Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAMLAKA YA MAJI TARIME YAZINDUA BODI YA MAJI

Na Dinna Maningo,Tarime.

Mamlaka ya Maji Mjini Tarime imezindua Bodi ya maji yenye wajumbe 7 lengo likiwa kushirikiana na kutoa mawazo yao katika kushughulikia maswala ya maji ili kuhakikisha changamoto za maji zinatatuliwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo Kaimu Meneja wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira katika Mji wa Tarime Passian Martin alisema kuwa kwa miaka 6 mamlaka hiyo imekuwa ikifanya kazi bila bodi ya maji tangu mwaka 2012,nakwamba kuanzishwa kwake kutaongeza ufanisi wa kazi.

"Miaka yote hiyo mamlaka ilijiendesha yenyewe hivyo kukawa na changamoto katika maamuzi kwakuwa sasa tuna bodi mtatusaidia mambo mengi yanayohusu mamlaka ya maji",alisema Martin.

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Moses Marwa alisema bodi hiyo ina wajumbe ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Elias Ntirihungwa,Calvin Mwasha ambaye ni Mganga Mkuu halmashauri hiyo,Rose Hosea,Agnes Mwita,Diwani wa Kata ya Nyandoto Sinda Sabega, na Kaimu Meneja wa mamlaka ya Maji Passian Martin.

Pia Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Bodi waliunda kamati 2,Kamati ya fedha yenye wajumbe 4 Mwenyekiti Calvin Mwasha,Katibu Passian Martin, Elias Ntirihungwa na Rose Hosea,Kamati ya nidhamu yenye wajumbe 2 Mwenyekiti Sinda Sabega na Katibu Agnes Mwita.

Aliongeza kuwa bodi hiyo itakutana Mara moja kila baada ya miezi 3, kamati ya fedha itakutana Mara moja kila mwezi na kamati ya nidhamu itakutana mara moja kila baada ya miezi 3 na punde kunapotokea dharura.

Kaimu Meneja wa Maji alitaja majukumu ya Bodi ikiwa ni pamoja na kusimamia shughuli za mamlaka ya maji, kupitisha Bajeti ya fedha,kusimamia Vitabu vya kumbukumbu na uwasilishaji wa taarifa katika ngazi husika.

Wakichangia mjadala Wajumbe wa Bodi akiwemo Calvin Mwasha alihoji..."Mamlaka ina watumishi 18 na wengi wao ni vibarua je mamlaka ina mkakati gani wa kuwaajili?lakini pia tumekuwa tukiona miradi mikubwa ya maji kwenye wilaya zingine kama Bunda,Kilimanjaro je ni lini Tarime tutapata mradi mkubwa wa maji?tunateseka sana maji tunatumia maji ya mtoni na si safi na salama ni machafu hayafai ni hatari kwa Afya za watu" alisema.


Kaimu Meneja alijibu..."Tayari tulishatuma majina Wizarani ili taratibu za ajira zifanyike tunasubiri,pia tulishaandika maandiko mengi yakuomba mradi hatujapata tukituma Wizarani tunaambiwa tupitie Mamlaka ya maji Mkoa nako maandiko yanakwama kwakuwa tuna bodi tutashauriana cha kufanya",alisema Martin.

Kaimu Mhandisi wa maji halmashauri ya Mji Tarime Laurent Mganga alisema kuwa kupitia Wizara ya maji iliwajulisha kuwa tayali kuna mradi mkubwa wa maji Tarime,hata hivyo hawajaelezwa mradi huo utaanza lini nawanapoulizia uambiwa waendelee kuwa wavumilivu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com