Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BUNGE LAKUBALI MIKUTANO YA HADHARA ISIENDELEE KUFANYIKA HADI WAKATI WA KAMPENI ZA UCHAGUZI

Bunge limekubaliana mikutano ya kisiasa isiendelee kufanyika hadi wakati wa kampeni za uchaguzi.

Hatua hiyo ilifikiwa jana baada ya wabunge kuhojiwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kutokana na swali na Mbunge wa Moshi Mjini, Jafary Michael (Chadema), aliyetaka kujua ni kwanini Serikali imezuia mikutano ya kisiasa nchini.

Michael aliuliza swali hilo juzi usiku wakati Bunge lilipokuwa limekaa kama kamati, kujadili bajeti ya Wizara ya Tamisemi, iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Wizara hiyo, Seleman Jafo.

Katika hoja yake, Michael alianza kwa kutaka Serikali imweleze ni kifungu gani cha sheria kinachozuia mikutano ya siasa huku akitaka iruhusiwe kwa kuwa taifa linakabiliwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu.

“Uchaguzi ni ‘process’ kwani unaanzia wakati wa kuchagua wagombea hadi kwenye kufanya kampeni na kupiga kura.

“Kwa kuwa kwa sasa wanasiasa hatufanyi mikutano ya siasa kwa sababu mheshimiwa rais ameizuia, naomba mniambie ni kifungu gani cha sheria kinachozuia mikutano hiyo kwa kuwa mikutano ya siasa ni haki ya wanasiasa,” alisema Michael.

Baada ya hoja hiyo kuungwa mkono na wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mjadala wa hoja hiyo ulianza kwa kuhusisha wabunge wa Chadema, Aida Kenani na Lucy Magereri.

Wengine waliochangia hoja hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na Waziri wa Zamani wa Wizara hiyo, Mwigulu Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi (Chadema).

Katika michango yao, Kenani na Magereri walitaka mikutano ya kisiasa iruhusiwe kwa sababu inatambuliwa kikatiba huku Mwigulu na Kangi wakisema hakuna sababu ya mikutano hiyo kuruhusiwa hadi uchaguzi utakapofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa upande wake, Kangi alisema hakuna mikutano ya siasa iliyozuiwa bali inaruhusiwa kwa kupata kibali kutoka kwa Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye jukumu la kulinda raia na mali zao.

Baada ya michango hiyo, Naibu Spika alilazimika kuwahoji wabunge kuona kama wanakubaliana na hoja ya Michael ya kutaka mikutano ya siasa iruhusiwe, lakini wabunge wengi walitaka mikutano hiyo isiruhusiwe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com