Vijana wengi wanapohitimu wanatarajia kupata kazi ambazo wamesomea lakini kutokana na ukosefu wa ajira wanaishia kufanya kazi ambazo hawakuzitarajia.
Kuna wale ambao hutumia muda mwingi kusafiri au kubisha milango ya ofisi moja hadi nyingine kutafuta kazi.
Wataalamu wa masuala ya kazi wanasema mbinu hiyo ya kutafuta kazi imepitwa na wakati.
Hii ni kwa sababu teknolojia mpya ya mawasiliano imebadilisha mambo mengi duniani ikiwa ni pamoja na jinsi kazi zinavyotafutwa.
BBC imezungumza na Mwikali Muthiani ambaye ni mshauri wa masuala ya ajira nchini Kenya kuwapatia vidokezo vijana waliohitimu na ambao hawana kazi.
Mwikali anasema kuna kazi nyingi ambazo zimeibuka kutokana na uwepo wa teknolojia ya dijitali.Kampuni nyingi zimeng'amua umuhimu wa mitandao hiyo kwa biashara zao.
''Zamani ulikuwa unaulizwa ulikuwa mzuri kwa kitu gani ulipokuwa shule na kitu hicho ndicho kilitoa mwongozo wa kile utakachosomea chuo kikuu au taasisi ya kiufundi lakini katika ulimwengu wa sasa mambo yamebadilika'' anasema Mwikali.
Aidha ameongeza kuwa ni vyema kusomea kozi kwa mfano ya udaktari, uwakili, uhandisi, na uwanahabari miongoni mwa zingine lakini pia ni vyema kufahamu mazingira ya sasa ya kazi hasa za kidijitali
''Kazi hizi zinatarajiwa kuimarika na kuwa kubwa mwaka huu wa 2019.
Vijana wanaotafuta kazi baada ya kuhitimu vyuo vikuu wanashauriwa kutoangazia ajira zilizo zoeleka tu kama vile uhandisi, uwakili, uwalimu au udaktari.
Kwa kujiandaa vilivyo na kuwa na ujuzi wa ziada unaohitajika, unaweza kujiajiri au kujitengenezea kipato cha ziadi ikiwa umeajiriwa.
Waajiri wanatafuta nini?
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mtandao wa LinkedIn unaowaleta pamoja waajiri na waajiriwa hizi ndizo sifa zinazolengwa na waajiri mwaka 2019.
↠Ubunifu
↠Ushawishi
↠Ushirikiano
↠Kumudu mazingira tofauti ya kazi
↠Usimamizi wa muda
Sifa hizi pia zikitumiwa vizuri na vijana wataalamu wa masuala ya ajira wanasema inaweza kuwasaidia kupata nafasi za ajira katika ulimwengu wa dijitali unao waleta watu pamoja kupitia mitandao ya kijamii.
Usimamizi wa mitandao wa kijamii
Mtandao wa kijamii wa Facebook una watumiaji bilioni 1.79, Twitter ina zaidi ya watumiaji milioni 317, Instagram ina zaidi ya watumiaji zaidi ya milioni 500 na WhatsApp ina zaidi ya watumiaji bilioni Moja.
Kwa ufupi ikiwa mitandao hii ya kijamiii ingelikuwa nchi bila shaka ingelikuwa nchi iliyo na watu wengi zaidi duniani.
Kwa mujibu wa Mwikali Muthiani mshauri wa masuala ya ajira, mashirika mengi yameng'amua umuhimu wa mitandao hiyo kwa biashara zao.
Japo wazazi wanaweza kushangaa kwanini watatoto wao wanachukua muda mwingi kutumia mitandao ya kijamii huenda ikatoa nafasi za kazi hasaa mtumiaji akiwa makini na kuitumia kwa njia ya ubunifu.
Vijana waliyohitimu wanapotafuta kazi ya uhasibu, uwakili au uhandisi pia wanashauriwa kutafuta kazi za usimamizi wa mitando ya kijamii ya makampuni na biashara kubwa ambazo zimeonekana siku hizi kukumbatia majukwaa haya kuendeleza biashara hiyo.
Kazi ya kublogu.
Watu wengi siku hizi wamefungua blogu zao wenyewe na kufanya kazi majumbani mwao.
Ikiwa wewe ni mpenzi wa kufanya utafiti na kuandika basi huenda kazi hii ikakufaa na pia kukuletea kipato.
Pia unaweza kutoa ushauri wa kile ulichosomea kwa wale waotazamia kuchukua somo hilo.
Kuunda Programu Tumishi ama app
Kuna App za karibu kila kitu siku hizi.
Kwa mfano Google play store ina apps milioni 2.2 huku Apple app store ikiwa na apps milioni 2.
Hii inaashiria kuwa apps hizi ni maarufu sana duniani na zitaendelea kuongezeka.
Ukiwa na ujuzi wa kuunda app hizi bila shaka utapata nafasi ya kazi.
Mchambuzi wa data
Katika miaka kumi ililiopita mashirika yamekuwa mbioni kufanya utafiti wa namna ya kujiimarisha kibiashara.
Baadhi ya mashirika hayo yanatafuta watu walio na ujuzi wa kuchambua data na kuwasilisha maelezo kwa ufasaha kwa ajili ya kuimarisha biashara zao.
Mtaalamu wa usalama wa habari
Kazi yake ni kuhakikisha anailinda usalama wa mtandao na app za makapuni na watu binafsi kuhakikisha zipo salama dhidi ya wadukuzi.
Huku ulimwengu ukiendelea kupanuka kidigitali kazi za wataalamu hawa itaendela kuongezeka.
Mtaalamu wa Utafutaji wa Teknolojia ya Kutafuta (SEO)
Intaneti ina zaidi ya mitandao bilioni moja na mingine mingi inaendelea kubuniwa.
Japo kila mtandao unawalenga watu maalum kila mmoja angelipendelea mtandao wake uonekane mtu anapotafuta kitu kinachohusiana na taaluma yake.
Kuwa na mtandao uliyo na habari nzuri haitoshi unahitaji kuwekeza katika vitu ambavyo vitaufanya ukurasa wako kuwa maarufu kwa kuhakikisha Google inauorodhesha kwa kiwango cha juu.
Unahitaji mtaalamu wa SEO aliye na uwezo wa kuchambua mtandao wako na kukushauri vitu vinavyohitajika kufanya ili kuimarisha mtandao wako.
Mtaalamu wa kuhifadhi data mbadala.
Kazi hii inahusisha kuhifadi kazi nje ya hardrive ya komputa yako ya kazi ili kuwawezesha watu wengine kuzifikia bila kutumia kompyuta.
Hii ni teknolojia mpya inayoendelea kukua hasa ikizingatiwa kuwa kampuni nyingi zimeanza kutoa huduma zao nje ya mahali pao pa kazi, wafanyikazi wao wanahitaji kuwezeshwa kufikia taarifa muhimu za wakati wowote kutoka sehemu yoyote.
Chanzo - BBC