Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro
Kikosi Kazi cha CARD kwa kushirikiana na Mshauri wa CARD, kimeagizwa kuandaa rasimu ya awali ya mkakati wa kuendeleza zao la mpunga nchini mapema kabla ya June, 2019.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe leo tarehe 24 Aprili 2019 wakati wa kikao cha kazi cha maandalizi ya uandaaji wa Mpango mkakati wa pili wa kuendeleza uzalishaji wa zao la Mpunga nchini (National Rice Development Stratergy II - NRDS II) kilichofanyika katika Hoteli ya Edema Mkoani Morogoro.
Alisema kuwa ili kikamilishe hiyo kazi lazima kuwe na takwimu sahihi zinazoonyesha hali halisi ya uzalishaji wa mpunga nchini. ” Ni lazima kutoa takwimu zenye uhakika zitakazowezesha mpango wa pili wa kuendeleza zao la mpunga kukamilika ipasavyo, Timizeni wajibu wenu mliopewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais wetu mpendwa, Mhe Dr. John Pombe Joseph Magufuli” Alikaririwa Mhandisi Mtigumwe
Alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwa takwimu hizo kikosi kazi hicho kitaanza kuandika rasimu ya mpango mkakati wa kuendeleza zao la mpunga, awamu ya pili kwa kuzingatia kuwa CARD wameazimia kuongeza uzalishaji mara mbili zaidi hivyo Tanzania inapaswa kuzalisha mara mbili zaidi ya mwaka jana.
Alilitaja lengo kuu la Mpango Mkakati wa Tanzania katika uzalishaji wa zao la Mpunga nchini, kuwa litakuwa ni kuzalisha kutoka tani 2,219,628 za sasa na kufikia tani 4,500,000 ifikapo mwaka 2030.
Mhandisi Mtigumwe alisema kuwa Mpango mkakati wa kuendeleza zao la Mpunga unaandaliwa kwa kushirikiana na "Coallition for African Rice Development" (CARD), ambapo makao makuu yake yako Nairobi, nchini KENYA. Tanzania ni moja kati ya chi 32 ambazo ni wanachama.
Pamoja na CARD kumaliza kipindi cha awamu ya kwanza, mwaka 2018, nchi wanachama pamoja na wafadhili walikutana Octoba 2018 huko Tokyo, Japan ambapo walifanya tathmini ya awamu ya kwanza na ilionyesha kuwa lengo lilifikiwa.
Aidha, walikubaliana kuanzisha awamu ya pili ya CARD, kuanzia 2018 hadi 2030. Awamu hii inatarajiwa kuzinduliwa nchini Japan, mwezi wa Agosti, 2019. Moja ya jambo muhimu na linalozingatiwa ili kila nchi ipate nafasi ya kupata miradi itakayonufaika na CARD, ni kuwa na Mpango Mkakati wa Kuendeleza zao la Mpunga Awamu ya Pili (2018-2030). Lengo kuu la CARD, awamu ya pili ni kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani 28 milioni (zilizofikiwa katika awamu ya kwanza mwaka 2018) hadi tani 56 milioni mwaka 2030 kwa nchi zote wanachama.
Mtigumwe alisema kuwa kama ilivyofanyika kwa nchi nyingine, na kwa kuzingatia kwamba zao la mpunga ni mojawapo ya zao muhimu la chakula na biashara linalozalishwa takribani mikoa yote hapa nchini, mwaka 2008 Wizara ya Kilimo iliandaa pia Mpango Mkakati wa Kuendeleza zao la Mpunga (NRDS I). Mpango huo ulikuwa ni wa miaka 10 na ulikamilika mwaka 2018 ambapo ulitoa matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa mpunga kutoka tani 899,000 mwaka 2008 hadi tani 2,219,628 mwaka 2018.
CARD ni Muungano wa Wabia ambao hupokea maandiko mbalimbali ya miradi ya uzalishaji na usindikaji wa mpunga na kuyatafutia fedha kwa ajili ya utekelezaji, na huongozwa na Sekretariati ya CARD, iliyoundwa na Wabia wanachama. Hadi sasa kuna Wabia 23. Miongoni mwa Wabia hao, kama alivyokwishawataja Mkurugenzi ni JICA, Benki Kuu ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika na wengineo.