Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na Radio Kwizera Shaaban Ndyamukama amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, akiwa jijini Mwanza.
Ndyamukama aliyekuwa akiandikia wilayani Ngara mkoa wa Kagera amefikwa na mauti akiwa Mwanza ambako alikuwa akihudhuria mafunzo ya uandishi wa habari za haki za binadamu zilizokuwa zikitolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Akizungumza leo Jumamosi Aprili 6, 2019 na Mwananchi, Hassan Yusuf ambaye ni mkwewe, amesema afya ya Shaaban ilibadilika jana usiku na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu lakini akafikwa na mauti wakati akiendelea kupatiwa huduma.
“Alikuwa akilalamikia maumivu ya kichwa, uchovu wa mwili na kichefuchefu. Ilipofika usiku hali yake ilibadilika na tukamkimbiza hospitali lakini juhudi za kuokoa maisha yake zilishindikana. Madaktari wanasema amefariki kwa tatizo la shinikizo la damu,” amesema Yusuf.
Mratibu wa MCL inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, MwanaSpoti na MCL Digital, Kanda ya Ziwa, Peter Saramba amesema kuanzia Jumatano ya Aprili 3, 2019, Shaaban alikuwa akitumia dawa za Malaria baada ya kupimwa na kukutwa na vimelea vya ugonjwa huo.
“Kweli maisha ya binadamu ni fumbo lisilofumbuka kwa akili za kibinadamu; siyo rahisi kuamini kuwa Shaaban tuliyekuwa pamoja tukitaniana na kucheka siku mbili zilizopita tayari amebadilika jina na kuitwa marehemu,” amesema Saramba.
Amesema ingawa alikuwa akilalamikia udhaifu wa mwili kiafya, bado alikuwa imara na mchangamfu na haikuwa rahisi yeyote kuhisi alikuwa katika siku zake za mwisho duniani.
“Siku zote za mafunzo alikuwa mchangamfu na imara kiasi cha kuwaimbisha washiriki wenzake nyakati za mchana walipoonyesha kuchoka; hata aliposhauriwa kwenda kupumzika baada ya kuanza kutumia dawa za Malaria, Shaaban hakukubali kirahisi alisisitiza kuendelea na mafunzo,” amesema Saramba.
Amesema mwili wa Shaban umehifadhiwa Hospitali ya Sekou Toure na taratibu zinaendelea za kuhitimisha safari yake ya mwisho hapa duniani.
Mmoja wa watoa mada katika mafunzo hayo kutoka LHRC, Frida Eligius amesema taarifa za kifo cha Shaaban zimemshtua kutokana na jinsi alivyokuwa imara na asiyeonyesha kuzidiwa hata alipokuwa akiumwa wakati wa mafunzo.
Kauli kama hiyo pia ilitolewa na mkufunzi mwingine kutoka LHRC, Tito Magoti aliyeongeza, “Siyo rahisi kupokea na kukubali ukweli kwamba Shaaban hatunaye tena duniani. Ni taarifa za kushtua na kusikitisha sana.”
Mhariri wa Habari wa gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka anasema, “Ni pigo kwa kampuni, tumepoteza jembe, Shaaban alikuwa ni mtu aliyejituma sana na hata ukimpigia simu unahitaji habari fulani haraka alikwenda kuitafuta bila shida.
“Tutakumbuka pia kuwa Shaaban ndiye aliyeandika habari ya mtoto Antony aliyemzuia baba yake asiuze shamba, habari ambayo ilivuta hisia za watu wengi,” anasema Timbuka na kuongeza kuwa:
“Hatuna maneno mengi ya kusema, mapenzi ya Mungu yametimizwa, tuzidi kumwombea na tuzidi kuiombea familia yake ambayo inapita katika kipindi kigumu kisichoelezeka.”