Serikali ya China kupitia Jeshi la Ukombozi la China, kikosi cha Anga limetoa msaada wa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Taifa kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam unaogharimu Shilingi Bilioni 56.
Ujenzi huo wa awamu ya pili ya chuo hicho utakifanya kuwa cha kisasa na miundombinu rafiki na kukiwezesha chuo hicho kudahili zaidi ya wanafunzi 100 kwa wakati mmoja baada ya ule wa awamu ya kwanza uliofanyika 2013 na kumalizika 2015.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, aliishukuru Serikali ya China kupitia jeshi la ukombozi la watu wa China kwa msaada huo kwani utasaidia kuongeza kozi na idadi kubwa ya wanafunzi.
Alisema mafunzo yanatolewa katika chuo hicho yanalenga ulinzi wa taifa na kimataifa kwa sasa na baadaye kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kisayansi katika mikakati ya maendeleo ya taifa.
Dk Mwinyi pia alisema mbali na ujenzi wa chuo hicho pia wamejenga kituo maalumu kwa mafunzo maalum ambacho kipo Mapinga Bagamoyo, Pwani na hivi karibuni wataanza ujenzi wa makao makuu ya jeshi mkoani Dodoma eneo la Kikombo.