Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI WATOA UFAFANUZI AJALI YA MAGARI MAWILI YALIOUA WATU 2


Jeshi la Polisi mkoani Arusha limetoa ufafanuzi wa utata wa tukio la ajali iliyotokea juzi na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi saba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa,Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Jonathan Shanna alisema kuwa, waliofariki ni wawili na sio nane kama ambavyo ilisambaa juzi kwenye mitandao.

Aliongeza kuwa, ajali hiyo haikutokana na mashindano ya magari kama ilivyoelezwa awali bali wahusika walikuwa wakisherehekea sikukuu ya Pasaka kwa kuendesha magari kwa kushindana.

Pia aliongeza kuwa, huwa ni kawaida yao kufanya hivyo wakati wa sikukuu yoyote wakijumuisha marafiki wa upande wa Kenya na Tanzania.

Aliwataja marehemu wa ajali hiyo kuwa ni Onesmo Mwangi raia wa Kenya na Peter Donard mkazi wa Arusha,ambapo miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya Selian.

Alisema, majeruhi wa tukio hilo ni saba ambao ni Robin Allan
raia wa Kenya, Rajab Mhesa (31) mkazi wa Arusha,Robbin Kurya, raia wa Kenya,Anord Twahil na Shedracka Anord (13) ambaye ni mwanafunzi.

"Wengine ni Bisco Mshanga (29) mkazi wa Arusha na Stella Musoni raia wa Kenya," aliongeza Kamanda Shanna.

Aidha, alifafanua kuwa ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 9, alasiri eneo la Oldonyosambu katika Barabara ya Arusha Namanga ikiyahusisha magari mawili yaliyokuwa yameongozana, Toyota Saloon na Mitsubishi Saloon huku chanzo cha ajali ni kutokana na dereva wa mbele kukata kona ghafla huku dereva wa nyuma akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari.

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amewaomba wananchi kutoa taarifa kwa serikali pindi kunapotokea kusanyiko lolote hasa pembezoni mwa barabara kuu za Arusha-Moshi na Arusha Nairobi.

Aliyasema hayo jana katika Hospitali ya Selian iliyopo Ngaramtoni jijini Arusha alipokwenda kuwajulia hali majeruhi wanne wa ajali iliyotokea katika mashindano hayo ambao wamelazwa katika hospitali hiyo.

Alieleza kuwa, Serikali kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama itasaidia kufanya maandalizi ya kiusalama kwa ajili shughuli mbalimbali walizoziandaa kuliko kuandaa mikusanyiko hiyo kwa mazoea kama wanavyofanya kwa miaka mingine.

"Tuwaombe msitumie utamaduni wa kawaida nchi ya Tanzania haiongozwi kwa utamaduni wa kawaida, kwamba kila mwaka tunafanya matukio kama haya, hivyo 'its ok' kwa kuwa 'its a weekend'.

"Tunachohitaji ni kulinda watu watu na wakusanyike katika hali ya kiusalama zaidi, kwa kuwatengenezea mazingira mazuri kupitia jeshi letu la polisi Kitengo cha Usalama Barabarani watu wa intelijensia na wengine,"alisema DC Muro.

Aidha, aliwataka watanzania kuziacha mamlaka husika zinazotakiwa kutoa taarifa sahihijuu ya jambo lolote ikiwemo tukio la ajali hiyo kwa kusema taarifa yake imeelezwa sivyo kwenye mitandao ya kijamii.

"Nakanusha habari zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa wamefariki watu nane raia wa nchi jirani,habari hizi si za kweli tumepokea miili ya marehemu miwili tu na majeruhi wanne na jitihada za kunusuru maisha yao zinaendelea kufanyika na uzuri baadhi ya ndugu zao wameshafika toka nchi jirani hata na wa hapa Tanzania,"aliongeza DC Muro.

Kwa upande wake Daktari wa hospitali hiyo, Petro Mbuya alisema walipokea maiti mbili ambazo zimehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo pamoja na majeruhi wanne ambapo wawili kati yao wameumia vichwa. 

Mmoja uti wa mgongo huku mgonjwa mwingine walimpa rufaa ya kwenda kuonana na daktari bingwa wa mfumo wa fahamu katika Hospitali ya Mkoa ya Mt.Meru huku akiwataja majeruhi hao kuwa ni Anord Twahili ,Clara,Stela Musoni (21) raia wa Kenya na Bosco Mshanga (29).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com