Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TEKNOLOJIA MPYA YATUMIKA KUMNASA CHATU MKUBWA MWENYE MIMBA

Hifadhi moja ya taifa Florida, Marekani imemnasa chatu mkubwa mwenye urefu wa futi 17 (mita 5.2) kwa kutumia teknolojia mpya ya kuwanasa viumbe wavamizi.

Nyoka jike huyo, ambaye ndiye mkubwa zaidi kuwahi kunaswa kwenye hifadhi ya Big Cypress alikuwa na uzito wa kilo 63.5 na alikuwa na 'mimba' ya mayai 73.

Chatu ambao ni wavamizi kwenye eneo hilo wanatishia pakubwa maisha ya viumbe wa asili wa jimbo la Florida.

Watafiti katika hifadhi hiyo waliwategeshea vifaa maalum madume ya chatu ili kuwatafuta majike yanayopandwa na kukaribia kutaga.

"Timu ya watafiti ilimfuatilia dume moja lililofungwa kifaa hicho na kumnasa jike huyo karibu yake," imeeleza taarifa ya hifadhi hiyo kupitia mtandao wa Facebook.

Pamoja na kuondosha nyoka wavamizi, hifadhi hiyo inatumia matokeo ya tafiti zake ili kustadi tabia za nyoka na kutengeneza njia mpya za kukabiliana nao.

Chatu wanachukuliwa kama viumbe wavamizi jimboni Florida toka walipoonekana kwa mara ya kwanza katika viunga vya Everglades miaka ya 1980.

Aina hiyo ya nyoka ina asili ya bara Asia lakini baadhi ya chatu katika jimbo hilo wanaaminika kuachiwa kutoka kwenye umiliki wa watu waliokuwa wanawafuga.

Lakini chatu wengi katika jimbo hilo walitoroka kwenye vituo vya utafiti na uzalishaji baada ya Kimbunga Andrew cha mwaka 1992.

Nyoka hawana wanyama wa asili wa mwituni wa kuwawinda katika jimbo la Florida, hivyo hakuna namna ya asili ya kupunguza namba yao.

Maelfu ya chatu yanakadiriwa kuwa wanaishi meituni katika jimbo la Florida na wamekuwa wakilaumiwa kwa kupotea kwa wanyama wengi.
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com