Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Jeshi La Polisi Mkoa Wa Dodoma Linawashikilia Watu Watatu Kwa Tuhuma Za Makosa Mbalimbali Yakiwemo Kupatikana Na Nyara Za Serikali,kughushi Na Kujipatia Mali Kwa Njia Ya Udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana April 3 ,kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma SACP.Gilles Muroto alisema tukio la kwanza ni kupatikana na nyara za serikali ambapo amebainisha mnamo tarehe 1 April, 2019 mtaa wa Kilimani wilaya na Jiji la Dodoma alikamatwa A.8070 SSGT Comas Joseph Ndasi askari magereza wa gereza la Msalato [51] akiwa na pembe za ndovu vipande 6 sawa na tembo 3 vye uzito wa kg 13 thamani ya Tsh.103,5000,000 alivyoficha kwenye mfuko akiwa anamsubiri mteja kwa ajili ya kufanya mauzo.
Kamanda Muroto ametaja tukio la pili ni la Mohammed Ahmed Hamis ambaye amekamatwa kwa kosa la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu ambapo alijipatia magari mawili ,Toyota Land cruiser V-8 Lenye namba za usajili T.366 BRX rangi Nyeusi na gari No.T.581 DKS Toyota aina ya Noah .
Kamanda Muroto amefafanua tukio lilitokea Mikocheni jijini Dar Es Salaam mwaka 2017 ambapo mtuhumiwa alijitambulisha kwa mwenye magari kuwa afisa usalama anahitaji magari kwa ajili ya kazi maalum ambapo aliandika mkataba wa kukodi magari hayo na alipoyapata alitoweka nayo na hakurejesha hadi alipokamatwa April 2 jijini Dodoma .
Mtuhumiwa aliyatumia magari hayo pia kujipatia pesa kwa watu mbalimbali kwa kuyawekea dhamana kukopa pesa kisha kulitelekeza gari na jeshi la polisi litampeleka Dar es Salaam alikoshitakiwa na atafikishwa mahakamani.
Na tukio la tatu ni la kujifanya Afisa wa serikali ambapo mnamo tarehe 26 Machi,2019 alikamatwa Ambokile Hezron Mwampulo [32] akijifanya afisa usalama wa Taifa akidanganya watu na kukusanya fedha akiwaahidi kuwapatia ajira katika idara ya usalama wa Taifa na taasisi nyingine za serikali .
Kabla ya kukamatwa alijipatia fedha kiasi cha Tsh.950,000 kutoka kwa watu wawili ambapo Tsh.550,000 kwa mtu mmoja na Tsh.400,000 kwa mtu wa pili.
Mtuhumiwa baada ya kukamatwa alifanyiwa upekuzi Nyumbani kwake Ndachi jijini Dodoma ambapo alikamatwa na nakala 15 za vyeti vya watu mbalimbali ,barua 3 za maombi ya ajira za watu tofauti na nakala ya leseni moja na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Hata hivyo jeshi la polisi limetahadharisha watu kujihadhari na matapeli wanaotumia vibaya majina ya taasisi za serikali na kuwaibia na serikali ina utaratibu wake wa kuajiri watu .