Na Dinna Maningo -Tarime.
Baadhi ya wananchi mjini Tarime wamekuwa hawalipi ankra za maji kwa wakati huku Taasisi za Umma zikiwa zinaongoza kwa madeni yenye jumla ya Milioni 13,092,625.50 deni la Mwezi mmoja jambo linalokwamisha utendaji wa Mamlaka ya maji.
Akizungumza kwenye kikao cha uzinduzi wa Bodi ya maji mjini Tarime Meneja wa Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira katika Mji wa Tarime Passian Martin alisema kuwa deni hilo ni la mwezi Machi, 2019.
Martin alizitaja Taasisi hizo za Umma kuwa ni Jeshi la Magereza linadaiwa Milioni 5,311,131.00,Tarime Teachers Collage (TTC) inadaiwa kiasi cha Milioni 1,046,005.00,Hospital ya Halmashauri ya Mji wa Tarime Million 4,178,431.00,Tarime Sekondari Laki 148,874.00, 27 KJ-Rest House 204,300.00, 27 KJ 100,635.00.
Zingine ni RPC (Tarime/Rorya) 69,574.00, RPC Tarime - Police Line 436,017.00, RPC Tarime- Canteen 660,734.00, RPC Tarime-Kikosi cha Mbwa 316,671.50, S/M Buhemba Mazoezi 80,175.00, NTC Tarime 228,078.00,Bomani Sekondari 210,000.00 na TTC Rest House 102,000.00.
Martin aliongeza kuwa mbali na madeni hayo Mamlaka ya maji inakabiliwa na changamoto zikiwemo za kutokuwa na dira za maji kwa zaidi ya 40% ya wateja waliounganishiwa maji,hivyo gharama za malipo kutoendana na matumizi halisi ya maji.
"Tukifuatilia madeni tunaambiwa wanategemea pesa kutoka hazina sasa utakatia hospitali maji!pia hatuna mfumo wa kielectroniki utakaowezesha kutoa Ankra kwa wakati na kuongeza uwezo wa kukusanya mapato,mfumo wa Umeme uliopo ni Luku,hivyo Mamlaka kulazimika kununua umeme kila mara kwa gharama kubwa tofauti na mwongozo unavyosema gharama za umeme zitalipwa na Wizara ya Maji",alisema.
Martin alisema kuwa Mamlaka hiyo inakabiliwa na ukosefu wa chanzo cha maji cha kudumu ili kutosheleza mahitaji na mita kuchafuka kutokana na kutokuwepo ubora wa maji hivyo kufanya usomaji wa mita kuwa mgumu.
Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu Bodi ya maji Sinda Sabega ambaye ni Diwani Kata ya Nyandoto (CCM) aliitaka Mamlaka kuzipa Taasisi muda wa siku 14 ziwe zimelipa madeni vinginevyo zikatiwe huduma ya Maji huku akiitaka Mamlaka kutoa orodha ya madeni ya Wananchi ili iwe rahisi kufatilia.
Mwenyekiti wa kamati ya Fedha Bodi ya maji Calvin Mwasha ambaye ni Mganga mkuu wa Halmashauri ya mji wa Tarime yeye aliahidi wiki mbili deni la hospitali litakuwa limelipwa kwakile alichosema hawezi kuwa mjumbe wa bodi halafu hospitali idaiwe .
Mjumbe wa Bodi Rose Hosea aliwataka wajumbe kuwa kwa kuwa tayali bodi imeundwa ambayo haikuwepo kwa miaka 6 ni vyema ikaonyesha jitihada madhubuti kuhakikisha Taasisi hizo zinalipa na siyo kuonewa huruma huku Mwenyekiti wa Bodi Moses Marwa akiahidi bodi hiyo kuwa itahakikisha inasimamia masuala ya maji.