UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2018/2019 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2019/2020. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2018/2019 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2019/2020.
3. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutokana na uongozi wao makini katika ujenzi wa Taifa letu. Ni dhahiri kuwa juhudi na maono yao katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali, zinaleta manufaa na tija kwa wananchi.
4. Mheshimiwa Spika, katika hatua ya kuboresha utendaji Serikalini, hivi karibuni Mheshimiwa Rais alifanya mabadiliko madogo kwenye Baraza la Mawaziri. Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb.), kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, na Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Kabudi (Mb.), kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ni matumaini yangu kuwa Bunge lako Tukufu litaendelea kuwapatia ushirikiano wa kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
5. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, baadhi ya waheshimiwa Wabunge na wananchi tunaowawakilisha walifikwa na misiba ya ndugu, jamaa na marafiki. Aidha, Taifa lilikumbwa na maafa kutokana na ajali za vyombo vya majini na nchi kavu. Ajali hizo ziligharimu maisha ya watu, kusababisha majeruhi na uharibifu wa mali. Mwenyezi Mungu awajalie afya njema waliopata majeraha na azipumzishe roho za marehemu mahala pema. Amina!
6. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mhe. Mohammed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mhe. Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi; na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mhe. George Boniface Simbachawene Mbunge wa Kibakwe. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge. Aidha, nichukue nafasi hii kuwapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi nzuri wanazofanya.
7. Mheshimiwa Spika, napenda pia kukupongeza wewe binafsi, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge kwa kuliongoza Bunge letu tukufu kwa weledi na umakini mkubwa. Ni imani yangu kuwa mtaendeleza hekima na weledi mlionao katika kuliongoza Bunge kuisimamia Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Vilevile, nimpongeze Katibu wa Bunge na wasaidizi wake kwa namna wanavyolisaidia Bunge kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
8. Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, nawashukuru watumishi wote wa umma kwa kutekeleza majukumu yao na kukamilisha kuandaa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2019/2020.
9. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa, napenda kuwashukuru Mhe. Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu); Mhe. Angellah Kairuki, Mbunge Viti Maalumu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji); Mhe. Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira); Mhe. Stella Alex Ikupa, Mbunge Viti Maalumu na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu) kwa kujitoa kwao katika kutekeleza majukumu na ushirikiano wanaonipa.
10. Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu ambao ni: Bibi Maimuna K. Tarishi (Waziri Mkuu na Bunge); Bwana Andrew W. Masawe (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu); Bibi Dorothy A. Mwaluko (Sera, Uratibu na Uwekezaji); na Wafanyakazi wote kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
11. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Sekta Binafsi na Taasisi za Dini kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga uchumi wa viwanda ili kufikia azma ya kuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
12. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitawashukuru wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kuniunga mkono. Niwapongeze kwa kutekeleza shughuli za maendeleo jimboni kwa ufanisi, wakati mimi Mbunge wao nikitekeleza majukumu ya kusimamia utendaji wa Serikali. Kipekee, ninamshukuru mke wangu mpendwa, Mary na familia yangu kwa uvumilivu wao wakati wote ninapokuwa nikitekeleza majukumu yangu ya kitaifa. Nawashukuru sana kwa upendo wanaoendelea kunionesha na kunitia moyo.
MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI WA MWAKA 2019/2020
13. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2019/2020 yamezingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/2020 ambao ni wa nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka wa kutekeleza Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021). Dhima ya Mpango huo ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.
14. Mheshimiwa Spika, Mpango huu unatekelezwa sanjari na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015 – 2020; Ahadi za Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na zile alizozitoa katika hotuba yake ya kuzindua Bunge hili mwezi Novemba, 2015. Vipaumbele vya mpango wa mwaka 2019/2020 ni kuendelea kuimarisha msingi wa uchumi wa viwanda; kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu; kuendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji; na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango.
15. Mheshimiwa Spika, katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Umeme wa Maji wa Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa (SGR), barabara pamoja na kukuza sekta ya anga. Utekelezaji wa miradi hiyo ya miundombinu wezeshi ya kiuchumi una lengo la kufungamanisha ukuaji wa sekta hizo na sekta nyingine hususan za biashara, kilimo na utalii.
16. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuimarika kwa sekta hizo kutachochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Nitoe rai kwa Wabunge, Wafanyabiashara na Wajasiriamali, Viongozi na Watendaji wa Serikali, Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia, Washirika wa Maendeleo, na Wananchi wote kwa ujumla, kuiunga mkono Serikali katika kutekeleza Mpango huu ili kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
17. Mheshimiwa Spika, mwezi Juni 2018, wakati akizindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II), Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema, ninanukuu,
“Tumekuwa wakimya na hatuelezi kwa kina masuala tunayofanya. Niwaombe basi viongozi wenzagu wa Serikali, kila tunapopata nafasi tuseme mambo tunayoyafanya…… Tusipofanya hivyo yanayosemwa yataonekana kuwa kweli.’’ Mwisho wa kunukuu.
18. Mheshimiwa Spika, bila kumung’unya maneno katika kipindi hiki cha zaidi ya miaka mitatu kazi kubwa tena ya kihistoria imefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini. Hivyo, niungane na Mheshimiwa Rais kuwakumbusha viongozi na watendaji wakuu wa Serikali kuwa tunalo jukumu la kuhakikisha umma wa Watanzania unafahamishwa kuhusu shughuli zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na mafanikio makubwa yanayopatikana.
19. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yamepatikana mafanikio mengi ambayo wananchi wanapaswa kufahamishwa. Aidha, Mheshimiwa Rais ameonesha dhamira ya dhati ya kisiasa katika kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea. Halikadhalika, ameweza kuhakikisha dhamira hiyo ya kujenga uchumi imara usiyo tegemezi inaenea kwa viongozi wengine, watendaji na wananchi kwa ujumla.
20. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kuendelea kukua na kuimarika kwa uchumi ambao unachochewa na jitihada za Serikali za kuwekeza kwenye miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege sanjari na kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme. Aidha, kuimarika kwa Shirika la Ndege Tanzania ni sehemu ya mafanikio hayo, ambapo Serikali imefanikisha ununuzi wa ndege sita mpya ikiwemo Dreamliner Boeing 787. Ununuzi wa ndege hizo umesaidia kuitangaza nchi, kuongeza mapato ya Serikali, fursa za ajira kwa vijana na kuwa kichocheo kwa Sekta nyingine kama vile kilimo, utalii, mifugo na uvuvi.
21. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam-Morogoro na Morogoro-Makutupora unaendelea vizuri na kwa kasi ya kuridhisha. Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wake wa Elimumsingi Bila Malipo.
Mpango huo umesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa ambao pengine wangekosa fursa ya kupata elimu kutokana na kushindwa kulipa ada na michango mingine. Hii imejidhihirisha kutokana na ongezeko la uandikishaji wanafunzi kutoka milioni 1.57 mwaka 2015 hadi milioni 2.08 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 35.2. Kwa mwaka 2019 uandikishaji ulikuwa milioni 1.58. Kutokana na takwimu hizi ni dhahiri kuwa kwa sasa watoto wote wanaofikia umri wa kwenda shule wanaandikishwa bila kikwazo chochote.
22. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya nchi nzima, kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 31 mwaka 2015/2016 kufikia Shilingi Bilioni 270 mwaka 2018/2019. Ongezeko hilo limeongeza upatikanaji wa dawa muhimu kufikia asilimia 96 katika mwaka 2018/2019. Aidha, tiba za kibingwa zinatolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali mpya za Rufaa za Benjamini Mkapa na Mloganzila.
Hospitali hizo zinatoa huduma za kibingwa zikiwemo upasuaji wa moyo, ubongo na uti wa mgongo ambazo awali zilipatikana nje ya nchi na hivyo, kuigharimu Serikali fedha nyingi.
23. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuanza kwa ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwenye Bonde la Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) pamoja na kuendelea na kazi ya kusambaza umeme vijijini. Mafanikio hayo na mengine yatafafanuliwa kwa kina na sekta husika wakati watakapowasilisha bajeti zao.
24. Mheshimiwa Spika, bajeti hii ya nne ya Serikali ya Awamu ya Tano, ni bajeti inayolenga kukamilisha kwa kiasi kikubwa yale tuliyowaahidi wananchi wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiomba ridhaa ya kuongoza Dola katika Uchaguzi Mkuu Mwaka 2015. Kwa msingi huo, nisisitize kwamba, Sekta na Taasisi zote za Serikali zikamilishe utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 - 2020.
25. Mheshimiwa Spika, kwa kasi ambayo Serikali yetu imeonesha na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha zaidi ya miaka mitatu, ni matarajio yetu kuwa ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 zitakamilishwa ifikapo mwaka 2020.
HALI YA UCHUMI
26. Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kueleza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha uchumi na mafanikio yanaonekana. Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2018, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2017.
Ukuaji huu wa uchumi umechangia kutoa ajira na kuongeza mapato ya Serikali yaliyowezesha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
27. Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei ulipungua kutoka wastani wa asilimia 4.0 Januari, 2018 hadi asilimia 3.0 Januari, 2019. Kiwango hiki cha chini cha mfumuko wa bei kimetokana na kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti.
28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuimarisha na kujenga misingi na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuwa na mapato endelevu kwa ajili ya kugharamia matumizi yake. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia jukumu lake la msingi la kutafuta mapato kutoka vyanzo vya ndani na nje na kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za umma kupitia bajeti ya Serikali itakayowasilishwa hapa Bungeni mwezi Juni 2019.
Usimamizi wa Mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa
29. Mheshimiwa Spika, ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka 2016/2017, umeonesha kuwa Halmashauri 166 kati ya 185 zimepata hati safi sawa na asilimia 90, Halmashauri 16 zimepata hati zenye shaka ikilinganishwa na Halmashauri 32 mwaka 2015/2016. Matokeo hayo yanaonesha kuimarika kwa usimamizi wa fedha pamoja na uwajibikaji wa watendaji na Viongozi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Nazielekeza Halmashauri zote nchini kuendelea kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha zinazopelekwa katika halmashauri hizo ili kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Vitambulisho vya Wajasiriamali Wadogo
30. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa wajasiriamali wadogo nchini katika kuchangia pato la Taifa na kukuza uchumi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa vitambulisho 670,000 kwa ajili ya wajasiriamali wadogo ambao mitaji yao haizidi Shilingi milioni nne. Lengo la kutoa vitambulisho hivyo vyenye kugharimu shilingi 20,000 kwa kila kimoja ni kuwatambua, kuwaandalia maeneo ya kufanya biashara bila usumbufu wowote na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza mapato ya ndani.
31. Mheshimiwa Spika, hadi tarehe 10 Machi 2019, jumla ya vitambulisho 496,221 sawa na asilimia 74 vilikuwa vimegawiwa kwa wajasiriamali wadogo katika mikoa yote nchini. Aidha, tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo, Serikali imekusanya Shilingi bilioni 9.9.
Naendelea kusisitiza kwamba viongozi na watendaji wote katika Serikali za Mitaa kuwapatia ushirikiano wa kutosha wajasiriamali wadogo na kutowabughudhi.
HALI YA SIASA
32. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya kisiasa na demokrasia imeendelea kuimarika nchini. Katika mwaka 2018/2019, zilifanyika chaguzi ndogo za wabunge katika majimbo 10 na madiwani katika kata 231 kwenye maeneo mbalimbali nchini. Majimbo yaliyoshiriki uchaguzi ni Buyungu, Korogwe, Monduli, Ukonga, Liwale, Serengeti, Simanjiro, Ukerewe, Babati Mjini na Temeke. Katika chaguzi hizo, Wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walishinda majimbo yote na kata 230 ambapo CHADEMA walishinda Kata moja. Nichukue fursa hii, kuvipongeza vyama vyote vilivyoshiriki katika chaguzi hizo, na kipekee naipongeza CCM kwa ushindi mkubwa ilioupata katika chaguzi hizo.
33. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeendelea kusimamia na kukuza mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ili kudumisha amani, utulivu na mshikamano uliopo katika nchi yetu. Katika kutekeleza jukumu hilo, Sheria ya Vyama vya Siasa Namba.5 ya Mwaka 1992 Sura ya 358 imefanyiwa marekebisho ili kuondoa mapungufu yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji na hivyo kuiwezesha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Hii ni mara ya saba kwa Sheria hii kufanyiwa marekebisho tangu kutungwa kwake mwaka 1992 kwa kuzingatia mahitaji ya wakati husika. Nitoe wito kwa Vyama vya Siasa nchini kuendesha shughuli zao za siasa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria hiyo ili kuwa na uwazi, uwajibikaji, kudumisha amani na kukuza demokrasia nchini.
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kuelimisha umma kuhusu utekelezaji wa Sheria hiyo, kusimamia vyama vya siasa nchini na kuhakikisha vinajiendesha kama Taasisi. Vilevile, itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010 katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019
35. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019 ambao ni uchaguzi wa sita tangu kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1994 chini ya Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa. Hivi sasa, Serikali imekamilisha zoezi la uhakiki wa maeneo ya utawala ambayo yatashiriki kwenye uchaguzi huo katika Halmashauri zote 185. Lengo la uhakiki huo ni kujiridhisha na usahihi wa maeneo hayo kwa idadi na majina ili kufanikisha maandalizi ya bajeti na mahitaji mengine muhimu ya uchaguzi huo.
36. Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imekamilisha maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi zitakazotumika kusimamia uchaguzi huo mwezi Oktoba 2019. Nitoe wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi katika upigaji kura ili waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua au kuchaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwezi Oktoba 2019. Serikali kwa upande wake itaendelea kuhakikisha kunakuwepo na mazingira salama na tulivu kwa kipindi chote cha uchaguzi.
Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020
37. Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza Maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pamoja na uhakiki wa vituo vya Uandikishaji wa Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2020. Hadi sasa, Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura zimeandaliwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 792 na 793 ya tarehe 28 Desemba 2018.
Aidha, uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura nao umekamilika, ambapo kwa upande wa Tanzania Bara vituo vimeongezeka kutoka 36,549 vilivyokuwepo mwaka 2015 hadi kufikia vituo 37,407 mwaka 2018, sawa na ongezeko la vituo 858. Kwa upande wa Zanzibar vimeongezeka vituo 27 kutoka 380 vya mwaka 2015 hadi kufikia vituo 407 mwaka 2018. Natoa wito kwa wananchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha mara zoezi hilo litakapoanza.
BUNGE
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Bunge limetimiza wajibu wake wa kikatiba na kikanuni kwa kufanya mikutano mitatu na huu ukiwa wa nne. Katika mikutano hiyo, masuala mbalimbali yamejadiliwa na kutolewa ufafanuzi na Serikali ikiwemo hoja za Kamati za Kudumu za Bunge. Aidha, jumla ya maswali ya msingi 374 yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali yakijumuisha pia maswali ya nyongeza 978.
Katika utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, maswali ya msingi 19 pamoja na moja la nyongeza yaliulizwa na kujibiwa. Vilevile, Miswada ya Sheria ya Serikali 12 iliwasilishwa, kujadiliwa na kuridhiwa na Bunge kuwa Sheria za nchi. Maazimio ya Bunge matatu pamoja na Itifaki za kimataifa nne ziliridhiwa na kupitishwa na Bunge kwa utekelezaji wa Serikali. Ni matumaini ya Serikali kwamba Bunge lako tukufu litaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi kikatiba la kutunga sheria na kuisimamia Serikali.
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Ofisi ya Bunge itafanya ukarabati katika Ukumbi wa Bunge na Ukumbi wa Msekwa, kusimika mitambo ya Studio ya Bunge na kuboresha miundombinu mingine ya Ofisi zake ikiwa ni pamoja na Usimikaji wa mitambo ya usalama katika majengo ya Bunge na kukamilisha ujenzi wa nyumba za viongozi wa Bunge.
MAHAKAMA
40. Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuona haki inatendeka nchini. Ili kutekeleza dhamira hiyo, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa kufanya maboresho ya kiutendaji kwa vyombo vya maamuzi ikiwemo Mahakama.
41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019 jumla ya mashauri 231,927 yalifunguliwa katika mahakama zote nchini hadi Februari, 2019. Kati ya hayo, mashauri 224,950 sawa na asilimia 96 yamesikilizwa na kutolewa hukumu. Ufanisi huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa Majaji 21 wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu. Vilevile, kukamilika kwa miundombinu muhimu ya Mahakama imewezesha kuongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi.
42. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanzisha huduma ya mahakama inayotembea ikiendesha shughuli zake kwa kutumia magari maalumu katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya mahakama. Huduma hii imesaidia kuongeza kasi ya Mahakama kusimamia haki kwa kutumia mifumo rafiki ya utoaji haki nchini. Aidha, mahakama nchini zimeanza kutekeleza utaratibu wa kutoa nakala za hukumu bure kwa wananchi kupitia huduma ya Posta Mlangoni ambapo hadi Februai 2019, jumla ya nakala 5,942 zimetolewa. Katika mwaka 2019/2020, Serikali itawajengea uwezo watumishi wa mahakama; kuimarisha mifumo ya utoaji haki; na ukarabati wa miundombinu ya Mahakama nchini.
SERIKALI KUHAMIA DODOMA
43. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuhamishia shughuli zake Jijini Dodoma tangu Mheshimiwa Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atoe tamko la Serikali kuhamia Dodoma tarehe 23 Julai 2016. Mpango huo, unatekelezwa kwa awamu mbalimbali zinazojumuisha uhamisho wa watumishi, ujenzi wa makazi na miundombinu, uboreshaji wa huduma za jamii na ujenzi wa Mji wa Serikali.
44. Mheshimiwa Spika, katika awamu hizo, jumla ya watumishi 8,883 wa Wizara na Taasisi za Serikali wamehamia Dodoma. Serikali inaendelea kukamilisha taratibu za kuhakikisha watumishi waliobaki wanahamia Dodoma. Aidha, ujenzi wa majengo ya Ofisi za awali za Wizara 23 likiwemo Jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali umekamilika.
45. Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Julai 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikabidhi hati miliki 64 za viwanja kwa mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Kibalozi Jijini Dodoma. Niendelee kutoa wito kwa Mashirika ya Kimataifa na Mabalozi wahamishie Ofisi zao Jijini Dodoma.
46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendeleza ujenzi wa mji wa Serikali na Jiji la Dodoma kwa kuimarisha huduma za jamii, miundombinu ya masoko, barabara, mfumo wa maji safi na maji taka. Natoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika Jiji la Dodoma kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Jiji la Dodoma.
Maendeleo ya Sekta Binafsi
47. Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza jukumu lake la msingi la kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa Sekta Binafsi ili iweze kutoa mchango uliokusudiwa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Sekta Binafsi inashiriki ipasavyo katika maendeleo ya Taifa letu kwa kutengeneza ajira, kuongeza uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma na kukuza uchumi.
48. Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha malengo hayo, Serikali inachukua hatua mbalimbali za makusudi za kuboresha sheria na mifumo ya kodi, kuimarisha miundombinu pamoja na kuendeleza mazungumzo na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa. Mathalan, tarehe 22 Januari 2019, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokutana na wadau wa Sekta ya Madini alitoa maelekezo kwa viongozi na watendaji wa Serikali kuhakikisha wanachukua hatua za kukuza Sekta hiyo.
49. Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Februari 2019, nilikutana na wawakilishi wa wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa lengo la kujadiliana kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao. Katika Mkutano huo, niliambatana na viongozi na watendaji wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kutoa ufafanuzi na kutatua kero mbalimbali zilizowasilishwa na wafanyabiashara hao. Aidha, Serikali inafarijika kupata mrejesho kutoka Sekta Binafsi kwamba mahusiano ya pande hizi mbili yanaendelea kuimarika. Natoa wito kwa viongozi na watendaji wote wa Serikali kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki kwa Sekta Binafsi.
Uwekezaji
50. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji katika kujenga uchumi wa nchi yetu, Serikali imeendelea kutoa uzito katika uwekezaji ambapo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alichukua hatua ya kuhamishia masuala ya uwekezaji katika Ofisi yangu na kuteua Waziri wa Nchi kushughulikia masuala ya uwekezaji. Vilevile, Mheshimiwa Rais amekihamishia kituo cha Uwekezaji nchini kuwa chini ya Ofisi yangu. Hatua hizo zitasaidia kuimarisha uratibu wa masuala ya uwekezaji nchini na kuhakikisha kwamba changamoto mbalimbali zilizopo zinashughulikiwa kwa ufanisi ili kuwezesha nchi yetu kuvutia zaidi mitaji ya uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi yetu.
51. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha na kuvutia wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi ili wawekeze nchini. Katika kuhamasisha uwekezaji kutoka nje, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi za Balozi zetu za Nje na Balozi za nje zilizopo hapa nchini, kiliandaa na kuendesha makongamano na semina mbalimbali zilizowalenga wawekezaji kutoka ndani na nje.
52. Mheshimiwa Spika, uhamasishaji huo, umefanikisha kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali za kimkakati. Hadi kufikia Februari, 2019 jumla ya miradi mipya 145 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC). Kati ya miradi hiyo, miradi 104 sawa na asilimia 72 inamilikiwa na wawekezaji wa ndani; miradi 38 sawa na asilimia 26 inamilikiwa na wawekezaji kutoka nje na miradi mitatu sawa na asilimia 2.01 ni ya ubia. Miradi hiyo, inatarajia kuwekeza mitaji ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.84 na kuzalisha ajira mpya 15,491.
53. Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuvutia uwekezaji nchini, hali ya uwekezaji imeendelea kuimarika ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha kuwa Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji kati ya nchi za Afrika Mashariki.
54. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka 2018 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inaonesha kuwa Tanzania imevutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 1.18, ikifuatiwa na Uganda Dola za Marekani Bilioni 0.7 na Kenya Dola za Marekani Bilioni 0.67.
55. Mheshimiwa Spika, taarifa nyingine ya “The Africa Investment Index (AII) 2018” inaonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 za Afrika katika kutoa fursa za masoko na vivutio vya uwekezaji. Vilevile, taarifa ya “Where to Invest in Africa” ya mwaka 2018, inaonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya saba kati ya nchi 52 zinazovutia zaidi kwa uwekezaji Barani Afrika. Napenda kutoa rai kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazojitokeza kutokana na ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na pia uwekezaji wa sekta ya umma kwenye miundombinu kwa kuthubutu kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.
56. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo kutekeleza mapendekezo ya Mpango Kazi Jumuishi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini; kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Kilimo
Hali ya Upatikanaji wa Chakula
57. Mheshimiwa Spika, hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2017/2018 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019 imeendelea kuimarika kutokana na hali nzuri ya mvua katika maeneo mengi ya nchi, kuongezeka kwa tija na uzalishaji. Uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia tani milioni 16.89 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya tani milioni 13.57. Hivyo, nchi ina ziada ya chakula ya tani milioni 3.32 za mazao yote. Hii ni hatua nzuri na ya kujivunia kwani usalama wa chakula ni usalama wa nchi.
Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)
58. Mheshimiwa Spika, tarehe 4 Juni 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Programu hiyo, inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo kwa maana ya mazao, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima hususan wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.
59. Mheshimiwa Spika, ikiwa sehemu ya Utekelezaji wa ASDP II, Serikali inaiimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili kuwa benki mama itakayoongoza mipango inayolenga kutatua changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini. Lengo la Serikali ni kuifanya TADB kuwa benki ya mfano na ya kisasa katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini kutoka kilimo cha mazoea cha kujikimu kwenda katika kilimo cha kibiashara na uzalishaji wenye tija katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
60. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari 2019, TADB imetoa mikopo ya shilingi bilioni 100.7 ikilinganishwa na shilingi billioni 10 mwaka 2017. Mikopo hiyo, imewanufaisha zaidi ya wakulima na wafugaji milioni moja nchi nzima. Aidha, TADB tayari imekwishafungua Ofisi mbili za Kanda Jijini Dodoma na Mwanza. Rai yangu kwa Menejimenti na Bodi ya TADB ni kwamba kamilisheni ufunguzi wa ofisi zilizopangwa kwa wakati ili kutatua changamoto za upatikanaji wa pembejeo na miundombinu duni ya uzalishaji, usafirishaji, uchakataji wa mazao na masoko zinazokabili wakulima wadogo nchini.
Uzalishaji wa Mazao Makuu ya Biashara
61. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao makuu ya kimkakati yakiwemo chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku umeimarika kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ikiwemo kuimarisha ushirika. Kwa mfano, uzalishaji wa zao la pamba uliongezeka kutoka tani 132,934 mwaka 2017/2018 hadi kufikia tani 222,039 mwaka 2018/2019 wakati uzalishaji wa zao la Kahawa uliongezeka kutoka tani 45,245 hadi kufikia tani 65,000. Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa mazao hayo na mengine kwa kuwa ndiyo mhimili wa kutoa malighafi za kuendesha viwanda na yana mnyororo mpana wenye fursa ya kutoa ajira nyingi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
Mkakati wa Uzalishaji wa Zao la Chikichi
62. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya kununua mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Aidha, uzalishaji mdogo wa zao la chikichi ni miongoni mwa sababu za kushindwa kujitosheleza kwa mahitaji ya mafuta ya kula nchini. Kutokana na changamoto hiyo, Serikali imeamua kuweka nguvu kubwa kwenye uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ili kuondokana na utegemezi na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni.
63. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeanza kuimarisha kilimo cha zao la chikichi hususan katika mkoa wa Kigoma ili kusaidia upatikanaji wa mbegu bora za chikichi. Lengo ni kuzalisha na kusambaza kwa wakulima miche ipatayo milioni 20 katika kipindi cha miaka minne (2018/2019 hadi 2021/2022). Vilevile, Serikali imeamua kukifanya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kihinga, mkoani Kigoma kuwa Kituo cha Utafiti wa Mbegu Bora za Chikichi.
64. Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba maamuzi haya ya Serikali yameanza kuzaa matunda. Mathalan, hadi kufikia Februari 2019, Kituo cha Kihinga kimezalisha mbegu 4,747 ambazo zimefanyiwa uoteshwaji wa awali. Katika mwaka 2019/2020, Serikali imepanga kuzalisha miche ya chikichi milioni 5. Ni matarajio ya Serikali kwamba usimamizi mzuri wa Mkakati huo wa miaka minne utalisaidia Taifa kuondokana na uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje, kutengeneza fursa mbalimbali za ajira na kuwaongezea kipato wakulima wa chikichi.
Mifugo na Uvuvi
65. Mheshimiwa Spika, Serikali inaimarisha sekta ya mifugo na uvuvi kwa kushirikiana na sekta binafsi. Katika mwaka 2018/2019, Serikali ilianzisha Dawati la Sekta Binafsi kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji katika sekta za mifugo na uvuvi. Lengo la Serikali ni kuongeza uwekezaji wenye tija utakaowezesha wafugaji na wavuvi kuongeza kipato, kuzalisha malighafi za kutosha za viwanda na kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa.
66. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba Sekta ya Mifugo na Uvuvi inakua na mnyororo mpana wa ongezeko la thamani kwa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao ya mifugo na uvuvi. Hadi sasa, viwanda 99 vya kusindika mazao ya mifugo vimeanzishwa vikiwemo viwanda 17 vya nyama, 76 vya maziwa na 6 vya ngozi.
67. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuweka msisitizo katika kuwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji kwenye viwanda; kuimarisha usimamizi wa rasilimali katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu; na kuimarisha miundombinu na kukuza biashara ya mazao ya uvuvi.
Utalii
68. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii imeendelea kuimarika na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Pato la Taifa na kuongeza ajira. Mathalan, idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2018 imeongezeka na kufikia watalii milioni 1.49 ikilinganishwa na watalii milioni 1.33 walioingia nchini mwaka 2017. Vilevile, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.43 mwaka 2018 ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 2.19 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 7.13.
69. Mheshimiwa Spika, katika kutangaza vivutio vya utalii, mwaka 2018/2019 Serikali imeanzisha Chaneli ya Utalii (Tanzania Safari Channel) ili kuvutia watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea vivutio vyetu. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha Chaneli hiyo kwa kuipatia wataalamu, vifaa na vitendea kazi stahiki. Chaneli hii itaendeleza taswira na sifa nzuri ya Tanzania kimataifa sambamba na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa biashara ya utalii nchini.
70. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya utalii kwa kuihamasisha na kuiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta hiyo. Aidha, sanjari na kutangaza utalii, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo usafiri wa anga ili kuvutia watalii wengi zaidi nchini.
Viwanda
71. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa dhima ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu wetu. Katika kipindi cha miaka mitatu ya kutekeleza azma hii, Serikali inaridhika kuona hamasa na uthubutu wa Watanzania kwa kushirikiana na nchi rafiki kuhamasika na kuwekeza katika ujenzi wa viwanda. Katika mwaka 2018/2019, Serikali imeendelea kuhamasisha Sekta Binafsi kuanzisha na kuendeleza viwanda nchini. Vipaumbele ni katika viwanda vinavyotumia malighafi za hapa nchini; viwanda vinavyozalisha ajira kwa wingi; na kuendelea kubainisha maeneo ya viwanda katika mikoa yote na kuendeleza maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZ & SEZ) pamoja na kongani za viwanda nchini.
72. Mheshimiwa Spika, moja ya malengo ya Serikali ni kuinua uchumi wa wananchi kwa kuwawezesha kupata mitaji ya kufanyia kazi zao. Katika kufanikisha malengo hayo, Serikali kupitia SIDO imeendelea kuratibu Mfuko wa Wafanyabiashara Wananchi yaani “National Entrepreneurship Development Fund (NEDF)”. Katika mwaka 2018/2019, jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.74 ilitolewa ambapo mikopo 520 yenye thamani ya Shilingi milioni 788 ilitolewa kwa wanawake na mikopo 493 yenye thamani ya Shilingi milioni 958.8 ilitolewa kwa wanaume.
73. Mheshimiwa Spika, ili kutimiza azma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, Serikali inaendelea kuandaa mipango kabambe ya miji na kuhakikisha, maeneo yanatengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda. Katika mipango kabambe ya miji 17 iliyokamilika na ile inayoandaliwa, jumla ya ekari 127,859 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya viwanda. Vilevile, kwa kushirikiana na Mamlaka za Upangaji za Halmashauri za Wilaya za Kibaha na Kilosa, Serikali imetenga hekta 2,710 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo. Pia, Mamlaka za Upangaji zimeagizwa kuzingatia utengaji wa asilimia 10 ya kila eneo la Mpango Kabambe wa Mji kwa ajili ya uwekezaji wa biashara na viwanda.
74. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali imeandaa Mwongozo wa Tathmini ya Mazingira Kimkakati ambao utawezesha mpango wa uchumi na viwanda kufanyiwa Tathmini ya Mazingira Kimkakati. Katika maboresho ya kanuni yaliyofanyika, yanampa Waziri mwenye dhamana ya mazingira mamlaka ya kutoa vibali vya muda kwa ajili ya miradi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na hivyo kuboresha taratibu za uwekezaji wa viwanda nchini.
75. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuhuisha, kuboresha na kutekeleza Sera, Sheria, Taratibu na Mikakati ya Maendeleo ya Viwanda, biashara na masoko hususan kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini; kuimarisha na kusimamia mfumo wa biashara ya ndani; na kutumia kikamilifu fursa za masoko zenye unafuu wa kodi na usio wa kodi. Vilevile, Serikali itaendelea kujenga uwezo wa Taasisi za utafiti zinazohusika na maendeleo ya viwanda na kuhamasisha uanzishaji na maendeleo ya viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati.
Madini
76. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Madini na mchango wake katika kukuza uchumi, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutoa kipaumbele katika kulinda rasilimali za madini na kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania. Katika hilo tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuelekeza Mamlaka za Serikali kutunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umiliki wa Maliasili Na. 5 ya Mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Katika Mikataba ya Maliasili za Nchi Na. 6 ya Mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura 123.
77. Mheshimiwa Spika, Serikali pia, imeendelea kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo ya uchimbaji; kuwakopesha zana za uchimbaji; kuwapatia utaalamu na matumizi ya teknolojia katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Aidha, Serikali inashughulikia kero zinazowakabili wachimbaji wadogo ili waweze kuendesha shughuli zao za uchimbaji mdogo na kunufaika na rasilimali ya madini.
78. Mheshimiwa Spika, mfano mzuri wa utekelezaji wa dhamira hiyo nzuri ya Serikali ni kitendo cha Mheshimiwa Rais kukutana na kufanya mazungumzo na wachimbaji wadogo mwezi Januari 2019, Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua kero zao. Vilevile, Mheshimiwa Rais alielekeza kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya zuio kwa wachimbaji wadogo maelekezo ambayo tayari yamefanyiwa kazi.
79. Mheshimiwa Spika, kufutwa kwa kodi na tozo hizo kunatarajiwa kupunguza utoroshwaji wa madini; kuwatambua wachimbaji wadogo kupitia masoko ya madini yatakayoanzishwa na kuwapunguzia gharama za uendeshaji wa shughuli zao. Hatua hiyo pia, itaongeza wigo wa mapato kwa nchi kwa kuwa sasa madini yatauzwa katika utaratibu unaotambulika rasmi. Rai yangu kwa wachimbaji wote wadogo, endeleeni kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kutekeleza majukumu yenu.
80. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kukuza soko la ndani la madini kwa kuvutia wawekezaji na kuhamasisha shughuli za uongezaji wa thamani madini nchini. Pia, mkazo utawekwa katika kusimamia uanzishwaji na uendeshaji wa masoko ya madini yenye ushindani mkubwa ili kudhibiti utoroshaji wa maliasili hiyo. Aidha, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo, huduma za utafiti, teknolojia, mitaji na masoko.
Nishati
81. Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga uchumi wa viwanda sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme ya kutosha, uhakika na nafuu. Kwa kutambua hilo, Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme yenye lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na ukuaji wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
82. Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba, 2018 niliungana na Mhe. Dkt. Mostafa Madbouly Waziri Mkuu wa Jamhuri ya kiarabu ya Misri kushuhudia uwekaji saini mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme wa MW 2,100 kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya JV Arab Contractors & Elsewedy Electric ya Misri. Mradi huo unaotarajiwa kukamilika 2021/2022 utawezesha ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha upatikanaji wa umeme tena kwa bei nafuu.
83. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa Februari, 2019 uwezo wa jumla wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umeongezeka kutoka takriban MW 1,205 mwaka 2015 hadi kufikia MW 1,614 mwaka 2019. Ongezeko hilo limewezesha kuwa na umeme wa ziada wa wastani wa zaidi ya MW 300.
84. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza kwa mafanikio makubwa mpango wa usambazaji wa umeme vijijini. Katika mwaka 2018/2019, vijiji 1,782 vimeunganishwa na umeme. Aidha, tangu kuanza kwa usambazaji wa umeme vijijini, tayari vijiji 5,746 vimeunganishiwa umeme kati ya vijiji 12,268 vilivyopo nchini; sawa na takriban asilimia 47 ya vijiji vyote.
85. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme wa maji na kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu ambapo vijiji vyote vitakavyosalia vitapatiwa umeme.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
86. Mheshimiwa Spika, rasilimali ardhi ina umuhimu wa pekee katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na uzalishaji mali. Kutokana na umuhimu huo, Serikali inachukua hatua madhubuti za kuiendeleza rasilimali hii kwa kuipanga, kuipima na kuimilikisha kwa taasisi na wananchi kama inavyopaswa. Katika mwaka 2018/2019, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi, (2013 – 2033) ambapo jumla ya mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 263 katika Wilaya 45 imeandaliwa.
87. Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia migogoro mbalimbali ya matumizi ya ardhi ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro, Wizara za kisekta zimeanza kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais tarehe 15 Januari, 2019.
Maelekezo hayo, ni pamoja na kurasimisha vijiji 351 vilivyokuwemo kwenye hifadhi za misitu na mapori tengefu yaliyokosa sifa pamoja na kufuta jumla ya ekari 121,032 za ranchi na mashamba yaliyotelekezwa. Hatua hizi zimewezesha wananchi kupata ajira na pia kupata sehemu za kufanya shughuli za kilimo, ufugaji na makazi.
88. Mheshimiwa Spika, kupitia Mradi wa Mikopo ya Nyumba unaosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania, Serikali imeshusha riba ya mikopo inayotolewa kwa mabenki na taasisi za fedha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.5 na jumla ya wananchi 4,174 wamenufaika na mikopo inayotolewa na benki na taasisi hizo za fedha. Aidha, Mfuko wa Mikopo Midogo Midogo ya Nyumba ulio chini ya Benki Kuu umeongezewa mtaji wa dola za Marekani milioni 18 ambapo taasisi za fedha tano zimepatiwa mtaji wa shilingi bilioni 13.87 kwa ajili ya kukopesha wananchi wa kipato cha chini kwa masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.
89. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali kwa mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi, (2013 – 2033), ikiwemo kupima, kupanga na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini na kutekeleza programu ya kurasimisha makazi katika miji mbalimbali. Aidha, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda hifadhi na vyanzo vya maji ili kuleta manufaa endelevu kwa Taifa na pia kuhimiza kilimo na ufugaji wenye tija utakaoleta maendeleo endelevu.
Barabara
90. Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami ili kuimarisha na kurahisisha mawasiliano ya usafiri na usafirishaji wa watu, bidhaa na mazao mbalimbali. Hadi kufikia Februari 2019, jumla ya kilomita 266.78 za barabara kuu na za mikoa zimekamilika na kilomita 392.2 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami. Halikadhalika, Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja matano katika Mto Lukuledi (Lindi), Mara (Mara), Sibiti (Singida), Momba (Rukwa na Songwe) na Mlalakuwa (Dar es Salaam) na ujenzi wa madaraja 8 unaendelea katika sehemu mbalimbali nchini. Ujenzi wa miradi hii, utatoa fursa mbalimbali kwa wananchi kupata ajira pamoja na kupata soko kwa bidhaa na mazao yao.
91. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza ujenzi wa miradi ya barabara inayolenga kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa barabara kuwezesha mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge kwa kiwango cha changarawe kutoka Ubena Zomozi mpaka Selous (km 177.6); na ukarabati wa barabara ya kutoka Kibiti – Mloka – Selous (km 201). Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa barabara kutoka Tabora – Mpanda (km 370), Makutano – Natta – Mugumu – Loliondo (km 239), Loliondo – Mto wa Mbu (km 213), na barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo – Lumecha (km 464).
Kuondoa Msongamano wa Magari Jijini Dar es Salaam
92. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kuondoa msongamano wa magari kwenye Jiji la Dar es Salaam, ili kurahisisha usafiri na usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi. Miradi iliyokamilika ni ujenzi wa barabara ya juu ya Mfugale na barabara za mlisho. Miradi inayoendelea na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni Ujenzi wa Barabara za Juu kwenye makutano ya Ubungo (Ubungo Interchange), Upanuzi wa barabara ya Kimara Mwisho – Kiluvya (km 19.2) kutoka njia mbili kuwa nane, Daraja Jipya la Selander na Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya II na III.
93. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa mikoa ambayo haijaunganishwa na barabara kuu za lami.
Vivuko
94. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali imekamilisha ujenzi wa vivuko viwili vipya vya Magogoni – Kigamboni na Kigongo - Busisi. Aidha, ujenzi wa vivuko vipya vinne vya Kayenze – Bezi, Nyamisati – Mafia, Nkome - Chato – Muharamba na Bugolora - Ukara unaendelea. Vilevile, Serikali imekamilisha ukarabati wa kivuko cha MV Pangani II (Pangani) na ukarabati mkubwa wa vivuko viwili vya MV Sengerema (Mwanza) na MV Kigamboni (Dar es Salaam).
95. Mheshimiwa Spika, Serikali pia, imekamilisha ujenzi wa maegesho ya Bwina (Geita) na Lindi – Kitunda (Lindi). Pia, taratibu za manunuzi kwa ajili ya ujenzi wa maegesho ya Nyamisati – Mafia (Pwani), Kayenze - Bezi (Mwanza) na Mlimba - Malinyi (Morogoro) zinaendelea.
Viwanja vya Ndege
96. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usafiri wa anga nchini Serikali inakamilisha ujenzi wa Jengo la Tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini
Dar es Salaam. Jengo hilo ambalo hadi kufikia Februari 2019 ujenzi wake umefikia asilimia 95.5 litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka pindi litakapokamilika Mei 2019.
97. Mheshimiwa Spika, jengo hilo linatarajiwa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu cha utalii kwa kuwezesha watalii wanaoingia nchini kuelekea katika maeneo mbalimbali ya vivutio vyetu na nchi jirani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Mpango huu wa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu cha utalii unakwenda sambamba na maboresho ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL). Lengo ni kuhakikisha watalii wanaoingia nchini wanakuwa na usafiri wa uhakika kuvifikia vivutio vyetu na kuelekea katika nchi za jirani. Kwa kufanya hivyo, shughuli za kiuchumi nchini zenye kufungamana na utalii hususan ajira, huduma, biashara na usafirishaji zitaimarika na kuwaongezea kipato watu wetu.
98. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza dhamira ya kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kisasa, Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato. Lengo la Serikali ni kulifanya Jiji la Dodoma ambalo ndilo Makao Makuu ya Nchi kuwa kitovu cha mawasiliano na maeneo mengine nchini. Kwa sasa kazi inayoendelea ni kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Kiwanja kuendana na hadhi na mahitaji ya Makao Makuu ya Nchi.
99. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea na ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vingine vya ndege vya Songwe, Kigoma, Sumbawanga, Shinyanga, Tabora, Mtwara, Songea, Nachingwea, Lindi, Iringa na Musoma ambavyo viko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Reli
100. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa awamu ya kwanza wa Reli ya Kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 42.8 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2019. Halikadhalika, ujenzi wa awamu ya pili wa reli hiyo ya kisasa kutoka Morogoro hadi Makutupora Jijini Dodoma umefikia asilimia 6.07. Hadi sasa Mradi kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora umeshaajiri wafanyakazi wazawa wapatao 6,335 sawa na asilimia 90 ya wafanyakazi wote.
101. Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa reli mpya ya kisasa, Serikali katika mwaka 2018/2019 imeendelea na kazi ya kuboresha, kujenga na kukarabati miundombinu ya reli ya kati kwa kuondoa reli zote nyepesi na kuweka reli mpya zenye uzani wa paundi 80 kwa yadi kati ya stesheni ya Dar es Salaam na Isaka. Aidha, kazi ya ukarabati wa reli ya Tanga – Arusha imekamilika kwa sehemu ya Tanga – Same (km 199).
102. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea na kazi ya ujenzi wa reli ya kisasa, ukarabati na ujenzi wa reli ya kati na nyingine ikiwemo ya Tanga – Arusha ili kuimarisha huduma za usafirishaji na biashara kwa ujumla.
Bandari
103. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, kazi ya kuboresha Bandari ya Dar es Salaam kupitia Mradi wa Dar es Salaam Maritime Gateway inaendelea. Lengo la Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa majini na kuiwezesha kushindana na Bandari nyingine katika Ukanda huu. Kazi za kuboresha gati namba moja hadi gati namba namba saba na ujenzi wa gati jipya la kuhudumia meli za magari zimekamilika kwa asilimia 65.
104. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza azma yake ya kumaliza changamoto ya usafiri kwa njia ya maji katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Katika kutekeleza azma hiyo, Septemba 2018 Serikali iliingia mikataba minne na Kampuni ya KTMI ya Jamhuri ya Korea kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya ya kisasa ziwa Victoria; chelezo na ukarabati wa meli za MV Victoria na MV Butiama.
105. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari madogo 200 utafanywa na kampuni ya KTMI kwa kushirikiana na SUMA JKT. Aidha, ujenzi na ukarabati wa meli hizo, utakwenda sambamba na kujenga uwezo kwa wataalamu wetu wa ndani katika tasnia ya ujenzi na ukarabati mkubwa wa meli kwa kushirikiana na kampuni zitakazotekeleza ujenzi huo. Aidha, katika mwaka 2019/2020, Serikali itasimamia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika na ukarabati mkubwa wa meli za MV Liemba, MV Umoja na MV Serengeti.
SEKTA YA MAWASILIANO
Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
106. Mheshimiwa Spika, ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba katika mwaka 2018/2019, Zanzibar imeunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya ujenzi. Huduma kwa wateja zitaanza kupatikana Juni 2019. Matumizi ya huduma za mkongo kwa upande wa Zanzibar yatachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuinua kipato cha wananchi.
107. Mheshimiwa Spika, sambamba na Mkongo wa Taifa, Kituo cha Data cha Taifa kimeendelea kutoa huduma bora kwa taasisi za Serikali na taasisi binafsi hasa katika kuongeza ukusanyaji wa mapato Serikalini. Hadi kufikia Desemba 2018, kituo kimeweza kuunganisha wateja 79 ambapo Taasisi na Idara za Serikali ni 56 na taasisi binafsi 23. Uhamasishaji unaendelea kufanyika kwa kuunganisha Taasisi nyingi zaidi ili kuendelea kukuza usalama na kupunguza gharama za uendeshaji wa miundombinu ya TEHAMA nchini.
108. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine ya kuhakikisha kunakuwepo udhibiti wa kutosha katika mawasiliano, Serikali ilipokea Mfumo wa kusimamia Mawasiliano (TTMS) wenye uwezo wa kubaini takwimu mbalimbali zinazopita katika mitandao ya mawasiliano. Mfumo huo pamoja na mambo mengine utasaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali katika sekta ya mawasiliano kwa kutambua mapato na takwimu za miamala ya fedha mtandao sanjari na kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao kwa kugundua mawasiliano ya ulaghai.
109. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kufikisha huduma hiyo katika Makao Makuu ya Wilaya zote nchini. Aidha, Serikali itaendelea kuhamasisha Taasisi na wateja wengine kuunganishwa na Kituo cha Data cha Taifa.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
110. Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza kwa mafanikio makubwa Mpango wa Elimumsingi bila malipo wenye lengo la kuhakikisha kila mtoto wa Tanzania mwenye umri wa kwenda shule anapata haki ya kupata elimumsingi bila kikwazo cha ada na michango mingine. Aidha, katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali imetumia Shilingi bilioni 711.22 kutekeleza Mpango huo. Katika mwaka 2018/2019 Serikali tayari imetoa Shilingi bilioni 166.44 hadi Februari, 2019 kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo nchini. Utekelezaji wa mpango huo, umeongeza idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika shule za msingi na Sekondari nchini.
111. Mheshimiwa Spika, sambamba na utekelezaji wa elimumsingi bila malipo, Serikali kwa kushirikiana na wananchi na Washirika wa Maendeleo imeboresha miundombinu ya shule za awali na msingi ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa 6,521 kwa shule za msingi na hivyo kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa kutoka 119,647 vilivyokuwepo mwaka 2017 hadi 126,168 Februari 2019, sawa na ongezeko la asilimia 5.5. Kwa upande wa shule za Sekondari, vyumba 2,499 vya madarasa vimejengwa na kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa kutoka 40,720 Mwaka 2018 hadi 43,219 kufikia Februari, 2019. Aidha, madarasa 2,514 yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
112. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha taifa letu linajenga uchumi ulio imara, linajenga jamii inayoheshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu, Serikali pamoja na mambo mengine imeendelea kuwekeza katika elimu ya juu. Serikali imeendelea kuhakikisha watanzania wote wenye sifa wanapata elimu ya juu kwa kupewa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Katika mwaka 2018/2019, Shilingi bilioni 412.4 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu. Hatua hiyo, imeongeza idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo kufikia wanafunzi 119,214 kutoka wanafunzi 98,300 mwaka 2015.
113. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa wigo wa utoaji elimu nchini unapanuka. Hivyo, ili kulinda ubora wa elimu yetu ninazielekeza mamlaka zote zinazohusika na usimamizi na udhibiti wa ubora wa elimu zitekeleze majukumu yao ipasavyo kwa kutoa miongozo na kufanya kaguzi za mara kwa mara.
Maji
Upatikanaji wa Maji Vijijini
114. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 kwa kujenga miradi ya maji sehemu mbalimbali nchini ili kusogeza huduma hiyo karibu zaidi na wananchi. Hadi Februari 2019, jumla ya miradi 65 ya maji vijijini ilikamilishwa ambapo wananchi milioni 25.36 waishio katika vijiji hivyo wamenufaika. Kutokana na kukamilika kwa miradi hiyo, hali ya upatikanaji wa maji vijijini imeongezeka kutoka asilimia 58.7 Julai 2018 na kufikia asilimia 64.8 Februari, 2019. Katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea na ukarabati wa miundombinu ya maji iliyochakaa na kukamilisha miradi mingine 482 iliyopo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwenye Halmashauri nchini.
Upatikanaji wa Maji Mijini
115. Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza miradi ya maji katika Jiji la Dar es Salaam, Miji Mikuu ya Mikoa, Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi katika miji hiyo. Hadi Februari 2019, upatikanaji wa maji safi na salama katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine yanayohudumiwa na DAWASA umefikia asilimia 85.
Katika Miji Mikuu ya Mikoa, upatikanaji wa huduma ya maji imefikia wastani wa asilimia 80. Aidha, katika Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa upatikanaji wa huduma ya maji umefikia wastani wa asilimia 64.
116. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kukamilisha miradi mbalimbali ya maji pamoja na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria mpya ya huduma za maji na usafi wa mazingira.
Afya
Miundombinu ya Huduma za Afya
117. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa uchumi wa viwanda unakwenda pamoja na ujenzi wa taifa lenye watu wenye afya bora wanaoweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi husika. Kwa msingi huo, Serikali inaimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa kujenga, kukarabati na kuvipatia mahitaji muhimu vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Katika kufanikisha azma hiyo, vituo vya kutolea huduma za afya nchini vimeongezeka kutoka vituo 7,678 mwaka 2017 hadi 8,119 mwaka 2018, sawa na ongezeko la vituo 441. Ongezeko hilo limesaidia kusogeza huduma ya afya karibu zaidi na wananchi na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga pamoja na kuboresha afya za wananchi wetu kwa ujumla.
Ujenzi na Ukarabati wa Hospitali
118. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali tano za mikoa ambayo ilikuwa haina Hospitali za Rufaa. Katika miradi hiyo, jumla ya Shilingi bilioni 6.5 zimetolewa kwa Mikoa mipya ya Songwe, Katavi, Njombe, Geita na Simiyu.Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali 67 katika halmashauri mbalimbali ambapo jumla ya Shilingi bilioni 100.5 sawa na Shilingi bilioni 1.5 kwa kila halmashauri zimetolewa.
119. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaboresha zaidi miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa kufanya ukarabati na upanuzi wa miundombinu hiyo, kuendelea na ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa isiyokuwa na hospitali pamoja na kuendelea na ujenzi wa Hospitali za wilaya katika Halmashauri ambazo hazina hospitali hizo.
Upatikanaji wa Dawa na vifaa tiba
120. Mheshimiwa Spika; ujenzi wa vituo vya kutolea huduma ya afya nchini unakwenda sambamba na upatikanaji wa dawa na vifaa na vifaa tiba. Hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya nchini imefikia asilimia 96.7 mwaka 2018/2019.
121. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa, Serikali imefunga Mashine mpya za X-ray 11 katika hospitali za Ruvuma, Morogoro, Simiyu, Magu, Chato, Singida, Nzega, Njombe, Bukoba, Amana na Mpanda. Vilevile, Serikali imekamilisha kuweka mashine ya MRI, CT-SCAN, Digital X-Ray mashine, Moden Utrasound mashine na vifaa vya Wodini vyenye thamani ya shilingi bilioni 12 katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI). Katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa Dawa, vifaa, na vifaa tiba katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya nchini.
Huduma za Afya za Kibingwa
122. Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Benjamin Mkapa. Huduma za kibingwa zinazotolewa ni upandikizaji figo, upasuaji wa moyo, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, upasuaji wa mishipa ya fahamu na ubadilishaji wa nyonga pamoja na upandakizaji wa vifaa vya kusaidia usikivu.
123. Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma hizo za kibingwa ambazo awali zilipatikana nje ya nchi pekee umepunguza gharama za kupeleka wagonjwa wengi nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Kwa mfano, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, kulikuwa na wagonjwa 38 waliokuwa na mahitaji ya kupatiwa matibabu nje ya nchi ikilinganisha na wagonjwa 114 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2017.
124. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaimarisha huduma za kibingwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali za magonjwa Maalum kwa kuendelea na ujenzi wa majengo ya kutolea huduma, kusimika mitambo ya uchunguzi na vifaa tiba.
Ulinzi wa Wanawake na Watoto
125. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa kipindi cha 2017/18 – 2021/2022. Katika mwaka 2018/2019, Serikali imeanzisha Kamati 3,605 za Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika ngazi mbalimbali. Kati ya hizo, Kamati 1,289 zimeanzishwa katika ngazi ya Kata na Kamati 2,313 katika ngazi ya Mtaa/Kijiji. Lengo la kamati hizi ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa wanawake na watoto katika jamii. Aidha, uanzishaji wa Kamati umeongezeka kutoka Kamati 7,383 mwaka 2017/2018 hadi Kamati 10,988 mwaka 2018/2019, sawa na ongezeko la asilimia 48.83. Katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22).
Huduma kwa Wazee
126. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa wazee nchini wanapata matibabu kupitia vitambulisho vinavyowawezesha kupata matibabu bure.
127. Katika mwaka 2018/2019 wazee 247,771 wamepatiwa kadi za matibabu bure. Juhudi hii imewezesha wazee waliopata vitambulisho vya matibabu bure kuongezeka kutoka wazee 213,025 mwaka 2015/2016 hadi kufikia wazee 1,042,329 mwaka 2018/2019, sawa na ongezeko la wazee 829,304. Serikali itaendelea kuwatambua wazee na kuhakikisha inawapatia vitambulisho vya matibabu bure wazee wote nchini.
Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu
128. Mheshimiwa Spika, mwaka 2018/2019, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa Sera, Sheria na Mikataba inayohusu haki na huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010. Sheria hiyo, pamoja na masuala mengine, inamtaka kila mwajiri mwenye waajiriwa kuanzia 20 kuwa na watumishi wenye ulemavu wasiopungua asilimia 3.
129. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea kutoa chakula, matibabu, malazi, ushauri nasaha na mafunzo ya stadi za kazi kwa wanafunzi wenye ulemavu katika vyuo vya Singida na Yombo – Dar es Salaam. Vilevile, Serikali imewezesha upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kuzifikia huduma mbalimbali bila vikwazo. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na viti mwendo, fimbo nyeupe, magongo ya kutembelea, viti maalum vya kuogea, miwani maalum, kofia pana, vifaa vya kukuzia maandishi, mafuta kinga kwa ajili ya Watu wenye Ualbino na mashine za kuchapia maandishi ya nukta nundu kwa Wasioona.
130. Mheshimiwa Spika, Serikali imeratibu maadhimisho ya siku za watu wenye ulemavu ili kuondoa unyanyapaa miongoni mwa jamii ikiwa ni pamoja na; siku ya Fimbo nyeupe, Siku ya Viziwi na Siku ya watoto wenye ulemavu. Katika maadhimisho hayo, elimu ya kutowanyanyapaa watu wenye ulemavu ilitolewa. Aidha, Serikali imeendelea kuratibu uundwaji wa Kamati za Watu wenye Ulemavu ambapo Kamati 26 zimeundwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara, ngazi ya Halmashauri Kamati 140, ngazi ya Vijiji Kamati 5,024 na ngazi ya Mitaa Kamati 2,284.
131. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utoaji huduma kwa watu wenye ulemavu, Serikali imekamilisha uundaji wa Baraza jipya la Ushauri la Taifa kwa Watu wenye Ulemavu baada ya lililopita kumaliza muda wake. Ni matajio ya Serikali kwamba Baraza hilo litaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuishauri Serikali kuhusu huduma kwa watu wenye ulemavu hususan masuala ya afya, ajira, elimu na miundombinu pamoja na kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu.
132. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itafanya mapitio ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na.9 ya mwaka 2010 ili iweze kwenda na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, kukusanya maoni na mapendekezo ya uendeshwaji wa Mfuko wa Taifa kwa Watu Wenye Ulemavu pamoja na kuratibu uendeshaji wa shughuli za Baraza la Ushauri la Taifa kwa Watu wenye Ulemavu.
ULINZI NA USALAMA
133. Mheshimiwa Spika, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kubwa katika kuhakikisha hali ya amani, usalama na utulivu nchini inaimarika. Katika mwaka 2018/2019, Serikali imelitumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania kusaidia mamlaka za kiraia katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali kama vile uokoaji wa watu na mali zao pamoja na ujenzi wa mji wa Serikali katika eneo la Mtumba, Dodoma.
134. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kushiriki kwenye misheni za kulinda amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Misheni hizo ni MINUSCA huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR); MONUSCO Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC); UNAMID nchini Sudan; UNFIL nchini Lebanon; UNISFA huko Abyei na UNMISS nchini Sudan Kusini.
135. Mheshimiwa Spika, ushiriki wa Jeshi letu pamoja na vyombo vingine vya usalama katika misheni hizo za amani, umeendelea kuvipatia uzoefu, kuongeza maarifa na mbinu mbalimbali za kijeshi na kiintelijensia. Aidha, vyombo vyetu vimeendelea kujifunza matumizi ya vifaa vya kisasa na kuanzisha au kuimarisha mahusiano ya kijeshi na nchi nyingine zinazoshiriki kwenye misheni hizo.
136. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Serikali imeendelea kudhibiti hali ya ulinzi na usalama nchini kwa kuboresha mazingira ya kuishi askari na kufanyia kazi;
kutoa huduma bora za kubaini, kutanzua na kudhibiti uhalifu; kudhibiti vitendo vya rushwa ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kupambana na uhalifu nchini. Hali hii imechangia kupunguza makosa ya kiuhalifu kutoka makosa 37,602 mwaka 2017 hadi kufikia makosa 36,228 mwaka 2018.
137. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uhamiaji Serikali inatekeleza kwa mafanikio makubwa awamu ya pili ya Mradi wa Uhamiaji Mtandao, ambayo inahusisha utoaji wa huduma ya Viza pamoja na Vibali vya Ukaazi vya Kielektroniki. Aidha, tarehe 26 Novemba 2018, nilizindua mfumo huo ambao sasa unamuwezesha mteja kufanya maombi yake kwa njia ya mtandao. Mfumo huo, utarahisisha utoaji wa huduma bora za uhamiaji, kuimarisha ulinzi na usalama, kuongeza udhibiti wa wageni wanaoingia nchini, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta ya uwekezaji.
138. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama, kuendelea kutoa fursa za mafunzo kwa vyombo vya ulinzi na usalama, kuvipatia vifaa na zana za kisasa na kuendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na makosa yanayovuka mipaka.
KAZI, AJIRA NA VIJANA
Maendeleo ya Vijana
139. Mheshimiwa Spika, nguvukazi ya vijana ni mhimili muhimu katika kuwezesha nchi yetu kufikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025. Katika 2018/2019, Serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Vijana imewezesha vikundi vya vijana 755 ambavyo vimepatiwa mikopo ya Shilingi Bilioni 4.2 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Aidha, imeibua bunifu 31 za Vijana katika sekta ya sayansi na teknolojia. Kati ya hizo, bunifu 11 zimefanyiwa tathmini ya kisayansi na kwa sasa ziko katika hatua mbalimbali ikiwemo kuwekwa kwenye kiota atamizi (Incubator) kabla ya hatua ya majaribio na uzalishaji.
140. Mheshimiwa Spika, bunifu nyingi zimefanyika nchini kama vile: kifaa cha kupimia matatizo ya moyo; kiti maalum cha kuhudumia watoto wenye usonji; mfumo wa kuwasha na kuzima taa za nje za ndege kwa kutumia simu ya mkononi; mguu wa ndege kwa ajili ya matumizi ya kufundishia vyuoni; na gari linalotumia mfumo wa umeme. Katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kimitaji kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mapato ya ndani ya Halmashauri na Programu ya kukuza ujuzi.
Ukuzaji Ujuzi
141. Mheshimiwa Spika, ushiriki wa nguvukazi ya taifa hususan vijana ni muhimu katika kufikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati inayoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Hivyo basi, Serikali inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayolenga kuwapatia vijana ujuzi stahiki ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa kujiajiri au kuajiriwa.
142. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, jumla ya vijana 32,563 wamewezeshwa kupata mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa. Hii inahusisha vijana 18,800 waliopata mafunzo ya ujuzi wa kilimo kwa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba pamoja na vijana 2,720 waliopatiwa mafunzo ya ufundi wa fani mbalimbali pamoja vijana 10,443 waliopatiwa mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi kwa fani za ufundi wa magari, useremala, uashi, upishi, huduma za vyakula na vinywaji, ufundi umeme, uchomeleaji, ufundi bomba, uchongaji vipuri na ushonaji nguo.
143. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuwezesha vijana kupata mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri, kuajiriwa na stadi za kazi kwa vijana 46,950 katika fani mbalimbali. Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza vijana kuchangamkia fursa za mafunzo haya kwa kuwa ni nyenzo muhimu kuwawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
Fursa za Ajira
144. Mheshimiwa Spika, utengenezaji wa fursa za ajira umeendelea kuwa agenda ya kipaumbele ya Serikali ya Awamu ya Tano. Suala hilo, limezingatiwa katika sera, mipango na programu zote za maendeleo ya kitaifa na kisekta. Hadi kufikia Februari 2019, jumla ya ajira 221,807 zimezalishwa nchini. Kati ya ajira hizo, ajira 146,414 sawa na asilimia 66 zimetokana na utekelezaji wa miradi ya umma ya ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi kama vile ujenzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, umeme, ujenzi wa Mji wa Serikali Jijini Dodoma, uimarishaji wa Shirika la Ndege Tanzania pamoja na ajira za moja kwa moja katika Utumishi wa Umma. Aidha, ajira 75,393 ambazo ni asilimia 34 ya ajira zilizozalishwa zimetokana na uwekezaji katika sekta binafsi.
145. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hususan Waajiri na Wafanyakazi, Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo pamoja na Vyama vya Kiraia itaendelea kutekeleza programu zinazowezesha kuibua fursa zaidi za ajira.
Masuala ya Kazi na Wafanyakazi
146. Mheshimiwa Spika, utulivu na amani mahali pa kazi ni nguzo muhimu kuwezesha uzalishaji na tija katika maeneo mbalimbali ikiwemo viwandani na hivyo kukuza uchumi wa nchi yetu. Kwa kutambua ukweli huu, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi ili kuwezesha mazingira yanayopelekea kazi za staha pamoja na uwepo wa amani na utulivu mahali pa kazi.
Katika mwaka 2018/2019, jumla ya kaguzi 2,516 zimefanyika zikihusisha kaguzi za kawaida 2007, kaguzi maalum 382 na kaguzi za ufuatiliaji 127. Vilevile, jumla ya Amri Tekelezi 455 zilitolewa kwa waajiri na waajiri 16 walifikishwa Mahakamani kwa kukiuka Sheria za Kazi. Jumla ya shilingi milioni 285 zilitozwa kama adhabu kwa waajiri waliopatikana na hatia. Aidha, jumla ya Waajiri 414 na Wafanyakazi 2,572 walielimishwa kuhusu Sheria za Kazi.
147. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi kwa kusimamia uundwaji wa Mabaraza ya wafanyakazi mahala pa kazi. Katika mwaka 2018/2019, Mabaraza 116 yameundwa na Mabaraza 110 yamepewa elimu kuhusu wajibu na majukumu yao na ushirikishwaji wa wafanyakazi mahala pa kazi. Aidha, katika kuimarisha mahusiano mema miongoni mwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi, vikao 9 vya maridhiano vilifanyika kwa lengo la kusuluhisha migogoro ya kivyama na viongozi.
148. Mheshimiwa Spika, Serikali pia, inasimamia na kuratibu ajira za wageni nchini kwa kutumia Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Namba.1 ya mwaka 2015. Katika mwaka 2018/2019, jumla ya vibali vya kazi 8,703 vilitolewa, jumla ya maombi 974 yalikataliwa na maombi 1,701 yalipewa msamaha. Aidha, katika kusimamia na kuratibu Huduma za Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini, jumla ya maombi 20 ya wakala yamepatiwa usajili na maombi matatu yamekataliwa.
149. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa Sheria za kazi ili kuwezesha utulivu mahala pa kazi na hivyo kuchochea uwekezaji na ukuzaji wa uchumi. Hii itahusisha kufanya kaguzi za kazi, kufanya mapitio na marekebisho ya Sheria za Kazi na kufanya utambuzi wa wadau wanaotekeleza shughuli za kukomesha utumikishwaji wa mtoto.
Hifadhi ya Jamii
150. Mheshimiwa Spika, Serikali inaboresha Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Katika mwaka 2018/2019, Serikali imeanza utekelezaji wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma Na.2 ya Mwaka 2018 kwa kuunganisha Mifuko ya LAPF, GEPF, PSPF na PPF na kuanzisha mfuko mmoja wa PSSSF. Kutokana na maboresho hayo, Serikali imelipa madeni yote ya wastaafu wa PSPF wa mwaka 2017/2018 wapatao 9,971 yenye thamani ya Shilingi bilioni 888.39. Hatua hii ni kubwa kwa kuwa imeweza kutatua kero za wastaafu ambazo zilidumu kwa muda mrefu.
151. Mheshimiwa Spika, tarehe 29 Desemba 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikutana na viongozi wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania ambapo alielekeza kila Mfuko wa Pensheni uendelee kutumia kikotoo chake cha zamani katika kipindi cha mpito cha miaka mitano ijayo. Katika kutekeleza maagizo hayo, PSSSF kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi imeandaa Mpango Kazi wa namna ya kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais katika kipindi cha mpito (2019 – 2023) ikiwa ni pamoja na kufanya uhakiki wa jumla ya wastaafu 81,525 wa mfuko huo.
152. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais kwa kushirikiana na Shirikisho la Wafanyakazi ili kuwezesha kupata kanuni ambazo zitakidhi matarajio ya wafanyakazi wa Sekta ya Umma na Binafsi na kuhakikisha mifuko inakuwa endelevu.
MASUALA MTAMBUKA
Vita Dhidi ya Rushwa
153. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inaendelea kutekeleza majukumu yake ya mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuelimisha umma kuhusu athari za rushwa, kuchunguza tuhuma za makosa ya rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya vyombo vya sheria. Aidha, Serikali imeendelea kujenga uelewa kwenye Taasisi za Umma na kuweka mfumo thabiti wa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa Awamu ya Tatu (NACSAP III) ili kupata matokeo yaliyo bora zaidi katika vita dhidi ya Rushwa nchini.
154. Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji mzuri wa Mkakati huo na juhudi zinazofanywa na TAKUKURU na wadau wengine nchini, tatizo la rushwa limepungua. Katika upimaji wa hali ya rushwa uliofanywa na mashirika ya kimataifa yameonesha Tanzania kufanya vizuri miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki. Kwa mfano, ripoti ya taasisi ya Transparency International ya mwaka 2018, Tanzania imeshika nafasi ya pili baada ya Rwanda kwenye mapambano dhidi ya rushwa.
155. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa Awamu ya Tatu (NACSAP III) katika Sekta zote kwa mfumo jumuishi na msisitizo ukiwekwa kwenye mfumo wa mrejesho kwa wadau kama nguzo muhimu ya tathmini ya utekelezaji wa Mkakati huu. TAKUKURU pia, itaendelea kukamilisha uchunguzi wa majalada ya tuhuma za rushwa unaoendelea na tuhuma mpya zitakazojitokeza pamoja na kuendesha mashauri yanayoendelea mahakamani na mashauri mapya yatakayofunguliwa Mahakamani. Aidha, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 itahuishwa.
Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya
156. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mapambano dhidi ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya. Aidha, Serikali imeendelea kubaini mtandao wa waingizaji wa dawa hizo hapa nchini na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahalifu hao. Kutokana na juhudi hizo, Septemba 2018, nchi yetu ilipata heshima kubwa ya kuandaa Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa Vyombo Vinavyopambana na Dawa za Kulevya Afrika (HONLEA AFRICA) uliofanyika Jijini Dar es Salaam. Kupitia mkutano huo, vyombo vyetu vya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya viliweza kubadilishana mbinu, uzoefu, kupeana mikakati ya kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya pamoja na kubadilishana taarifa kuhusu kadhia hiyo.
157. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Januari 2019, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola imefanikiwa kukamata watuhumiwa 11,617 wakiwa na dawa za kulevya za aina mbalimbali kama vile heroin, cocaine, bangi na mirungi. Aidha, ekari zaidi ya 59 za mashamba ya bangi ziliteketezwa nchini katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Dodoma na Mara.
158. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa waraibu wa dawa za kulevya, Serikali imeendelea kutoa huduma kwa kutumia dawa ya Methadone katika mkoa wa Dar es Salaam na vituo vipya katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya. Aidha, kufikia Januari 2019, watumiaji wapatao 6,500 wanapata huduma za tiba ya methadone katika vituo vilivyopo nchini. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa waraibu wanaopatiwa matibabu hawarejei tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
159. Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha azma hiyo, Serikali imetenga shilingi billion mbili kwa ajili ya ukuzaji ujuzi kwa vijana. Mpango huo utawahusisha vijana ikiwa ni pamoja na wale walioachana na matumizi ya dawa za kulevya. Vijana hawa watapelekwa viwandani na sehemu mbalimbali za kazi kwa lengo la kukuza ujuzi wao na baadaye kupatiwa fursa za ajira.
160. Mheshimiwa Spika, dawa za kulevya zina athari kubwa kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla. Hivyo, napenda kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano haya kwa kutoa taarifa kuhusu watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini. Aidha, rai yangu kwa waraibu ambao wamepatiwa ujuzi kujiunga kwenye vikundi vidogo vidogo ili waweze kupatiwa mikopo na hivyo kujiajiri katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Mapambano Dhidi ya UKIMWI
161. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 - 2022/2023 ambao unalenga kuzuia maambukizi mapya na vifo vitokanavyo na UKIMWI nchini. Tathmini ya utekelezaji wa Mkakati wa Tatu wa Taifa uliomaliza muda wake Juni 2018 umeonesha kwamba; vifo na maambukizi mapya ya UKIMWI yamepungua. Kutokana na tathmini hiyo, ulifanyika utafiti (Tanzania HIV Impact Survey) mwaka 2016/2017 katika ngazi ya kaya ambao umeonesha kwamba kiwango cha Maambukizi ya VVU kwa Tanzania Bara kimeshuka kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 4.8 mwaka 2016/2017.
162. Mheshimiwa Spika, bado tuna changamoto ya watanzania wengi kutojua afya zao na idadi kubwa ya WAVIU kutokuwa kwenye mpango wa matunzo na matibabu. Pamoja na dawa za ARV kutolewa bure, inakadiriwa kuwa kuna takriban WAVIU 500,000 ambao hawapati dawa hizo.
Nitoe rai kwa wadau wote nchini kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha watu kupima na kujua hali zao za maambukizi ya VVU. Aidha, kwa wale watakaokutwa na maambukizi waingizwe kwenye mpango wa matibabu mapema iwezekanavyo na WAVIU wanaotumia dawa za kufubaza waendelee kutumia dawa hizo pasipo kuacha.
163. Mheshimiwa Spika, Serikali na Wadau mbalimbali wakiwemo wa ndani na nje wameendelea kuchangia Mfuko maalum wa Kupambana na Kudhibiti UKIMWI nchini (AIDS TRUST FUND) ili kuondokana na utegemezi wa wafadhili. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2018 Mfuko uliweza kukusanya Shilingi milioni 864. Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 750 zimetolewa na Serikali na Shilingi milioni 114 zimekusanywa kutoka kwa wadau kupitia matembezi ya hiari na harambee. Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika bajeti yake kwa kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa UKIMWI kila mwaka.
164. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI ili kufikia lengo la TISINI TATU ifikapo mwaka 2020. Lengo la Mkakati huo ni kwamba hadi kufikia mwaka 2020, asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamejua hali zao za maambukizi; asilimia 90 ya waliopima VVU na kugundulika kuwa na maambukizi wapatiwe dawa za kufubaza (ARV) na asilimia 90 ya watu wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU.
Uratibu wa Maafa
165. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na jumuiya za kikanda za EAC, SADC, Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) na Mashirika yake katika masuala ya usimamizi wa maafa kwa kufanya mafunzo ya vitendo na mazoezi ya pamoja ya kukabiliana na maafa. Vilevile, Serikali imetoa elimu kuhusu usimamizi wa maafa kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchini.
166. Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu jirani zetu wa Msumbuji, Malawi na Zimbabwe walipata maafa yaliyosababishwa na kimbunga kikali kiitwacho Idai. Maafa hayo yalisababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa miundombinu na mazingira na watu wengi kukosa makazi katika nchi hizo. Kutokana na athari hizo, Serikali ilitoa msaada wa dharura wa kibinadamu wa tani 214 za chakula, tani 24 za madawa mbalimbali na vifaa vya kujihifadhi. Tumuombe Mwenyezi Mungu awajalie afya njema wale wote waliopata majeraha na azipumzishe mahala pema roho za marehemu. Amina!
167. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za kuimarisha mifumo ya kufuatilia mienendo ya majanga na utoaji wa tahadhari ya awali ili kujenga jamii iliyo salama na stahimilivu. Aidha, Serikali itahakikisha kuwa mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali inazingatia vihatarishi vya maafa na hivyo, kuipunguzia gharama kubwa za kukabili na kurejesha hali baada ya madhara kutokea.
MASUALA YA MUUNGANO
168. Mheshimiwa Spika, Muungano wetu ni matokeo ya mahusiano ya kihistoria ya pande zote mbili, hivyo, hatunabudi kuuheshimu na kuulinda ili uendelee kudumu kwa faida ya watu wetu.
Katika kuimarisha Muungano wetu, Serikali zote mbili zimeendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoukabili.
169. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika tarehe 21 Januari, 2019 kiliridhia utozwaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia sifuri (0%) kwenye umeme unaouzwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kufuta malimbikizo ya deni la kodi ya VAT lililofikia Shilingi Bilioni 22.9 kwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwenye umeme uliouzwa na TANESCO.
170. Mheshimiwa Spika, kutokana na mafanikio haya yanayoendelea kupatikana katika utatuzi wa kero za Muungano, naomba nirudie kutoa wito wangu kwa Watanzania kuendelea kudumisha muungano wetu ambao ni tunu na mfano wa kuigwa barani Afrika na dunia nzima.
UHUSIANO WA KIMATAIFA
171. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kuimarisha na kuendeleza mahusiano mema baina yake na Mataifa mengine na pia Mashirika ya Kikanda na Kimataifa duniani. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa kutokana na jitihada hizo, Tanzania imeendelea kuwa nchi rafiki kwa mataifa yote duniani. Aidha, Serikali imeshiriki katika mikutano na majukwaa muhimu ya kikanda na kimataifa na kutetea maslahi ya Nchi ikiwemo kutoa ufafanuzi pale ambapo baadhi ya watu wa ndani na nje wenye nia mbaya walipojaribu kupotosha ukweli na kuchafua taswira ya Taifa letu.
172. Mheshimiwa Spika, Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika mwezi Agosti 2018, nchini Namibia ulimteua Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake na kwa kuendelea kutekeleza kwa ukamilifu wajibu na heshima hiyo aliyopewa na Wakuu wenzake wa Nchi na Serikali.
173. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taratibu za SADC Makamu wa Mwenyekiti ndiye anayekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa mwaka unaofuata. Hivyo, mwezi Agosti mwaka huu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuchukua nafasi ya Uenyekiti wa SADC katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika Jijini Dar es Salaam. Napenda kutumia fursa hii kuwasihi wale wote wanaohusika na maandalizi ya mkutano huu mkubwa na muhimu kutekeleza jukumu hilo kwa bidii, weledi na ufanisi wa hali ya juu.
174. Mheshimiwa Spika, Mkutano huu utawaleta Nchini Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri, Maofisa Waandamizi, wawakilishi wa jumuiya za wafanyabiashara, waandishi wa habari na wengineo kutoka Nchi 15 Wanachama SADC. Hii ni fursa muhimu siyo tu kwa Serikali bali pia kwa sekta binafsi nchini kujiandaa kuwapokea wageni hawa kwa malazi, usafiri, chakula na utalii. Nitoe wito, kwa watanzania kujipanga vyema na kuchangamkia fursa zitakazoambatana na ujio wa mkutano huo.
175. Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu, Sera ya mambo ya nje ni mtambuka na ni mwendelezo wa sera ya ndani ya nchi katika nyanja na maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.
Kwa kuzingatia muktadha huo, nitumie fursa hii kuwasisitiza mabalozi wetu nje kuendelea kutafuta mitaji ya uwekezaji hususan katika miradi ya vipaumbele, masoko mapya ya bidhaa zetu, kutangaza fursa za utalii na kutafuta fursa za mafunzo.
176. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itahakikisha utekelezaji wa diplomasia ya kiuchumi unaendelea kupewa kipaumbele cha kutosha ikiwa ni pamoja na kukamilisha Sera ya Taifa ya Diaspora; kuendelea kushiriki kwenye utengamano wa kikanda; kuimarisha ujirani mwema na mahusiano na taasisi za kimataifa; kupigania mfumo wa haki wa utawala, siasa na uchumi na kuunga mkono juhudi za kulinda amani na utulivu duniani kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi yetu.

MICHEZO
177. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba imepita takriban miaka 39 tangu nchi yetu ishiriki kwa mara ya mwisho michuano ya mpira wa miguu kwa Nchi za Bara la Afrika maarufu AFCON. Hata hivyo, kusubiri huko kulikoma tarehe 24 Machi 2019 baada ya vijana wetu wa Taifa Stars kupata ushindi mnono wa mabao matatu bila majibu dhidi ya jirani zetu wa Uganda. Ushindi huo, unaipeleka Taifa Stars katika AFCON 2019 huko nchini Misri.
178. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza wachezaji, viongozi, benchi la ufundi, kamati za uhamasishaji wa ushindi, mashabiki na watanzania wote kwa kutimiza ndoto yetu ya muda mrefu ya kushiriki michuano hiyo mikubwa kabisa Barani Afrika. Aidha, nitoe wito kwa viongozi, wachezaji na walimu kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo iliyotangulia ili kujiweka sawa na michuano ya mwezi Juni 2019. Napenda mtambue kwamba lengo letu ni kwenda kushindana na si kushiriki. Niwatakie maandalizi mema na mafanikio katika michuano hiyo inayokuja.
179. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine nchi yetu inaendelea vyema na maandalizi ya mashindano ya mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 barani Afrika (AFCON – U17) yatakayoanza Aprili 2019. Katika mazungumzo niliyofanya na viongozi wa Serikali na vyama mbalimbali vya michezo nchini vikiongozwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) wamenihakikishia kwamba maandalizi ni mazuri na timu yetu itafanya vizuri.
180. Mheshimiwa Spika, iwapo Serengeti Boys itaibuka na ushindi walau katika michezo yake miwili tu itakuwa imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia huko nchini Brazil kwa vijana wa umri huo. Hii inatokana na ukweli kwamba kila kundi litatoa timu mbili ambazo zitaliwakilisha Bara la Afrika kwenye mashindano hayo ya dunia.
181. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuipongeza timu yetu ya Vijana wenye ulemavu wa akili kwa kuibuka na ushindi wa medali 15 katika Michezo Maalumu ya Olimpiki iliyohusisha riadha na mpira wa wavu huko Abudhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu Machi 2019. Mafanikio hayo ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyowahi kupatikana katika nchi yetu kwenye tasnia ya michezo. Aidha, niipongeze pia timu yetu ya mpira wa miguu kwa wanawake (Twiga Stars) kwa kuibuka mabingwa wa CECAFA mwaka 2018 pamoja na kuwa washindi wa kwanza wa mashindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Bujumbura, Burundi Julai 2018. Vilevile, nawatakia maandalizi mema na ushindi Twiga Stars katika mchuano wao wa tarehe 5 Aprili 2019 dhidi ya Timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikiwa ni hatua ya awali ya kuwania kufuzu kwa ajili ya michuano ya Olimpiki mwaka 2020 huko Tokyo, Japan.
182. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwahamisisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kesho katika uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuishangilia timu yetu ili ishinde kwa mabao mengi na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga katika hatua inayofuata. Viingilio vya mchezo huo vimepunguzwa mno. Kwa mfano wanawake ni Shilingi 500 tu na wanaume ni Shilingi 1,000. Lengo ni kutoa fursa kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yetu.Kwa upande wa riadha, timu yetu hivi sasa inashiriki michezoo ya riadha Nchini Rwanda. Ni matarajio yetu kwamba timu hiyo ya riadha itarejea nyumbani na medali za kutosha. Tunawatakia ushiriki mwema na mafanikio katika mashindano hayo.
183. Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kumpongeza mwanamasumbwi wa kitanzania Hassan Mwakinyo kwa kuendelea kuwa mfano bora kwenye tasnia hiyo ya masumbwi. Tarehe 23 Machi 2019 Mwakinyo aliendelea kung’ara katika anga za masumbwi na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya kumtwanga mpinzani wake Muargentina Sergio Gonzalez, huko Nairobi. Nitoe wito kwa vyama vya michezo kuendelea kuwalea vema wanamichezo hususan vijana ili waweze kuipaisha vema bendera ya Tanzania kwenye medani mbalimbali za michezo ndani na nje. Huu ni wakati wakila Mtanzania kuthamini michezo na kutambua kuwa michezo ni ajira na michezo inalipa.
184. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu vilabu vyetu vya mpira wa mguu vimekuwa havifanyi vizuri katika medani ya michuano ya Klabu Barani Afrika. Hata hivyo, katika msimu wa 2018/2019 Klabu ya Simba ya Dar es Salaam imeweza kututoa kimasomaso baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika. Kufanya vizuri kwa Klabu ya Simba kunaongeza uwezekano wa Tanzania kupatiwa nafasi nyingine mbili na kufanya jumla ya vilabu vinne vitakavyoshiriki mashindano hayo makubwa ya vilabu Barani Afrika katika misimu ijayo. Vilevile, ushindi wa Taifa Stars na Simba una manufaa makubwa kwa nchi yetu yakiwemo kuitangaza vyema nchi na kufungua fursa za ajira kwa vijana wetu hususan wanaojihusisha na soka.
185. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki wote wa Klabu ya Simba kwa mafanikio hayo makubwa. Tupo pamoja nanyi. Vilevile, niwatakie kheri, maandalizi mema na ushindi timu zetu zote ikiwemo Serengeti Boys katika mashindano ya AFCON - U17, Taifa Stars katika mashindano ya AFCON huko Misri Juni 2019 na Klabu ya Simba katika hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Barani Afrika.
HITIMISHO
186. Mheshimiwa Spika, wakati nikielekea kuhitimisha hotuba yangu hii, nitoe wito kwa Viongozi, Watendaji na watanzania wote kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Nirejee tena kuwakumbusha kwamba dhamira ya kufikia uchumi wa kati itafikiwa tu iwapo watanzania tutaweka mbele uzalendo na maslahi mapana ya taifa letu pamoja na kudumisha misingi ya umoja wa kitaifa.
187. Mheshimiwa Spika, lengo la uchumi wa viwanda ni kuharakisha ukuaji wa uchumi jumuishi wenye kupunguza umaskini, kuongeza uzalishaji, ajira na ustawi wa watu wetu. Lengo hilo litafikiwa kwa kufungamanisha sekta ya viwanda na sekta nyingine za uchumi ikiwemo biashara, kilimo na utalii.
188. Mheshimiwa Spika, kwa upande wake Serikali itaendelea kuonesha uthubutu na dhamira ya dhati katika kuhakikisha inatekeleza yafuatayo:
Mosi: kuendelea kupambana na rushwa, ufisadi, uzembe na uvivu sambamba na kuimarisha nidhamu kwa viongozi na watendaji wa ngazi zote katika kuwahudumia wananchi;
Pili: kusisitiza kwa viongozi, watendaji na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, ubunifu na uzalendo katika kujiletea maendeleo;
Tatu: wafanyabiashara na wajasiriamali kuendesha biashara zao kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyopo pamoja na kujenga tabia ya kuona fahari kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa letu;
Nne: kuielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujenga mahusiano rafiki na walipa kodi kwa lengo la kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa walipa kodi kuwa Taasisi hiyo inatumia nguvu na vitisho kudai kodi na kwa sababu hiyo kuzorotesha ukusanyaji wa mapato;
Tano: kuendelea kujenga mazingira mazuri na wezeshi ya kufanya kazi, biashara, kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi; na
Sita: kuwahimiza wananchi kutumia ipasavyo haki yao ya kidemokrasia kwa kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa Oktoba 2019. Aidha, Serikali itahakikisha Mamlaka zinazosimamia uchaguzi huo, zinashirikiana vyema na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha unaendeshwa kwa amani na usalama.
189. Mheshimiwa Spika, ni vema tukatambua kuwa tupo kwenye zama za ushindani wa kiuchumi. Kwa msingi huo, mafanikio yetu katika zama hizi yatategemea pia ubunifu, tija na uwepo wa ufanisi kwenye miundombinu wezeshi ya kiuchumi inayoendelea kujengwa na Serikali. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuhakikisha inasimamia ipasavyo rasilimali za taifa ili zielekezwe katika sekta ambazo zitatuwezesha kufikia malengo tuliyojiwekea pamoja na kuhimili ushindani wa kiuchumi uliopo.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2019/2020
190. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2019/2020, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe Shilingi Bilioni Mia Moja Arobaini na Nane, Milioni Mia Nane Themanini na Sita, Mia Tano Ishirini na Tatu Elfu na Mia Tano Themanini na Moja (148,886,523,581.00). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Themanini na Sita, Milioni Mia Mbili Tisini, Mia Tatu Hamsini na Tano Elfu (86,290,355,000.00) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Sitini na Mbili, Milioni Mia Tano Tisini na Sita, Mia Moja Sitini na Nane Elfu na Mia Tano Themanini na Moja (62,596,168,581.00) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
191. Mheshimiwa Spika, naliomba pia, Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Nne, Milioni Mia Moja Themanini na Mbili, Mia Tano Thelathini na Saba Elfu na Mia Sita (124,182,537,600.00) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Sita, Milioni Mia Tano Sabini na Tatu na Ishirini na Sita Elfu (116,573,026,000.00) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Saba, Milioni Mia Sita na Tisa, Mia Tano Kumi na Moja Elfu na Mia Sita (7,609,511,600.00) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.