Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema endapo wananchi wanyonge hawatatendewa haki, kuna hatari ya nchi kuingia kwenye machafuko yanayoendelea kutoka katika nchi nyingine za Afrika.
Alikuwa akirejea machafuko yaliyosambaa katika nchi za kiarabu hasa Tunisia na Libya na kusababisha viongozi wao kuondolewa madarakani.
Pia vuguvugu jipya limeibuka katika nchi nyingine za Sudan, ambako maandamano ya amani yamemuondoa Rais Omar al Bashir na Algeria ambako kiongozi wa muda mrefu, Abdelaziz Bouteflika aliondolewa pia kutokana na maandamano ya amani ya wananchi.
Jana, akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (Mviwata) kwa ajili ya kumbukumbu ya Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Sokoine mjini Morogoro, Dk Bashiru alisema bila ya kusimamia misingi ya haki na usawa, nchi haiwezi kuepuka yanayoendelea katika nchi hizo.
Huku akitoa mfano wa madereva wa bodaboda, Dk Bashiru alisema wamekuwa wakinyanyaswa na polisi, jambo alilosema linaweza kuchochea machafuko aliyoyafananisha na yaliyotokea nchini Tunisia mwaka 2011.
“Ndiyo maana mnaona mrundikano wa pikipiki kwenye vituo vya polisi na maeneo mengine,” alisema.
“Kwa hiyo akienda kwa kosa la Sh22,000 ili akomboe pikipiki tena ya mkopo, anakuta bili ya Sh104,000. Lakini mimi nikikamatwa polisi ananiambia utalipa baada ya siku saba, siyo pikipiki.
“Kwa nini kosa la pikipiki ni sawa na kosa la lori na ukikosa unalipa Sh30,000? Nijibuje mimi? Kwa nini kosa la lori anapewa muda wa kulipa sisi tunawekwa ndani? Katika nchi ile ile na sheria zile zile?
“Unajibuje huku umeahidi chama cha kutenda haki, Rais wa wanyonge? Wanakuangalia wanakuona tapeli. Ndiyo mwanzo wa nchi kuingia kwenye machafuko.”
Credit:Mwananchi
Social Plugin