Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAWILI WAKAMATWA, MMOJA AFUTIWA MKATABA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA KALAMBO


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mwenye rainboot za kijani) akitoa maagizo kwa timu ya wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ikiongozwa na Mkurugenzi mtendaji Msongela Palela (kulia) pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Julieth Binyura (kushoto).Picha na  Peter Kapola 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele) alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa majengo saba ya hospitali ya Wilaya ya kalambo iliyopo Matai mjini ambapo ndiyo makao makuu ya wilaya hiyo. 
Jengo la Mionzi (X - Ray) linaloendelea kujengwa katika hospitali ya Wilaya ya Kalambo. 
Sehemu ya Jengo la Wodi ya akinamama ikiendelea kujengwa katika hospitali ya Wilaya ya Kalambo. 
****
Na Peter Kapola - Rukwa 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kusitisha mkataba na fundi anayehusika na ujenzi wa jengo la maabara katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalambo huku akimtaka Mkurugenzi huyo kutafuta chumba katika eneo hilo ili asimamie kwa karibu ujenzi unaoendelea na kuhakikisha unaisha kwa wakati.

Ametoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Suleiman Jafo hivi karibuni baada ya kuitaka mikoa yote kusimamia ujenzi wa hospitali za wilaya na kufikia tarehe 13 hadi 25 Mei, 2019 majengo yote yawe yameshapauliwa na mikoa hiyo kutuma picha za majengo saba ya hospitali hizo.

Kwa kutekeleza hayo Mh. Wangabo amewaagiza mafundi wote wanaosimamia ujenzi wa majengo hayo saba kuhakikisha wanafikia usawa wa linta ifikapo tarehe 10 mwezi Mei mwaka huu na hatimae kumalizika kwa wakati.

Mh. Wangabo ameyasema hayo alipotembelea eneo la ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kalambo na kukutana na wataalamu wa halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Msongela Palela pamoja na mafundi waliopewa mkataba kwaajili ya ujenzi wa hospitali.

Baada ya kutembelea alisema kuwa hakuridhishwa na kasi ya ujenzi wa hospitali hiyo ya Wilaya ya Kalambo kwakua kasi ni ndogo pamoja na kujua kuwa kulikuwa na changamoto nyingi hasa kipindi cha mvua ambapo barabara zilikuwa hazipitiki hivyo vifaa mbalimbali kushindwa kufika kwenye eneo la ujenzi na kutahadharisha kuwa sasa mvua zimeisha hivyo hakuna sababu ya kuendelea na kasi ile iliyokuwepo.

“Lakini pia nimegundua kuwa kuna wajenzi wengine hata ‘saiti’ hawapo na ujenzi wa majengo yao unasuasua, sasa yule mjenzi wa maabara kule Mkurugenzi sitisha mkataba wake mara moja na utafute mjenzi mwengine ambaye ataleta mafundi wengi na hili jambo lichukue muda mfupi iwezekanavyo ili tarehe 10 mwezi Mei majengo yote haya saba yawe yamefika kwenye hatua ya linta na sio vinginevyo,” alisisitiza. 

Halikadhalika, alisikiliza kilio cha vibarua wanaoendelea na ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo na kugundua kuwa kuna kusuasua kwa malipo ya vibarua hao na hivyo kumuagiza Kamanda wa polisi wa Wilaya hiyo kuwakamata fundi anayehusika na ujenzi wa jengo la utawala Fadhili Salum pamoja na msaidizi wake Amir Rajabu kwa kushindwa kuwalipa vibarua wao tangu ujenzi huo uanze mwanzoni mwaka huu na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kufuatilia malipo ya vibarua hao kwa karibu ili wasiharibu kazi.

Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 105 kwa wilaya 67 kwaajili ya utekelezaji wa ujenzi wa hospitali za wilaya ambapo kila Wilaya ilipewa Shilingi bilioni 1.5 kwaajili ya ujenzi wa majengo saba ya hospitali hizo ambapo mwisho wa ujenzi huo na majengo hayo kuanza kutumika ni tarehe 30 June, 2019.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com