Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kigoma Dansani Shayo akizungumza na Waandishi wa habari ,kulia ni Katibu wa Vijana UVCCM Kigoma, kushoto ni katibu wa CCM Wilaya ya Kibondo, Stanley Mkandawile.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma kimewataka Wanasiasa wanaokichafua chama hicho ili kujipatia umaarufu kuacha mara moja tabia hiyo akidai wapo baadhi ya wanasiasa wanawadanganya wananchi kwa kukituhumu chama hicho ili waweze kuonewa huruma.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kigoma Dansani Shayo alisema kuna baadhi ya maneno yanasemwa na Wanasiasa akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe kwamba chama hicho kimewaaambia viongozi wa serikali kwamba wasilete maendeleo Kigoma.
Alisema chama hicho hakijawahi kuzuia maendeleo kuletwa Kigoma, kwa kuwa chama hicho kinatekeleza Ilani ya CCM na serikali inayotekeleza miradi yote Kigoma na maeneo mengi ni ya chama hicho hivyo hawawezi kushindwa kutekeleza miradi au kuizuia serikali kuleta maendeleo Kigoma kwa kuwa Watanzania wote ni wamoja.
Alisema katika mkutano wa Chama cha ACT wazalendo kilichofanyika Aprili 1 mwaka huu, Kiongozi wa Chama hicho na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe, alisema kwamba kamati ya siasa ya Kigoma mjini ilipokaa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walimwambia kwamba wasilete maendeleo katika jimbo hilo ikiwa ni pamoja na kuboresha zao la mchikichi Kigoma jambo ambalo ni la uongo na la upotoshwaji wa wananchi.
Alisema kama wanasiasa hao na Kiongozi huyo anataka kufanya Siasa, asifanye siasa za kusema uongo ili aweze kuonewa huruma na kujipatia ujiko isipokuwa ajipange na kuongelea ni nini amefanya katika kipindi ambacho alikuwa kiongozi wa jimbo hilo.
"Mpaka sasa kuna miradi mingi imeletwa na serikali ikiwemo mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa katika manispaa hiyo pamoja na barabara za manispaa ni fedha zilizoletwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kila siku Zitto anatembea nchi mbalimbali lakini mpaka sasa hakuna mradi wowote au aonyeshe wawekezaji aliowaleta kuleta maendeleo katika jimbo hilo", alisema Shayo.
Alisema kwa sasa chama hicho kimejipanga kuhakikisha wanashinda kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa kwa kuwa wananchi wana imani na serikali iliyopo madarakani na viongozi wake wanajiamini kwa kazi wanayoyafanya na kazi zilizofanywa na chama hicho.
Aidha Shayo alisema kwa sasa viongozi waliopo katika madaraka wa upinzani wajipange kuondoka kwa kuwa kwa sasa wananchi hawataki kudanganywa wanajiamini na wanajua nini wanafanya.
Social Plugin