Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BRELA YAWATAKA WANASHERIA WAACHE KUWADANGANYA WAFANYABIASHARA


Wakala wa usajili wa biashara na leseni nchini (BRELA) umewataka wanasheria ambao wanawasaidia wafanyabishara kusajili biashara zao kutowadanganya na badala yake wafuate taratibu zote na kanuni zilizowekwa na mamlaka hiyo katika usajili wa biashara.

Mamlaka hiyo imesema kuwa licha ya wanasheria kutambuliwa kama watu sahihi kuwasaidia wafanyabishara kusajili biashara zao, wanatakiwa kufuata kanuni na taratibu zote zilizowekwa.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa utawala Blera Bakari Mketo,  wakati akizungumza na wafanyabishara wa mji wa Bariadi Mkoani Simiyu   ambao tayari wamesajili biashara zao kwa kutumia mfumo mpya wa usajili kwa njia ya mtandao.

Mketo alisema wamekutana na baadhi ya wafanyabishara kutoka Simiyu, ambao waliambiwa na wanasheria kuwa baadhi ya vitu havihitajiki wakati wa kusajili jambo ambalo siyo kweli.

“ Mmoja wa wafanyabishara kutoka hapa Simiyu aliambiwa na mwanasheria kuwa baadhi ya nyaraka hazitakiwi, lakini huyu mwenye biashara akatupigia simu tukamwambia siyo kweli nyaraka zote zinahitajika na akafanikiwa kusajili,” alisema Mketo.

“ Tuwaombe wanasheria, najua tunafanya kazi kwa pamoja wanatakiwa kufuata sheria na taratibu zote zilizowekwa na Brela katika kuhakikisha wanawasaidia wafanyabishara wanasajili biashara zao vizuri,” alisema Mketo.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa Brela imefanikiwa kuongeza idadi ya wafanyabishara ambao wamesajili biashara zao, ambapo kwa kipindi cha robo ya tatu iliyoisha machi 31, 2019 wamesajili makampuni 4678 sawa na asilimia 69.

Kwa upande wake, Afisa kutoka Brela, Suzan Senso alisema kupitia mfumo mpya wa usajili kwa mtandao (online Registration System), watu wengi wameanza kuuelewa na kuanza kusajili biashara zao kwa kasi.

Aliwataka wafanyabishara nchini kuendeea kusajili kwa kutumia mfumo huo, ili kuondoa usumbufu na gharama za kusajili kwenda Dar es salaam,  na zaidi akiwataka kupiga simu Brela kwa ajili ya kupata ufafanuzi wowote.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com