Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara amesema kuanzia jana Jumatatu Aprili 15, 2019 wizara hiyo imehamia hivyo hivyo katika jengo la ofisi yake ‘pagale’ ambayo haijakamilika kama ilivyoagizwa na Rais John Magufuli.
Waitara ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 16, 2019 nje ya viwanja vya Bunge jijini Dodoma ikiwa zimepita siku tatu tangu Rais Magufuli atoe agizo hilo akizindua mji wa Serikali jijini Dodoma.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi alitoa agizo hilo ikiwa ni muda mfupi baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kueleza kuwa alikuwa na makubaliano na mawaziri kuwa siku majengo hayo yakizinduliwa wangehamia.
Majaliwa alimweleza Rais Magufuli kuwa kuna baadhi ya wizara ikiwamo Tamisemi ambazo majengo yao yamechelewa kukamilika kutokana na kuchelewa kupata fedha.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema hataki kusikia kunakuwa na kisingizio cha majengo mengine kuwa hayajakamilika badala yake, kama mtu ameshindwa akae hata chini ya mwembe ilmradi awe Mtumba ambako ndiko mji wa Serikali ulipo.
Rais Magufuli alisema muda wote atakapokuwa anawahitaji mawaziri, hakuna sababu ya kuwaita bali atawafuata kwenye majengo hayo hivyo akaomba kila mmoja ahamie kwa vitendo siyo maneno.
Akizungumzia agizo hilo Waitara amesema: “Mbona tumeshahamia tangu jana kwa mujibu wa maelekezo, ofisi ipo vizuri na nyaraka zipo katika ofisi zetu za awali.”
“Waziri, naibu waziri, naibu katibu mkuu na katibu mkuu wapo kule kukihitajika nyaraka zinaletwa pale. Tumetengeneza ofisi za muda. Tupo katika mazingira ya kumaliza (ujenzi wa ofisi hizo) na itakwenda mwezi mpaka mwezi mmoja na nusu, uzuri pale hatujengi upya tunamalizia tu ujenzi,” amesisitiza Waitara.
Leo Jumanne Aprili 16, 2019 Mwananchi lilifika katika ofisi hizo na kushuhudia viti vichache vikiwa vimewekwa katika banda la bati, huku baadhi ya watendaji waliokuwa katika magari mawili wafika eneo hilo na kutoa maelekezo na kuondoka.
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Social Plugin