Mjumbe wa Kamati ya watumiaji wa Maji Domu, Alexanda Mwakalasye akitoa maelekezo kwa wanahabari jinsi pampu ya dawa inavyofanyakazi wakati wa ziara ya Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja kujionea miradi ya jamii inavyotoa huduma iliyopo pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam. Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja akipata maelezo kwa Meneja Uhusiano wa Jamii wa DAWASA Bi. Neli Msuya (kulia) akielezea ramani ya mradi wa visima vya jumuiya ya watumia maji pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) akimsikiliza Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumiaji wa Maji Domu Rosemary Kasongo (kushoto) wakati akielezea maendeleo ya mradi wa usambazaji wa maji pembezoni mwa jijini la Dar es Salaam
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa maagizo kwa Jumuiya za watumia maji kuwaunganishia wananchi kwa Mkopo na walipe ndani ya miezi sita hadi mwaka pamoja na wamiliki wa visima binafsi wanaotoa huduma ya maji kwa jamii kujisajili ili wapatiwe vyeti vya ubora wa maji yao.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akimsikiliza Mwenyekiti wa jumuiya wa watumiaji maji Juwabire Khatibu Mzee changamoto za uendeshaji wa miradi ya visima vya jamii.
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam amewaagiza Jumuiya za watumia maji Kuwaunganishia maji wananchi kwa Mkopo na walipe ndani ya miezi sita hadi mwaka.
Ametoa maagizo hayo leo wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya pembezoni inayohudumia wananchi ambao hawapo kwenye mtandao wa DAWASA.
Akizungumza baada ya kutembelea miradi ya jumuiya za watumia majii na namna wanavyotoa huduma ya maji kwa wananchi Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa, angependa kuona wananchi wengi wanahudumiwa na jumuiya hizo hiyo amewaagiza waendelee na mchakato wa kuwaunganishia maji kwa njia ya mkopo wa miezi sita hadi mwaka mmoja.
Luhemeja amesema, mbali na kuwaunganishia maji wananchi kwa mkopo pia wapunguze bei ya maji na kufikia bei elekezi 1663 kwa Ujazo wa Lita 1000 ili kuwa na uwiano sawa wa bei za maji kwa wateja wote.
“Kwa sasa hivi huduma za Jumuiya ya watumia maji zote zitakuwa chini ya DAWASA, kwahiyo tunawataka bei za maji ziweze kupungua tunafahamu kuna changamoto zinawakabili ila tutakaa chini kati ya idara inayosimamia miradi yenu na jumuiya ili kuweza kuweka kila kitu sawa wananchi wapate maji kwa bei elekezi,”amesema Luhemeja.
Amesema kwa sasa wanaendelea kuvipitia visima vyote vilivyopo kwenye jumuiya za watumia maji ambazo vilijengwa na Dawasa, serikali, wadau wa maendeleo mbalimbali na jamii yenyewe na kukagua ubora wa maji ikiwemo na kujenga Water Treatment Plant kwa ajili ya kuweka maji dawa.
Luhemeja ameeleza kuwa, wateja wote waliounganishwa kwenye miradi hiyo jamii wataingizwa kwenye mfumo wa malipo wa Kieletroniki na watalipia kupitia mitandao ya simu ili kuboresha mapato ya kila mwezi.
Aidha, ametoa rai kwa wamiliki wote wenye visima binafsi na wanaofanya kazi ya kusambaza huduma ya maji kwa wananchi wafike kwa ajili ya kusajiliwa na maji yao kupimwa kuangalia ubora kama yanafaa kwa matumizi ya binadamu ikiwemo na kuuza maji kwa bei elekezi ya Ewura ya 1663.
Katika Ziara hiyo Luhemeja ametembelea miradi ya jumuiya mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya watumia maji ya Domu ambapo inatoa huduma kwa wateja 520 wa Kata ya Makangarawe, mradi wa jumuiya ya watumia maji wa Juwabire ukihudumia watu wa Biblia na Relini wakitoa huduma kwa wateja 420 waliounganishiwa sawa na watumia maji 25,000 wakizalisha lita 200,000 kwa siku na mahitaji halisi yakiwa lita 300,000.
Mbali na huo pia ametembelea mradi wa Mzinga A na B ambapo wote kwa pamoja amezitaka jumuiya hizo kutanua mtandao wao kaa kuwaunganishia wananchi wengi wanaotaka huduma ya maji, kuboresha maisha ya wafanyakazi na kingine kuongeza uwezo wa utendaji kazi wa kila siku.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji ya Juwabire Khatibu Mzee na Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji ya Domu Rosemary Kasongo wote wamesema kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo ni umeme kwa kuwa hawana standby generator kwa ajili ya kuliwasha pindi umeme unapokatika na kupelekea wananchi wakose maji kwa muda huo kwani wao huduma zao wanazitoa masaa 24.
Changamoto nyingine ni wateja kuchelewesha ulipaji wa bili za maji na kupelekea uendeshaji kuwa mgumu kwani wanategemea fedha hizo kuendeshea miundo mbinu ya maji na upotevu wa maji. Kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam inapata maji kwa asilimia 85 walitumia vyanzo vya Mto Ruvu, Mto Kizinga na visima na matarajio ni kufika asilimia 95 ifikapo June 2020.
Social Plugin