka na kuandaa rasilimali zinazohiotajika , Ni wajibu wetu kuhakikisha sheria zinasimamiwa kikamilifu ili kuepuka maafa“ alisisitiza Mongella.

Naye Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy Matamwe, ameitaka Kamati ya Usimamizi wa Maafa ya mkoa huo  kuandaa Mkakati wa Kupunguza madhara  ya maafa pamoja na Mpango wa kujiandaa na kukabili maafa, Aidha, ameeleza kuwa  Ofisi ya waziri Mkuu imeendesha mafunzo hayo  ili kuijengea uwezo kamati hiyo ambayo ni chombo cha kisheria hapa nchini kwa ajili ya kutathimini na kutekeleza masuala ya kitaalam kuhusu usimamizi wa maafa, kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote katika mkoa.

“Upunguzaji wa madhara ya maafa ni suala mtambuka linalohusika katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii sekta zote. Suala la usimamizi wa maafa linahitaji utashi wa kisiasa na kuwajibika kitaalam, kisheria, uelewa wa umma, elimu ya kisayansi, mipango makini ya maendeleo, ufanisi wa utekelezaji wa sera, mifumo ya tahadhari inayojibu matakwa ya jamii” alisema  Kanali., Matamwe.

Mwaka jana, Mwezi Septemba, mkoa wa Mwanza ulipata maafa makubwa baada ya Kivuko cha MV. Nyerere kuzama na kupoteza maisha ya watu zaidi ya 200 na wengine 40 waliokolewa. Kufuatia maafa hayo Mkoa huo umeendelea na jitihada za kuzijengea uwezo kamati za Usimamizi wa Maafa za mkoa huo

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa shughuli za maafa, yamehudhuriwa na wajumbe wote wa Kamati ya Usimamizi wa maafa kwa kuzingatia Kifungu cha 13 cha sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 7 ya mwaka 2015.

 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com